Na.Vero Ignatus Arusha.
Wakulima wakubwa kwa wadogo pamoja na wataalamu wa kilimo hapa nchini wametakiwa kuitumia fursa ya maabara ya serikali iliyopo katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania Kituo cha TARI TENGERU ili waweze kupima na kutambua magonjwa na kupata ushauri wa Uthibiti wa magonjwa na visumbufu vya mimea kwa gharama nafuu.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Kituo hicho Daktari Mpoki Shimwela wakati akizungumza na mwandishi wa Michuzi blog baada ya ukaguzi wa maboresho ya maabara hiyo iliyopo eneo la Tengeru Wilayani Arumeru mkoani Arusha, yaliyofanywa na Wakala wa Majengo ya Serikali Tanzania (TBA) kwa ufadhili wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSITECH).
Ameongeza kuwa lengo la maabara hiyo ni kufikia wakulima wengi ili waweze kutumia matokeo ya tafiti zilizofanywa katika kuzalisha miche, pamoja na vipando vya mimea ya aina nyingi kama vile Vanila, Viazi, mihogo pamoja na migomba
Ambapo mpaka hivi sasa miche ambayo tayari imeshafanyiwa tafiti na kuleta matokeo mazuri ni migomba hususani kipindi chote cha kilimo ili kumuinua mkulima kiuchumi na kufikia malengo yake.
Amesema Taasisi hiyo imejipanga vizuri ili Watanzania waweze kunufaika na maabara hiyo na kwa sasa wameanza kuzalisha zao la migomba peke yake, na kwamba baadaye utawekwa utaratibu ili kuendelea kuzalisha miche mingine ambayo itasaidia kuinua na kukuza kilimo Tanzania.
Amesema mbegu zinazotoka kwenye maabara hiyo zinakuwa na uhakika wa usafi na kutokuwa na magonjwa na wadudu hivyo mkulima anapokwenda kupanda shambani kwake ana uhakika wa mbegu anayoipanda na itatoa mazao ya uhakika kwa muda unaohitajika na kumwezesha mkulima kushindana katika soko hususani soko la ndani na nje ya nchi.
Akibainisha changamoto kubwa inayowakumba wakulima Daktari Mpoki amesema wakulima wengi bado hawana uelewa kuhusu huduma za utafiti hasa magonjwa ya mimea hivyo amewashauri kufuatilia utaalamu kutoka kwa watafiti wa kilimo pamoja na maafisa ugani ili waweze kuzalisha kwa tija badala ya mkulima kukimbilia dukani na kutumia kemikali bila kushauriwa na wataalamu hao.
Kwa upande wake Msimamizi na Mratibu wa mradi wa Maboresho ya Maabara hiyo,Mtafiti kutoka katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania Kituo cha TARI TENGERU Bi Fatuma Kiruwa amesema mradi huo umefadhiliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSITECH) ambapo umegharimu shilingi za Kitanzania milioni 399,999,370.
Aidha Mratibu wa Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano TARI-TENGERU Mtafiti Mwandamizi Bwana Peter Joseph amewakaribisha wakulima kufika katika Taasisi hiyo kujionea Miche mbalimbali iliyothibitishwa kiutafiti ikiwemo ile ya parachichi na pia waweze kushirikiana na watafiti wabobezi kujibu kero zao.
Katika Picha ni baadhi ya Miche ya migomba iliyozalishwa maabara ya Kilimo Tanzania Kituo cha TARI TENGERU,miche ya migomba ambayo tayari imeshafanyiwa tafiti na kuleta matokeo mazuri hususani kipindi chote cha kilimo. Kutoka kulia Emmanuel Mlinga, kushoto ni Mnkai Mkondo Kulia ,wakiwa mahabara ambapo mbegu zinazotoka kwenye maabara hiyo zinakuwa na uhakika wa usafi na kutokuwa na magonjwa na wadudu
By Mpekuzi
Post a Comment