Na Joseph Lyimo
IDADI kubwa ya wafugaji wa kuhamahama wanaoishi katika Wilaya ya Simanjiro na Kiteto Mkoani Manyara, wameendelea kupokea na kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19 kutokana na mpango wa Wizara ya Afya kuendeleza shughuli ya wananchi mbalimbali nchini kupata chanjo hiyo.
Baadhi ya maisha ya wafugaji wa Wilaya ya Simanjiro na Kiteto, yamekuwa yakuhama hama wao na mifugo yao ili kufuata malisho na maji, pindi maeneo wanayoishi yanakumbwa na ukame.
Wengi wao huwa wanaondoka na familia zao na kuondoka maeneo waliyokuwa wanaishi na wengine huondoka sehemu wanazoishi na kuziacha familia zao ila hurejea walipokuwa wanaishi mara baada ya kipindi cha ukame kumalizika.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya wataalam wa afya waliokuwa wanafanya shughuli ya kutoa chanjo ya UVIKO-19 ilikuwa vigumu kuwafuata wafugaji hao katika maeneo yao kutokana na wao kuwaondoka kufuata maji na malisho ya mifugo yao.
Badhi ya wafugaji hao walipata chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinopharm, ambayo walipaswa kuchanjwa mara mbili ili kumaliza dozi ila kutokana na kuhama hama walishindwa kumaliza na kupata chanjo ya pili.
Wafugaji hao walishindwa kumaliza dozi ya chanjo hiyo kutokana na kuhama hama na mifugo yao kutoka eneo moja kwenda eneo jingine kutokana na kufuata malisho hayo hivyo kujiweka katika hatari ya kupata UVIKO-19 na kudhurika zaidi kwa sababu ya kutomaliza dozi ya chanjo hiyo.
Mfugaji wa kata ya Naberera Elias Lembris anasema mwishoni mwa mwaka 2021 alipata chanjo kwenye kituo cha afya cha Naberera ila alipaswa kurudia chanjo hiyo baada ya miezi sita ila alishindwa kurudia kutokana na kuhama.
Anasema baada ya kuchanjwa haikupita muda mrefu akahama kutoka Naberera na mifugo yake kutafuta malisho eneo lingine hivyo alishindwa kupata dozi ya pili mara baada ya kuchanjwa kwa mara moja.
“Kutokana na hali ya ukame uliotokea kwenye eneo letu ilibidi nihame Naberera na kufuata malisho kwenye kata ya Kitwai mpakani na wilaya ya Kilindi mkoani Tanga ambapo hakukuwa na huduma ya chanjo ya UVIKO-19,” anaeleza Lembris.
Hata hivyo, anasema hivi sasa amepata chanjo ya UVIKO-19 baada ya kurudi kwenye kata yake ya Naberera na kukuta chanjo inaendelea kutolewa na amekamilisha dozi yake, kupitia chanjo ya Johnson jonhson.
Mfugaji mwingine Emmanuel Nyangusi anaeleza kuwa alishindwa kukamilisha dozi yake kutokana na kuhama baada ya kutokea ukame uliosababisha mifugo mingi kufa kwa kukosa malisho na maji.
“Mifugo mingi ilikufa kutokana na ukame, hakukuwa na majani wala maji ikatubidi kuhama kufuata malisho kwenye maeneo mengine hivyo kushindwa kukamilisha dozi ya chanjo ya UVIKO-19,” anasema Nyangusi.
Mfugaji wa kata ya Partimbo Wilayani Kiteto, Yohana Paresoi anaiomba Serikali kutumia kwa wafugaji dozi ambayo inatolewa mara moja kuliko kutumia dozi ambayo inawapasa kuchanjwa mara mbili ili waepuke kutokukamilisha dozi pindi wakihama hama.
Paresoi anaeleza kuwa yeye aliondoka kwenye kata yake na kuhamia kata ya Makame ili kufuata malisho ya mifugo yake kutokana na eneo hilo kukumbwa na ukame mwaka jana hivyo akashindwa kukamilisha dozi ya chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinopharm.
“Tunaiomba Serikali wanapowatuma wataalam wa afya kuja kutupatia chanjo ya UVIKO-19 wawe wanakuja na chanjo ambayo tunaambiwa tunachanjwa mara moja ili ukame ukitokea kama mwaka tukihama tuwe tumemaliza dozi,” anasema Paresoi.
Hata hivyo, mmoja kati ya wataalam wa idara ya afya Wilayani Kiteto wanaotoa huduma ya chanjo kwa kwenye maeneo ya wafugaji Halima Ally anasema kuwa hivi sasa wamekuwa wakitumia aina ya dozi ya Johnson Johnson ambayo inachomwa mara moja badala ya ile Sinopharm, inayochomwa mara mbili.
"Tulionelea ni vyema tutumie dozi ya johnson and johnson ambayo inatumika mara moja tu na ikapendwa na watu wengi na hili limesaidia sana kwa wafugaji kwani hata wakihama na mifugo yao wanakuwa wameshama dozi ya UVIKO-19,” anaeleza.
Anasema kutokana na hali hiyo wana matumaini kuwa jamii ya wafugaji wataweza kutumia fursa hiyo kwa kupata chanjo hiyo ya UVIKO-19 tofauti na kipindi cha mwishoni mwa mwaka jana walipohama hivyo kutokumaliza dozi za chanjo zao.
“Ukitaka kuwapata wafugaji ni lazima uwafuate sehemu walipo na kwa wakati kwani huwezi kuwatafuta malishoni lakini unaweza kuwapata kwenye vituo vya maji na wakati mwingine,inabidi tunawapa huduma muhimu wakiwa hapo kwenye maji hususan kwenye maswala ya chanjo kwa mifugo na binadamu,” anaeleza.
Anasema hatua hiyo, ndiyo njia ya kipekee ya kuhakikisha jamii ya wafugaji inashiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani wengi wa wafugaji huandamana na mifugo yao malishoni na endapo hawatafuatiliwa.
Kwa upande mwingine anasema kuwa jamii ya wafugaji wakishapatiwa elimu juu ya suala Fulani na wakalielewa huwa wanashiriki kufanya na kutekeleza kwani wengi wao hawana ubishi.
Mtaalamu wa ufuatiliaji na mdhibiti wa magonjwa wa Wizara ya Afya, Dkt Baraka Nzobo anaeleza kuwa endapo mtu atapata chanjo mara moja na hakumaliza dozi ya pili atakuwa hajapata chanjo kamili.
Dkt Nzobo anasema kwamba inatakiwa mtu akipata chanjo ya UVIKO-19 anapaswa kushiriki chanjo ya pili ili kumaliza dozi kamili ya kupambana na janga hilo la UVIKO-19 kuliko kuchanja mara moja.
Mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Dkt Aristidy Raphael anasema kuwa japokuwa maisha ya baadhi ya jamii ya wafugaji ni ya kuhamahama ila mwitikio wa wananchi wa eneo hilo hivi sasa katika kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 ni mkubwa.
Dkt Raphael anasema mara baada ya mkuu wa mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere kuzungumza na madiwani wa halmashauri nao wakawapa elimu jamii, mwitikio wa kupata chanjo umekuwa mkubwa.
“Japokuwa baadhi ya jamii ya wafugaji ni watu wa kuhamahama kutokana na kufuata malisho kwenye maeneo mbalimbali wamehakikisha kuwa wanawapatia chanjo ya UVIKO-19 ili kupambana na janga hilo kwani wamepatiwa elimu bila chanjo watapata maambukizi na kuathirika zaidi,” anaeleza.
Anasema kwamba pia madiwani wa halmashauri hiyo walikuwa wakwanza kushiriki kwenye chanja hivyo kuwa mfano kwani kiongozi wa jamii ya kifugaji hawezi kusisitiza chanjo ili hali wao wenyewe hajapata chanjo hiyo.
Dkt Raphael anasema mara baada ya mkuu wa mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere kuzungumza na madiwani wa halmashauri nao wakawapa elimu jamii hiyo, mwitikio wa wafugaji kupata chanjo umekuwa mkubwa hivyo wanashiriki chanjo kabla ya kuhama kutoka eneo moja kwenda nyingine.
Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara, Dkt Damas Kayera anaeleza kuwa wanatarajia kumaliza tatizo hilo kwa kutoa dozi ya chanjo ya johnson Johnson ambayo wanapata mara moja.
Dkt Kayera anasema kwamba hivi sasa jamii ya wafugaji wa mkoa wa Manyara wamehamasika zaidi na kushiri kwenye kupata chanjo ya UVIKO-19 tofauti na mwaka jana.
“Awali jamii ya wafugaji walikuwa wanahama kutokana na ukame hivyo kufuata malisho kwenye maeneo mengine hivyo kusababisha wengine kutomaliza dozi ya chanjo ya UVIKO-19,” anaeleza Dkt Kayera.
By Mpekuzi
Post a Comment