NFRA YAJA NA MPANGO WA KUONGEZA UWEZO WA KUHIFADHI CHAKULA |Shamteeblog.

Na Zainab Nyamka,Michuzi TV

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imejipanga katika kuhakikisha inaongeza uwezo wake wa kuhifadhi mazao yake kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000.

Hatua hiyo ni katika kuongeza wigo wake wa kuhifadhi nafaka kwenye maghala ili yatumike pale yanapohitajika.

Akizingumza wakati wa maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba, Afisa Uhusiano wa NFRA Angela Shangali amesema wapo katika hatua za mwisho za kuongeza wigo wa uhifadhi wa mazao yao ambapo yataongeza uwezo mkubwa wa kuyahifadhi.

“ lengo la serikali ni kuongeza wigo wa kuhifadhi hadi tani 501,000 kufikia mwaka 2025/2026 kwa kujenga miundo mbinu ya kisasa, kukarabati na kuimarisha maghala yake pamoja na njia sahihi ya  kuhifadhi mazao,” amesema

Shangali amesema, maghala hayo yatakuwa katika Kanda ya Arusha maeneo ya Manyara ambapo itahakikisha uhakika wa usalama wa chakula.

Amesema, lengo kuu la Wakala ni kuona serikali inajijengea uhakika wa chakula na heshima kwa mataifa mengine.

“Utekelezaji wa mpango mkakati wa wakala kupitia mpango wa uwekezaji utaboresha miundo mbinu ya wakala, kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka na kuwezesha matumizi ya teknolojia za kisasa katika uhifadhi wa mazao,” amesema.

Shangali amesema, dhima ya NFRA ni kuona upatikanaji wa akiba ya chakula cha kimkakati wakati wa upungufu wa chakula kwa kununua, kuhifadhi, kuzungusha na kuuza chakula kwa ufanisi na kwa manufaa ya jamii.

Amesema, wakala inahusika na utoaji wa chakula kwa waathirika au upungufu wa chakula kutokana na majanga mbalimbali kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na idara ya maafa Chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Aidha, NFRA pia inahusika na uuzaji nafaka kwa wasagishaji kwa madhumuni ya kuongeza upatikanaji wa nafaka katika masoko pale inapohitajika.

Shangali ameongeza kuwa, wakala imedhamiria kuongeza wigo wa kuhifadhi ili kukidhi mahitaji ya uhifadhi kitaifa kama yalivyobainishwa katika MKUKUTA   2 yanayotaka walala kuhifadhi chakula cha dharura ya kitaifa angalau kwa miezi minne.

“Utekelezaji wa adhma hii utatoa fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii ambazo zitanufaisha wananchi mbalimbali katika kuelekea Tanzania ya Uchumi wa Viwanda,”amesema Shangali.

Amongezea  na kusema, kwa sasa wakala wa Taifa  wa Hifadhi ya chakula wanauza nafaka ambazo ni mtama, mpunga na mahindi.

Kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo wanaohitaji kupata huduma ya ununuzi wa nafaka wafike katika ofisi za Kanda zilizopo nchini au Makao Makuu ya NFRA Dodoma , pia wanaweza kuwasiliana kwa barua pepe info@nfra.go.tz na wavuti www.nfra.go.tz

Moja ya maghala yatakayozinduliwa Mkoani Manyara kwa ajili ya kuongeza wigo wa uwekaji wa akiba wa mazao aina ya nafaka unaosimamiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Nchini



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post