Charles James, Michuzi TV
WANA vipaji! Ndivyo unavyoweza kusema kufutia Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Ifunda iliyopo mkoani Iringa kuanzisha mchakato wao wa kutengeneza Roboti Maalum litakalokua linasaidia wakulima kupulizia dawa kwenye mazao yao.
Ubunifu wa utengenezaji wa roboti hilo unafanywa na wanafunzi wawili, Oscar Metwa wa kidato cha sita mchepuo wa PCM na Isaya Faustine wa kidato cha kwanza.
Akizungumzia ubunifu huo, Isaya Faustine wa kidato cha kwanza amesema wamekuja na wazo hilo ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwainua wakulima na sekta ya kilimo kwa ujumla.
Amesema kwa sasa wako kwenye hatua za awali za utengenezaji wa roboti hiyo na wanatarajia kukamilisha ndani ya wiki moja kwani tayari washapata kibali cha kuanza mradi wao huo wa kutenegeneza roboti hilo.
" Wote tunafahamu kilimo ndio uti wa mgongo wa Nchi yetu hivyo sisi kama wabunifu tumeona tuje na kifaa hichi ambacho kitasaidia wakulima kuweza kupuliza dawa kwenye mashamba yao wakiwa majumbani mwao.
Roboti hili tutalitengeneza kwa mfumo wa Gari lakini halitokua na matairi bali minyororo kama vilivyo vifaru vile vya Jeshi, halafu Mkulima atapaswa kuwa na application kwenye simu yake ambapo akitaka kunyunyuzia dawa Mazao yake analipigia simu na lenyewe linafanya kazi hiyo," Amesema Isaya.
Amesema kukamilika kwa kifaa hicho siyo tu kitakua kinaokoa muda wa wakulima lakini pia kitawaepusha wakulima na maradhi ambayo wamekua wakiyapata kutokana na upulizaji wa dawa wanaoufanya kwenye mazao yao," Amesema Isaya.
Kwa upande wake Oscar Metwa ambaye amebuni pia kifaa cha kuzuia madhara yanayosababishwa na umeme ameiomba Serikali kuwatupia macho wabunifu vijana ili nao waweze kutoa mchango wao kwa Taifa lao.
" Mbali ya mpango wetu huu wa Roboti lakini pia nimebuni kifaa hiki cha kuzuia madhara yanayosababishwa na shoti za umeme ambapo tayari kifaa hiki kimefungwa kwenye mojawapo ya mabweni hapa shuleni na kinafanya kazi," Amesema Metwa.
Ametoa wito kwa wanafunzi wenzake nchini kutoogopa masomo ya Sayansi kwa kisingizio cha kwamba ni magumu bali waweke bidii katika kujisomea kwani hakuna somo gumu endapo utaliwekea bidii na kulipenda.
Nae Mkuu wa Shule hiyo, Yusuph Mwagala amesema katika kusapoti vipaji vya wanafunzi wao ambao wamekua wakifanya ubunifu mbalimbali wamekua wakiwaunganisha na Taasisi zinazokuza wabunifu pamoja na Vyuo mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu Cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) pamoja na Chuo Cha DIT kwa ajili ya kujiendeleza zaidi.
" Kama Shule tumekua tukiunga mkono juhudi za vijana wetu wanaofanya tafiti na ubunifu kwa kuwaunganisha na taasisi zinazokuza ubunifu lakini pia kuwaunganisha na Vyuo kama MUST na DIT ambapo kote huko wanaenda kujiendeleza zaidi.
Kuna ubunifu mbalimbali ushafanywa na vijana wetu ikiwemo kutengeneza pampu ya kumwagilia bustani lakini pia ubunifu mwingine ni huu wa kifaa cha kuzuia madhara yanayosababishwa na umeme ambapo kupitia kifaa hiki sasa tunatumia mfumo wa DC na siyo AC ," Amesema Mwalimu Mwagala.
Muonekano wa picha za Shule ya Sekondari ya Ufundi Ifunda iliyopo mkoani Iringa ambapo wanafunzi wake wamebuni teknolojia mbalimbali.
Mwanafunzi Oscar Metwa wa kidato cha sita Shule ya Sekondari ya Ufundi Ifunda Mkoani Iringa akitoa maelezo ya ubunifu wake wa kifaa cha kuzuia madhara yanayosababishwa na umeme ambacho amekibuni mwenyewe.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Ifunda mkoani Iringa, Mwalimu Yusuph Mwagala akizungumza na Wandishi wa Habari juu ya namna ambavyo wao kama Shule wanasaidia kukuza vipaji vya wanafunzi wao.
By Mpekuzi
Post a Comment