Baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu nchini wametangaza mkakati mpya wa madai ya Katiba mpya wa kukusanya saini milioni tano za watu wanaounga mkono madai hayo na kuyapeleka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mkakati huo umekuja kufuatia maazimio kuhusu hali ya haki za binadamu nchini iliyoadhimishwa siku ya Haki za Binadamu duniani Desemba 10 mwaka huu yaliyofanywa na wadau mbalimbali chini ya Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD) na Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata).
Tangu alipoingia madarakani Machi mwaka huu, Rais Samia alishaweka msimamo akitaka apewe muda kwanza aisimamishe nchi kiuchumi, ndipo atajadili masuala ya Katiba na demokrasia, jambo linalokosolewa na wapinzani wake.
Akizungumza leo Desemba 22 jijini hapa kuhusu maazimio ya haki za binadamu, Mwenyekiti wa TCDD, Dk Camillus Kassala alisema miongoni mwa maazimio hayo ni kuwataka Watanzania kuchukua jukumu la kurejesha Taifa lao katika kilele cha kuhifadhi, kulinda na kuendeleza haki za binadamu.
“Tumedhamiria kukusanya saini za Watanzanua milioni tano wanaohitaji Tanzania kuandika Katiba mpya, kisha saini hizo tutaziwasilisha Ikulu ya Magogoni na Chamwino kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan,” alisema Dk Kassala wakati akisoma maazimio hayo.
Naye mwanaharakati na mwanasiasa mkongwe Prince Bagenda alisema suala la Katiba limejadiliwa kwa muda mrefu bila vitendo.
“Tumetoka kwenye ulingo wa kujadili mambo haya kinadharia, tunataka vitendo. Kama tunavyoonyesha kwamba tuwahusishe watu, tunatafuta saini kujaribu kuwaonyesha watawala kwamba hatuko peke yetu tunaoelewa tatizo la nchi yetu, tuko watu milioni tano na zaidi ya hapo,” alisema.
Akizungumzia hali ya siasa nchini, Bagenda amesema miaka mitano iliyoipita nchi ilipita kipindi kigumu, lakini baada ya kupita sasa umefika wasaa wa kuchukua hatua.
“Mimi nina hakika Mama Samia kuna mambo ni mwenzetu na atasikiliza. Sisi tunatumia njia ya kistaarabu, tunakusanya saini kwenda lkumwonyesha. Sio njia ya kuogopesha kama ya maandamano.
“Tunapompelekea ni ujumbe kwamba usione watu wamenyamaza, ukafikiri kila kitu kiko sawa sawa.”
Akifafanua kuhusu maoni ya wanasiasa kuhusu kuboreshwa kwa baadhi ya vipengele vya Katiba na sheria ili kuunda tume huru ya uchaguzi, Bagenda aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa chama cha NCCR Mageuzi, alionya suala hilo akisema litapooteza malengo ya kupata Katiba mpya.
“Itakuwa kosa kubwa kwa watu kukubali kuanza kubadilisha Tume bila kubadilisha Katiba. Kwa sababu unapokwenda una protection (kinga) ya Katiba unakwenda na uhakika kwamba utashindana unarudi nyumbani umeridhika,” amesema Bagenda.
Naye Bubelwa Kaiza kutoka taasisi ya Fordia alisema madai ya Katiba mpya ni mwendelezo wa mradi wa kitaifa wa mabadiliko ya kidemokrasia yaliyoanzishwa na Serikali yenyewe kuanzia mwaka 1990.
“Kuanzia mwaka 1990 Tanzania ilianza kutekeleza mradi wa mabadiliko na demokrasia, mwaka 1991 Serikali iliunda Tume ya Nyalali (Jaji Francis) iliyokuwa sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kitaifa wa mabadiliko ya demokrasia, haki za binadamu, ushindani katika siasa na ustaarabu wa siasa,” amesema Bubelwa.
from Author
Post a Comment