Spika wa Bunge, Job Ndugai
Dar es Salaam. Kuna ishara kubwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai ameumaliza mwaka 2021 vibaya.
Kauli yake kuhusu Serikali kukopa, siyo tu kwamba imepishana na mtazamo wa Rais Samia Suluhu Hassan, bali pia inaonekana kuchafua hali ya hewa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), baada ya baadhi ya wenyeviti wa chama hicho wa mikoa na jumuiya kujitokeza kumtetea Rais Samia.
Akizungumza Desemba 28, 2021 katika mkutano mkuu wa pili wa wanakikundi cha Mikalile Ye Wanyusi uliofanyika jijini Dodoma, Ndugai alitetea uamuzi wa Bunge kuanzisha tozo za miamala ya simu, kuliko kuendelea kukopa.
“Juzi Mama amekwenda kukopa 1.3 trilioni. Hivi ipi bora? Sisi Watanzania wa miaka 60 ya Uhuru kuzidi kukopa na madeni au tubanane banane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa makubwa haya yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe ‘and how’ (na kwa vipi). Tutembeze bakuli ndio heshima? Tukishakopa tunapiga makofi, sisi wa kukopa kila siku,” alisema Ndugai.
Huku akitetea tozo alisema: “Tukasema pitisha tozo, anayetaka asiyetaka pitisha tozo, lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyia?
Hata hivyo, siku moja baada ya kutoa kauli hiyo, Rais Samia akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa SGR iliyofanyika Ikulu ya Dar es Salaam Desemba 28, 2021 alisema Serikali itaendelea kukopa ili kukamilisha ujenzi wa reli hiyo.
Juzi Ndugai hakupatikana baada ya simu yake kuita bila kupokewa kila alipopigiwa.
CCM wamshukia
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wenyeviti wa CCM wa mikoa walisisitiza kumuunga mkono Rais Samia kukopa fedha kwenye vyombo vya kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Singida juzi, Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Alhaj Juma Kilimba alitetea mikopo iliyochukuliwa katika awamu ya sita ya Rais Samia, huku akionya wanaomkatisha tamaa.
“Kuna mkopo wa Sh1.3 trilioni tulizopata kutoka Benki ya Dunia. Pesa hizi zimekuja kwa wakati na zimefanya kazi. Baada ya kukopwa zimeelekezwa kwenye kazi na zimegusa kila eneo,” alisema Kilimba.
Alitoa mfano wa mkoa huo uliopewa mgawo wa Sh28 bilioni akisema zimefanikisha ujenzi wa madarasa 700 ya shule za sekondari na pia zimetumika kuboresha miradi ya maji na afya.
“Hizi kelele za kukatisha tamaa za kusema kwa nini tunaendelea kukopa wakati tungetumia fedha za ndani? Sisi CCM tunaamini nchi yetu inajengwa kwa misingi mbalimbali, ikiwa pamoja na mikopo nafuu yenye tija,” alisema Kilimba.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba alipigilia msumari hoja ya Serikali kukopa fedha kwa masharti nafuu, alipokuwa akizungumza na viongozi wa chama hicho jijini hapa.
“Sisi Dar es Salaam tunafaidika sana na hii mikopo ya Benki ya Dunia. Mimi nampongeza Mama Samia kwa kuheshimika na vyombo hivyo, aendelee.
“Kwa mfano daraja la Jangwani litachukua karibu Sh190 bilioni, nani atatoa hela hizo? Ni mikopo nafuu ya WB,” alisema Kamba, ambaye hotuba yake ilipatikana kupitia mitandao ya jamii.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila alisema Rais Samia yupo njia sahihi katika usimamizi wa deni la Taifa na mikopo ya nje.
Aligusia ripoti ya taasisi ya Moody’s ya Agosti 30, 2021 iliyoipa Serikali ya awamu ya sita daraja la B2-Stable ambalo ni daraja la juu kulinganisha na nchi za Kenya, Ghana, Senegal, Ivory coast, Mauritius, Namibia, Afrika Kusini na Msumbiji.
“Kama Moodys ambayo ni taasisi inayongoza duniani kwa kufanya tathmini za uimara wa uchumi wa serikali na kampuni kubwa duniani inaonyesha uimara kiasi hiki wa Serikali ya awamu ya sita, hivyo ni vema wakosoaji wakawa wanarejea tafiti za kiuchumi badala ya maelezo ya jumla jumla,” alisema Kafulila.
Akizungumza juzi mkoani Iringa alipokuwa akikagua miradi ya elimu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kenan Kihongosi alisema kiwango cha fedha kilichokopwa kwenye awamu inayoongozwa na Rais Samia ni kidogo ikilinganishwa na awamu zilizopita, huku lengo likiwa kuleta maendeleo.
from Author
Post a Comment