WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) amefanya ziara ya kutembelea Shirika la Mzinga kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika.
Akiwa katika ziara yake katika Shirika hilo alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali na kujionea shughuli kadhaa zinazoendelea, kupatiwa maelezo ya kina ikiwa ni pamoja na hatua zilizofikiwa katika kuzalisha mazo ya msingi, mafanikio, yaliyopatikana, changamoto na mipango waliyojiwekea.
Hii ni ziara ya kwanza ya Mheshimiwa Waziri kutembelea Shirika hilo tangu ateuliwe na kuapishwa rasmi na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kuwa Waziri wa Ulinzi na JKT tarehe 13 Septemba, 2021.
Akiongea na Watumishi wa Shirika alibainisha kuwa ”nimekuwa nikijitahidi kupanga muda wa kutembelea Shirika la Mzinga kwa muda kidogo, nashukuru kuwa leo nimepata fursa ambapo nimeweza kupata wasaa wa kuja hapa kuzungumza na ninyi lakini pia kutembelea Shirika, kujionea mwenyewe , kupata uelewa mpana wa shughuli zinazofanywa hapa mzinga na kuzitambua changamoto”.
Dkt. Stergomena alikumbusha umuhimu wa Shirika hili kwa kusema kuwa” kama tunavyofahamu, Shirika la Mzinga ni muhimu sana, siyo tu kwa JWTZ na kwa Wizara lakini pia kwa mustakabali wa maslahi mapana ya Taifa letu kiulinzi, kiusalama na hata kiuchumi. Unyeti wa majukumu ya Shirika hili umeainishwa bayana katika Aya 4 (1), (2) ya Sheria ya Mwaka 1969 ya kuanzishwa kwa Shirika, lakini pia unyeti wa Shirika umeainishwa katika Notisi ya Serikali (Government Notice) Namba 196 kama ilivyochapishwa katika Gazeti la Serikali la mwaka 1973”.
Akitoa taarifa ya kwa Mheshimiwa Waziri, Meneja Mkuu, Brigedia Seif Hamis alisema “Shirika Mama la Mzinga lilianzishwa mwaka 1971 ukiwa ni mradi kwa ajili ya kuzalisha mazao kwa matumizi ya JWTZ. Tarehe 13 Septemba, 1974 mradi huu ulibadilishwa na kuwa Shirika la Umma (Public Corporation) chini ya Wizara ya Ulinzi na JKT kwa Tamko la Serikali Na. 219”.
Brigedia Jenerali Hamis aliongeza kwa kusema kuwa “Shirika la Mzinga kisheria linao wajibu wa kuzalisha mazao ya msingi na mitambo, kufanya tafiti mbalimbali, kukarabati vifaa na mitambo mbalimbali na kutekeleza majukumu yote muhimu kwa maendeleo ya Shirika na Taifa kwa ujumla.”.
“Shirika la Mzinga linajishughulisha na shughuli kuu mbili, kwanza, ni shughuli za kuzalisha mazao ya msingi ya mwaka 1971 na yale mazao yaliyoongezwa mwaka 2012. Pili, Shirika linajishughulisha pia, na shughuli mbadala ili kujiongezea kipato kwa lengo la kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikalini”, alimaliza.
Shirika limeendelea kufanya tafiti mbalimbali ambazo zimelenga kuboresha mazao linayoyazalisha. Mbali na kufanya tafiti Shirika pia, limeendelea kufanya maboresho kwa kununua mitambo mipya itakayotumika katika kuzalisha mazao ya msingi na mitambo, mafunzo kwa wataalamu wa Shirika, kuendeleza ushirikiano baina ya mashirika yaliyo chini ya Wizara ya Ulinzi na JKT katika kubadilishana uzoefu pamoja na maboresho ya miundombinu ya shirika.
Sambamba na maboresho hayo, juhudi kubwa zimeendelea kufanyika katika kutatua changamoto za uchakavu wa mitambo na majengo ya karakana, upungufu wa rasilimali watu, ubovu wa barabara, uvamizi wa mipaka ya eneo la Shirika pamoja na usalama wa kiwanda ambapo uzalishaji wa zao la msingi umeanza kuimarika zaidi hadi kufikia asilimia 97.5. Kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa Shirika hili.
By Mpekuzi
Post a Comment