WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameiagiza Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kuendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wafugaji ili wafuge kisasa.
Waziri Ndaki ameyasema hayo alipotembelea Kampasi ya Tengeru iliyopo mkoani Arusha kwa lengo la kufungua bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 ambalo litasaidia kupunguza changamoto ya miundombinu iliyopo.
“Wafugaji bado wanahitaji kupatiwa elimu ya ufahamu ili waweze kuelewa faida na hasara za kuendelea na njia ya ufugaji wa asili na njia bora za ufugaji wa kisasa utakaoweza kuwaletea tija ambapo kwa kuwatumia wataalam tunaowafundisha na waliopo katika maeneo mbalimbali tutaweza kubadilisha fikra za wafugaji wetu,” alisema Waziri Ndaki
Pia LITA imetakiwa kusaidia kutatua changamoto ya malisho kwa wafugaji kwa kutoa elimu juu ya umiliki wa maeneo na upandaji malisho. Waziri Ndaki amesema kupitia mashamba yao ya malisho ambayo hutumika kuwafundishia wanafunzi, pia wanaweza kuyatumia mashamba hayo kama mashamba darasa ambapo wafugaji watapata fursa ya kwenda kujifunza.
Aidha, amewashauri Bodi na Viongozi wa LITA kuangalia namna ya kutoa elimu ambayo itawasaidia wahitimu wa vyuo hivyo kwenda kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea kuajiriwa. Hili pia amewaeleza wanafunzi baada ya kufungua bweni la wasichana kuwa ni lazima wasome kwa nguvu wakilenga kujiajiri.
Waziri Ndaki ameipongeza Bodi na Uongozi mzima wa LITA kwa kazi nzuri wanayoifanya ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu kama bweni la wasichana licha ya changamoto walizonazo. Pia amewaahidi kuwa wizara itaendelea kutenga fedha za maendeleo katika bajeti kwa ajili ya kuendelea kutatua changamoto walizonazo zikiwemo za miundombinu, mitambo na vifaa mbalimbali na kwamba wizara itaangalia namna ya kuwasaidia ili kutatua changamoto ya usafiri kwa kununua basi la chuo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya LITA, Prof Malongo Mlozi amesema majukumu ya LITA ni kutoa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya Stashahada na Astashahada, kutoa huduma za ushauri na mafunzo ya muda mfupi kwa wafugaji, maafisa ugani pamoja na wadau wengine katika sekta, kufanya tafiti na huduma za ushauri ili kujitathmini na kuboresha mafunzo yanayotolewa na kuzalisha na kutunza aina mbalimbali za mifugo na malisho bora kwa ajili ya mafunzo na kuhudumia jamii ya watanzania.
Mtendaji Mkuu wa Wakalaya ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo, Dkt. Pius Mwambene amesema wakala imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo ongezeko la udahili kutoka 798 mwaka 2012/13 hadi wanafunzi 3,592 mwaka 2020/21, ongezeko la ufikiaji wafugaji kutoka 267 mwaka 2012/13 hadi 2,104 mwaka 2020/21. Pamoja na mafanikio hayo bado wakala inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za miundombinu, upungufu wa walimu na watumishi wengine, uhaba wa fedha za maendeleo, usafiri, mitambo, lakini pia baadhi ya wanafunzi wasaidiwe kupata fursa ya mikopo.
By Mpekuzi
Post a Comment