Naibu Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amezisisitiza Taasisi mbalimbali nchini kutoa nafasi kwa Watumishi wao kushiriki katika michezo ili kuimarisha afya zao.
Naibu Waziri Gekul amesema hayo Juni 30, 2021 Jijini Dodoma alipokuwa mgeni rasmi katika fainali za Mshindano ya Mpira wa Netiboli kwa Mkoa wa Dodoma yaliyoandaliwa na Chama cha Netiboli mkoani humo.
“Watumishi wakishiriki katika michezo itawajengea afya, urafiki, ushirikiano, amani, upendo na furaha pia, jambo hili ni kubwa kwa kuwa litawajengea mazingira wafanyakazi hao kutumikia vizuri majukumu yao”, amesema Naibu Waziri Gekul.
Aidha Naibu Waziri Gekul amesema kupitia Bajeti ya Mwaka 2021/ 2022 tayari kuna mkakati wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Michezo ambapo fedha zitakazopatikana zitatumika kutatua changamoto zinazokabili uendeshaji wa michezo ikiwemo mchezo wa Netiboli.
Awali katika risala ya chama hicho zimetajwa changamoto kadhaa ikiwemo uhaba wa fedha za Chama hicho kujiendesha, kukosekana kwa ofisi rasmi za chama na pia ukosefu wa viwanja vya mchezo wa Netiboli kwa Mkoa wa Dodoma ambazo Serikali imezipokea na kuonesha dhamira ya kuzishughulikia.
Katika mashindano hayo Timu ya TAMISEMI Dodoma imeibuka mshindi wa kwanza huku nafasi ya pili ikishikwa na timu ya Kongwa DC na nafasi ya tatu ikichukuliwa na Ihumwa Dodoma.
Mashindano hayo yamejumuisha jumla ya timu kumi ambazo ni TAMISEMI (Dodoma), Kongwa DC, Vijana (Dodoma), Ihumwa (Dodoma), Benjamin Mkapa Hospitali (Dodoma), Chuo Kikuu cha Kampala (Dar es Salaam), Wazalendo (Wanawake, Zanzibar), Wazalendo (Wanaume, Zanzibar), Muungano (Dodoma) na Bright (Dodoma).
By Mpekuzi
Post a Comment