Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu Bi Veronica S. Nchango akiongea na watumishi wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya KAIZEN kwa watumishi ambao wamehamia katika Wizara hiyo na watumishi ambao hawakuwahi kupata mafunzo hayo kabla. Mafunzo hayo yanatolewa kwa siku tatu kuanzia 16 Februari 16, 2022 hadi Februari 18 2022 katika Ukumbi wa Chuo Cha Elimu ya Biashara CBE Jijini Dodoma. Bi.Veronica Nchango amemwakilisha Katibu Mkuu katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
Na Doreen Aloyce, Dodoma
KATIKA Juhudi za kuendeleza uchumi wa Viwanda hapa nchini,Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara imeandaa mafunzo maalumu ya KAIZEN kwa watumishi wa Wizara hiyo lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi katika maeneo ya kazi jambo ambalo litaleta ufanisi mkubwa.
Aidha mafunzo hayo yenye kauli mbiu "KAIZEN kwa Tanzania ya viwanda shindani na maendeleo shirikishi" yamelenga pia watumishi waliohamia Wizara ya Uwekezaji na wengine ambao hawakuwahi kupata mafunzo hayo.
Akifungua mafunzo hayo ya siku tatu Mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu (DAHRM) kutoka Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara Bi Veronica Nchango amewataka washiriki kuwa Chachu kuchangia kukuza maendeleo ya viwanda na kuongeza uchumi wa Nchi.
Amesema kuwa Serikali inatagemea kupata matokeo yenye tija kwa Serikali kupitia mafunzo hayo huku akiwataka wakufunzi kuwafatilia kwa ukaribu ambao wamepata elimu kujua kama wanayofundishwa wanayafanyia kazi ili kuleta tija kwa Taifa letu na sio kuishia Kutoa mafunzo.
"Niwashukuru wale waliowezesha mafunzo haya wakiwemo Jaica ambao wamefadhili mradi huu ambao unalenga kuongeza tija na ubora Katika Sekta zote hivyo niwaombe muwe wasikivu kwa siku hizi tatu mkitoka hapa muwe mmeiva "
"Tunapaswa kuwa kioo kupitia KAIZEN kuwa na mtazamo chanya ili Jamii ione matokeo ya kuendeleza maendeleo ya viwanda hapa nchini" amesema Mchango.
Janne Lyatuu Mkuu wa Kitengo cha KAIZEN Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Janne Lyatuu ametumia fursa hiyo kuiomba Wizara kuwa mafunzo hayo yawe endelevu Nchi nzima.
"Tunaomba mafunzo yawe endelevu kwa watumishi wa Wizara na Nchi nzima na niwaombe wale wenye muamko wa kusoma masomo haya waelekee kwenye kuleta Mabadiliko kwa wizara.
Kwa upande wake Meneja wa Dodoma Semphao Manongi amesema kuwa endapo wataitumia dhana ya Kaizeni itasaidia kubadilisha uchumi wa nchi .
"Endapo tukiifanyia kazi hii dhana na kuitekeleza kama inavyotakiwa tunaweza kufufua viwanda vyetu na kuliokoa Taifa letu " amesema Manongi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo hayo wamesema kuwa mafunzo hayo yataenda kuwajenga na kuwaongezea uelewa ambao utawasaidia kuinua uchumi wa Nchi kupitia viwanda.
Mkuu wa Kitengo cha KAIZEN ( TKU) kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bi. Janne Lyatuu akimkaribisha mgeni rasmi aweze kuongea na watumishi wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya KAIZEN kwa watumishi ambao wamehamia katika Wizara hiyo na watumishi ambao hawakuwahi kupata mafunzo hayo kabla. Mafunzo hayo yanafanyika katika Ukumbi wa Chuo Cha Elimu ya Biashara CBE Jijini Dodoma.
Meneja wa SIDO Mkoa wa Dodoma Ndugu Semphao Manongi akitoa mafunzo kwa watumishi wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya KAIZEN kwa watumishi ambao wamehamia katika Wizara hiyo na watumishi ambao hawakuwahi kupata mafunzo hayo kabla .Mafunzo hayo yanafanyika katika Ukumbi wa Chuo Cha Elimu ya Biashara CBE Jijini Dodoma. Ndg.Semphao Manongi ni miongoni mwa wakufunzi wanaotoa mafunzo ya KAIZEN kutoka katika taasisi zilizo chini ya Wizara Uwekezaji, Viwanda na Biashara
Watumishi wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara wakifuatilia Mafunzo ya KAIZEN kwa umakini zaidi katika ukumbi wa Chuo Cha Elimu ya Biashara jijini Dodoma
Picha ya pamoja ya watumishi wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ambao hawakuwahi kupata fursa ya kuhudhuria mafunzo ya KAIZEN kabla, wakiwa na mgeni rasmi aliyefungua mafunzo hayo Bi.Veronica S. Nchango baada ya hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoendelea kutolewa katika Ukumbi wa Chuo Cha Elimu ya Biashara CBE Jijini Dodoma kwa siku tatu.
By Mpekuzi
Post a Comment