Wananchi wa Kitongoji cha Kwebamba,lilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, wamemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuingilia kati mgogoro wa ardhi ambao unazingonganisha Halmashauri mbili za mkoa wa Tanga juu ya umiliki wa eneo ambalo linasemekana limegunduliwa madini ya aina ya silicon.
Kwa mujibu wa wananchi umiliki wa eneo hilo katika kitongoji cha Kwebamba na msitu wa Bumba Mavumbi ambalo nalo limegunduliwa madini unaozigonganisha HalmashaurI Bumbuli na Korogwe umeanza kutishia amani baada ya watu wanaodaiwa kuwa wakazi wa Korogwe kuanza kuwatisha wananchi kwa mapanga pindi wanapowakuta kwenye mashamba yao ambayo wamegawiwa na serikali ya Kijiji chao.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wao wa Kijiji walisema kuwa ramani ya kitongoji hicho inaonyesha kuwa Kwebamba ipo Bumbuli, wilayani Lushoto. Walionyesha kuwashangaa viongozi wa wilaya ya Korogwe kudai kitongoji hicho kuwa kiko katika wilaya yao..
Mzee Athumani Akida (85) ambaye ni mwanzilishi wa kitongoji hicho alisema kuwa hata wataalam kutoka ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2009 walifika katika kitongoji hicho ili kupima eneo hilo na kuweka mawe ya mipaka ‘bikoni’ yanayoonyesha kuwa eneo liko Bumbuli, wilaya ya Lushoto.
Mzee Akida alieleza hofu yake kuwa mgogoro huo unaweza kutishia uvunjifu wa amani hivyo akamuomba Waziri mwenye dhamana ya ardhi afike haraka kutatua mgogoro huo
Mkazi mwingine wa Kwebamba, Yohana Mwavu (73) naye alieleza kushangaa madai ya viongozi wa Korogwe na kusema kama kitongoji hichi kiko kwao kwa nini hakiwapatii huduma zozote za kijamii.
Mzee Mwavu alieleza kwamba huduma zote ambazo hivi sasa wanazipata zinatoka Halmashauri ya Bumbuli. Aliwataka viongozi wa Korogwe waache kudai eneo hilo.
‘’Sisi tunapata huduma zote kutoka katika halmashauri ya Bumbuli. Bumbuli imetulea tangu zamani. Mimi na umri wangu huu nimezaliwa hapa. Kama Korogwe walijua sisi tuko katika halmashauri yao kwa nini hawatupi huduma zozote za kijamii?”, alihoji Mzee Mwavu.
" Mimi nina eka tano nilizopewa na Kijiji chetu cha Kwebamba. Nimelima mwenyewe na vijana wangu watatu,tena bila kualika Ungwe na shamba hili nilikuta ni pori. Baada ya mazao yangu kukomaa nilingiliwa na kundi la watu ambao walidai ni wafanyabiashara kutoka Korogwe ambao walisema sisi ni wavamizi tuwapishe. Sasa tunajiuliza mbona lilivyokuwa pori hawajaja kulima" Alisema Rehema Chamungwana.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Bumba, Afizai Daffa alieleza wao kama Kijiji walianza utaratibu wa kugawa maeneo ya wazi kwa wananchi mwaka jana. Alisema kwa mujibu wa sheria zao lengo lilikiwa kuwapatia wananchi sehemu ya kulima lakini imekuwa mwiba kwao na wamekuwa wakitishiwa na kikundi cha watu wakiambiwa ni wavamizi jambo ambalo amedai kusikitishwa na hali hiyo ya kutishiwa amani kwa wananchi wake hata viongozi wa Kijiji ambao wanatambua wapo hapa kihalali na kwa kwamba wanaitikia Halmashauri ya Bumbuli
Aliyekuwa Diwani wa eneo hilo kwa zaidi ya miaka 15, Hozza Mandia alisema kuwa,ramani inaonyesha kuwa kitongoji cha Kwebamba kiko eneo la Bumbuli. Hivyo, aliwataka Viongozi wa Korogwe kukaa meza moja na viongozi wa Bumbuli ili kumaliza mgogoro huo alioueleza kukosa sura nzuri kwa jamii.
Mandia, ambae pia ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli January Makamba, alisema Halmashauri ya Bumbuli kupitia Mbunge imefanya mambo mengi katika eneo hilo.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kusaidia mabomba ya maji (rola) ,Mabati ,Saruji pamoja na Tsh 5 milioni zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule pamoja na huduma nyingine za kijamii. Aliwataka wananchi hao wasiuze ardhi yao kwa kuwa itakuja kuwasaidia baadae huku akiwa sisitiza wawe watulivu kipindi ambacho wao kama viongozi wanatafuta muafaka wa suala hilo.
Naye Diwani wa Sasa wa kata ya Milingano, Peter Leonard, alisema kuwa kata yake ina vitongoji 22, ikiwemo kitongoji cha Kwebamba na kwamba aligombea akiwa anakitambua kitongoji cha Kwebamba kuwa kiko katika halmashauri ya Bumbuli.
Taarifa zinaonyesha kuwa ramani ya eneo hilo la Kwebamba ambalo sasa limeingia kwenye mgogoro baina ya pande hizo mbili, imechorwa tangu kipindi cha mkoloni.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya Lushoto, kalist Lazalo, amethibitisha kufahamu mgogoro huo na kwamba anajipanga kufika eneo hilo ili kujionea tatizo na kuwasikiliza wananchi. Alisema baada ya kujionea tatizo atalazimika kukutana na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe ili waone namna ya kutafuta suluhu ya mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Basila Mwanukuzi, alisema yeye hana taarifa ya mgogoro huo na kwamba endapo atapata taarifa ya mgogoro huo atalazimika kuandika barua kwa Mkuu wa wilaya ya Lushoto ili waangalie namna ya kutatua na kama itashindikana watalazimika kulipeleka kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adamu Malima.
By Mpekuzi
Post a Comment