TANESCO KUJA NA MKAKATI KUUNGANISHA UMEME NDANI YA SIKU SABA, YATAHADHARISHA WANATOA 'RUSHWA' ILI KUPATA HUDUMA. |Shamteeblog.


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

SHIRIKA la Umeme Tanzania(TANESCO) limesema moja ya mkakati wake ni kwamba kuanzia Aprili mwaka huu linataka mteja anapoomba kuunganishiwa umeme basi aunganishiwe ndani ya siku chache zaidi na isiwe zaidi ya siku hizo huku likitoa rai kwa wananchi wasikubali kutoa rushwa kwa namna yoyote ile kwa lengo la kupatiwa huduma.

Hayo yamesemwa leo Februari 20, 2022 na Msemaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Martin Mwambene  wakati akizungumzia kuhusu utekelezaji wa kampeni ya Shirika hilo ya kuunganisha umeme kwa wateja wote ambao wamelipia Sh.27,000 inayoendelea nchini kote ambayo imeanza rasmi jana.

"Leo ni muendelezo wa kampeni ambayo tumeianzisha na tuko hapa Kinondoni Kusini ambako ni miongoni mwa mikoa 129 na Wilaya 132 ambazo TANESCO tunazo nchi nzima, tunalofanya hapa ni kuhakikisha wateja waliofanya malipo ya Sh.27,000 wanaunganishiwa umeme na jana tulisema tulikuwa na wateja 90,000 na wanaendelea kupungua.

 "Lakini lengo la hii kampeni tunataka sasa mteja awe ana unganishiwa umeme ndani ya siku chache zaidi, tunataka iwe chini ya siku saba na isizidi siku hizo.TANESCO malengo yetu ni kuona mteja akiomba tu umeme basi anaunganishiwa ikiwezekana ndani ya siku moja, mbili au tatu na ikiwa imeshindikana kabisa isizidi siku saba,"amesisitiza Mwambene.

Aidha ametoa rai kwa wananchi wote hasa ambao ni wateja wa TANESCO wakiwemo walioomba kuunganishiwa umeme wasikubali kutoa fedha yoyote ile kama fedha ya ziada ili kuunganishiwa umeme au kupata huduma za Shirika."Mwananchi ukishalipa fedha ya kuunganishiwa umeme iwe Sh.27000 au fedha yoyote ile ambayo utakuwa umelipa kwa kutumia namba ya malipo, hutakiwi kutoa fedha yoyote ili kupata huduma zetu."

Ameongeza haijalishi mteja atakuwa mbali kiasi gani au alikuwa anataka nguzo ngapi, gharama ikishalipwa kwa utaratibu unaoeleweka kupitia namba ya malipo  hakuna malipo ya ziada na kusisitiza malipo yote yanayohusu TANESCO yanalipwa kwa 'Control Number' na sio vinginevyo kwani nje ya hapo itakuwa ni rushwa."Hivyo nitoe rai  usitoe rushwa na usishawishike kutoa rushwa".

Awali Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini Mhandishi Nickson Babu akizungumza kampeni ya kuunganishia umeme wateja waliolipa Sh.27000 amesema kwa leo wanatarajia kuunganishia wateja 300 katika mitaa mitatu ya Matosa, King'ong'o na Kimara.Lengo ni kutekeleza utoaji wa huduma kwa wateja wao.

"Jumla ya wateja 4300 wamefanya malipo ya Sh.27000 na wote wanahitaji kupata huduma tena kwa wakati na sisi kama ofisi tumejipanga kuwahudumia na hao 300 tutakaouwanganishia wataanza kutumia umeme leo, kampeni hii ni endelevu mpaka pale wateja wote waliolipia wawe wameunganishwa na kabla ya kumalizika Machi tutauwa tumemaliza.

Baada ya hapo tutaingia kwenye utaratibu mpya wa kuhakikisha mteja akiomba umeme anaunganishiwa ndani ya siku saba,"amesema.

Aidha amewasisitiza wananchi wasikubali kutoa rushwa kwa lengo la kushawishi kupatiwa huduma kwa haraka bali wafuate utaratibu uliopo wa kulipa gharama zinazohitahika kwa kutumia namba ya malipo.

"TANESCO gharama ambazo tunatoza ni ile ambazo tumeelekezwa na EWURA na zinalipiwa kwa Control number .Mteja akishapewa control number na akalipia hakuna kiasi chochote cha fedha ambacho mteja atatakiwa kulipa kama sehemu ya kuharakisha huduma yake, kitendo hicho kitatafsiriwa kama jinai kwa maana ya tendo la rushwa.


 "Pamoja na sisi kutoa rai hiyo tumeamua kujipanga kwa kuharakisha utoaji huduma zetu kama nilivyosema , kwa hiyo tunavyoharakisha kutoa huduma maana yake tunakwenda kupunguza vitendo vya rushwa na vitakufa moja kwa moja,"amesema Mhandisi Babu.

Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini wakiendelea na kazi ya kuunganisha umeme katika nyumba ya moja ya wateja wao ambao wamelipia Sh.27000 katika mtaa wa Masota,King'ong'o na Kimara B
Msemaji wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) Martin Mwambene akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 20,2022 kuhusu kampeni ya kuunganisha umeme inayoendelea nchini kote ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza moja ya malengo yao kuanzia Aprili mwaka huu mwananchi akiomba umeme basi ndani ya siku saba awe ameunganishiwa umeme.

Wananchi wakifuatilia maelezo ya Msemaji wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) Martin Mwambene kuhusu mipango mbalimbali inayotekelezwa na Shirika hilo katika kuwahudumia wananchi


Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO)Mkoa wa Kinondoni Kusini wakisoma majina ya wateja ambao wanatakiwa kuunganishiwa umeme baada ya kulipa Sh.27000 katika mtaa wa Matosa,King'ong'o na Kimara B .TANESCO wapo katika kampeni ya kuunganishia umeme wateja ambao inaendelea kote nchini


Zainabu Mohamed Hongo (kushoto) mkazi wa mtaa wa Masota akipata maelekezo kutoka kwa moja ya wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini namna ya kuingiza namba za mita anapohitaji kuongeza umeme baada ya leo kuunganishiwa umeme kwenye nyumba yake.

Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini wakipitia nyaraka muhimu za moja ya wateja ambao wako katika orodha ya wanaostahili kuunganishiwa umeme katika mtaa wa Mato.

Sehemu ya wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini wakiendelea kupakia vifaa vinavyotumika kuunganisha umeme kabla ya kwenda kuunganishia wateja wao leo Februari 20,2022

Zainabu Mohamed Hongo ambaye ni mkazi wa Matosa mkoani Dar es Salaam akiwasha taa kwa mara ya kwanza baada ya TANESCO Mkoa wa Kusini kumuunganishia umeme kwenye nyumba yake leo Februari 20,2022
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini Mhandisi Nickson Babu akizungumza na Wananchi wa Mtaa wa Matosa, King'ong'o na Kimara B kabla ya kuanza kuunganisha umeme kwa wateja waliolipa Sh 27000 katika Mkoa huo

 

 



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post