Wafugaji mjini Njombe wanufaika na dawa za ruzuku |Shamteeblog.


Na Amiri Kilagalila,Njombe

Vikundi 9 vya wafugaji katika Halmashauri ya Mji Njombe leo wamepokea dawa za ruzuku kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi zenye thamani ya shilingi milioni 3.5 ambazo zinatarajiwa kutumika katika majosho lengo ikiwa ni kupambana na magonjwa ya kupe kwa Mifugo na kupunguza gharama za uogeshaji wa mifugo.

Akitoa taarifa fupi ya mapokezi ya dawa hizo Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Mji Njombe Thadei Luoga amesema kuwa kumekuwa na magonjwa mbalimbali yanayoshambulia mifugo ikiwemo kupe jambo linalopelekea vifo vya mifugo na wakati huo Wafugaji kushindwa kuogesha mifugo yao kutokana na kushindwa kumudu gharama za ununuzi wa dawa hizo za mifugo.

"Zoezi lilianza mwaka 2018/2019 na tumekwisha pokea jumla ya lita 269 mpaka sasa.Dawa hizi zimekuwa na faida kubwa kwani idadi ya Ng'ombe wanaoogeshwa imeongezeka maradufu na pia imesaidia sana kupunguza magonjwa yanayoenezwa na kupe"Alisema Luoga

Aliendelea kusema"Tunaishurkuru sana Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwani tumepokea shilingi milioni 28 kwa ajili ya ujenzi wa majosho mawili yenye gharama ya shilingi milioni 14 kwa kila josho na majosho hayo yanajengwa katika Kata ya Iwungilo na Kifanya kwa upande wa Halmashauri yetu"

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Erasto Mpete amewataka viongozi wa kamati za uogeshaji na usimamizi wa Majosho 9 katika Halmashauri kuhakikisha kuwa wanaendelea kuwahamasisha wafugaji kuogesha mifugo yao lakini pia kusimamia kwa nidhamu mapato yatokanayo na shughuli za uogeshaji mifugo ili fedha zitakazopatikana ziweze kutumika kujenga na kuboresha mazingira ya majosho

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mheshimiwa Kissa Gwakisa ameishukuru Serikali kwa Msaada wa ruzuku hizo za dawa za mifugo na amesema kuwa zitakuwa na msaada mkubwa kwa wafugaji

"Tunaishukuru sana Serikali kwa kutupatia dawa hizi.Kwani zinakwenda kupunguza gharama za uogeshaji kwa wafugaji.Mfano Ng'ombe mmoja alikuwa anaoshwa kwa Shilingi 200 lakini kwa sasa atakwenda kuoshwa kwa shilingi 100 na mbuzi badala ya kuoshwa kwa shilingi 100 atakwenda kuoshwa kwa shilingi 50"Alisema Mkuu wa Wilaya

Kwa upande wao wanufaika wa ruzuku hiyo ambao ni wafugaji wameishukuru Serikali na kuahidi kuendelea kupeana elimu wao kwa wao na kuhamasishana umuhimu wa zoezi la uogeshaji mifugo.


 

By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post