Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa - TMA Mkoa Kagera Stiven Malundo
Afisa Mazingira Manispaa ya Bukoba Tambuko Joseph
Mwenyekiti wa mtaa wa Omukigusha Bw. Abdulhakim Idrisa
**
Na Mbuke Shilagi Kagera.
Mamlaka ya Hali ya Hewa -TMA- Mkoa wa Kagera imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika msimu huu wa mvua hasa kwa wanaoishi katika maeneo ya bondeni, ili kuepuka kupata madhara yatokanayo na mvua, ikiwemo kukumbwa na mafuriko.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne Aprili 5,2022 na Meneja wa TMA Mkoa wa Kagera Stiven Malundo wakati akizungumza na Malunde 1 Blog ofisini kwake, na kwamba mwezi huu wa Aprili mvua itakuwa nyingi zaidi kuliko ya mwezi Machi.
Bw. Malundo amesema kuwa kwa mwezi huu mvua zitanyesha kiwango cha wastani mpaka juu ya wastani, ambayo ni milimita 335 juu zaidi ya mwezi Machi na kuwataka wanannchi wote kutumia mvua hizo katika kilimo, kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu.
Kwa upande wake Afisa Mazingira wa Manispaa ya Bukoba Bw. Tambuko Joseph amesema kuwa tayari wamesafisha mto Kanoni ambao hupokea maji kutoka maeneo mbalimbali na kusababisha mafuriko katika mitaa ya Omukigusha uliyopo Kata ya Bilele na Buyekera uliopo kata Bakoba.
Bw. Joseph amesema kuwa wametoa elimu kwa wananchi wote wanaoishi karibu na mito kutotupa taka ndani ya mitaro na tutofanya shughuli zote za ujenzi ndani ya mita 60 za ukingo wa mito, na badala yake waongeze juhudi za kuulinda na kuepusha uharibifu.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Omukigusha Kata ya Bilele Bw. Abdulhakim Idrisa amesema kuwa mtaa wake tayari wamefanya usafi katika mitaro inayopeleka maji mto Kanoni na kwamba mto huo ambao umekuwa ukisababisha mafuriko katika mtaa huo kingo zake zimewekewa vifusi kuzuia maji yasivuke, kuongezewa upana pia kupanda matete katika kingo za mto huo, ili kuzuia mmomonyoko wa udongo ambao husababisha maji kuingia katika makazi ya watu.
Bw. Idrisa ameishukuru serikali kwa kudhibiti tatizo la mafuriko kwa miaka miwili katika eneo la mto Kanoni, ambalo lilikuwa chanzo kikubwa cha mafuriko katika mtaa wake, kwa kufanyiwa usafi na kupanuliwa, ili maji yanapojaa yasiingie kwenye nyumba za watu.
"Ninachowaomba wananchi wa mtaa wangu, waendelee kusafisa mitaro inayowazunguka ili iwe safi muda wote na kuweza kuruhusu maji ya mvua kupita kwa urahisi" amesema.
By Mpekuzi
Post a Comment