Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geoffrey Mizengo Pinda akiongea kwenye Baraza la wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili mkuu wa Serikali leo Dodoma katika ukumbi wa Takwimu ambapo ametumia nafasi hiyo kuwataka kufanya kazi kwa ushirikiano na kuepuka majungu.
Baadhi ya wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili mkuu wa Serikali wakisikiliza Kwa makini Naibu Waziri wa katiba na sheria Geoffrey Mizengo Pinda kwenye kikao cha pili cha baraza la wafanyakazi Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwa ni utekelezaji wa takwa la kisheria Katika kuwashirikisha wafanyakazi uongozi wa pamoja.
Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog-DODOMA
KUTOKANA na kuimarisha Mifumo ya usimamizi wa mashauri na uthibiti wa Ubora,Serikali imeokoa kiasi cha Shilingi Bilioni 236.6 kwa kushinda mashauri 444 ya madai yaliyomalizika hadi Januari 2022 na mashauri ya Usuluhishi 6.
Hatua hii imetokana na Serikali kuiongezea Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali bajeti yake kutoka Shilingi Bilioni 11.48 kwa Mwaka wa Fedha 2020/21 hadi Bilioni 12.13 kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 5.4.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi la Ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata katika kikao cha pili cha baraza la wafanyakazi wa Ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwa ni utekelezaji wa takwa la kisheria la kuwashirikisha Wafanyakazi katika Uongozi wa Pamoja Mahala pa Kazi.
Malata amesema,kuongezeka kwa bajeti ya OWMS kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 katika kipindi cha uongozi wa Awamu ya Sita, kumepelekea Ofisi kufanya shughuli zake kwa ufanisi na kupata mafanikio ya kuiwakilisha vyema Serikali Mahakamani na Mabaraza ya Usuluhishi.
"Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeendesha mashauri ya Madai 1,102 na ya Usuluhishi 117 hivyo kufanya jumla ya mashauri yaliyoendeshwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kuwa 1,219",amesema
Aidha, Mashauri ya Madai yaliyomalizika hadi Januari 2022 na Serikali kushinda ni 444 na Mashauri ya Usuluhishi 6 na hivyo kuokoa kiasi cha Shilingi Bilioni 236.6. Kuimarisha Mifumo ya Usimamizi wa Mashauri na Uthibiti wa Ubora,"amefafanua.
Licha ya hayo ameeleza kuwa katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha, Ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) imeimarisha mfumo wa kukusanya takwimu za kesi, kufanya ufuatiliaji wa mienendo ya kesi na kupitia sheria zinazohusu kesi za Madai na Usuluhishi.
"OWMS hutumia njia ya usuluhishi, majadiliano, na kufungua kesi Mahakamani na kusaidia mashauri kuisha kwa wakati na kunarejesha amani kwa pande husika na kuzifanya kuendelea na shughuli za maendeleo,"amesema.
Pia amesema Ofisi hiyo imeweza kuandaa Miongozo ya kusimamia na kuthibiti viwango vya ubora vya Mawakili katika uendeshaji wa kesi ikiwa ni pamoja na kuandaa Mkataba wa huduma kwa mteja ambao ni Serikali na Taasisi nzake.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2021/22 na mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, Mwenyekiti huyo wa baraza la wafanyakazi ameeleza kuwa OWMS imewawezesha watumishi kupata mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu yakiwemo Mafunzo ya Shahada za Awali kwa watumishi watatu (3) na Shahada za Uzamili kwa watumishi tisa (9).
Mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 92 wa kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mawakili, Makatibu sheria, Madereva, makatibu muhtasi na , Wahudumu yalitolewa;Mafunzo kwa Viongozi (Menejimenti) ili kuweza kuwakumbusha mambo ambayo wanapaswa kuyafanya na kuyaishi kama viongozi; Mafunzo kwa Mawakili kuhusu masuala ya kesi za Usuluhishi;Ajira na Ujazaji wa Nafasi za Watumishi.
"Vilevile Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeweza kujaza nafasi mbalimbali za za ajira,
Ofisi yetu pia ilipata vibali vya kuajiri watumishi 23 wapya, Watumishi watatu (3) kwa nafasi ya ajira mbadala na mtumishi mmoja (1) wa kuhamia. Tayari Ofisi imeweza kujaza nafasi hizo na kufikia watumishi 159 na upandishwaji wa madaraja,"amesema Mwenyekiti huyo.
Pamoja na mafanikio hayo, Mwenyekiti huyo ameweka wazi kuwa OWMS inakabiliwa na changamoto mbalimbali Ikiwemo upungufu wa Watumishi 153 kwa mujibu wa Ikama iliyopo kwa sasa ambayo ina jumla ya Watumishi 312; Maslahi kwa watumishi wa Ofisi ya Wakili wa Serikali hayaendani na uzito wa majukumu ya Ofisi; Ufinyu wa bajeti (Budget ceiling).
Kutokana na hayo amesema wanaendelea kufanya majadiliano na Serikali ili kuomba kuongezewa wigo wa bajeti (ceiling) kuweza kutoa huduma stahiki na kuboresha mazingira ya kazi.Kuomba Taasisi mbalimbali kuchangia katika kutatua baadhi ya changamoto.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geoffrey Mizengo Pinda amesema kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kuondoa uzembe na ubadhilifu mahala pa kazi na kulitaka baraza hilo kutambua wajibu wao kama chombo cha ushauri na kutambua haki na wajibu kwa wanaowahudumia.
Pinda amesema,ushiriki wa watumishi kwenye maamuzi katika dhana nzima ya Utawala bora,ni muhimu hali itakayorahisisha katika maamuzi kupitia vikao mbalimbali vya Idara, Baraza la wafanyakazi pamoja na mkutano wa wafanyakazi wote .
"Nyie ni taasisi inayosimamia haki za watu,hakikisheni haki inatoka kwa utaratibu ulio sahihi,epukeni vionjo vya rushwa vitawaangusha,fuateni utaratibu unaoelekezwa na katiba yetu",amesema
Vilevile Pinda amesema serikali inatambua uchache wa watumishi katika Ofisi hiyo na kusisitiza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya wakili mkuu wa Serikali inaendelea kufanyia kàzi suala hilo ili kuongeza ufanisi katika kazi.
Pamoja na hlo alitumia nafasi hiyo kuwataka wafanyakazi hao kujiepusha na migogoro isiyo na tija huku akiwataka kufanya kazi kwa upendo,uwazi na ushirikiano.
"Natambua kuna wakati huwa hakuna maelewano mazuri kati ya watumishi na Menejimenti lazima tupendane ili kazi ziende,bila upendo hamuwezi kupiga hatua,tambueni ni Kwa kushirikiana ndipo haki kwa wengine hutendeka,"amesisitiza.
By Mpekuzi
Post a Comment