*Kila hatua ya maisha yake inaacha somo kwa Wanasiasa, Watanzania
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
EWE Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na ardhi, nakuomba unipe utulivu, hekima na busara, naomba unipe utulivu kwa sababu nataka kumwelezea japo kwa kidogo mwanasiasa nguli Afrika, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Nataka kumwelezea Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kanali Mstaafu Abdulrahman Omari Kinana. Ukitaka kumwelezea Kinana lazima uwe na utulivu wa akili, huo ndio ukweli kabisa.
Watanzania wanamfahamu vema Kinana na kila mmoja anamfahamu kwa kiwango chake. Kinana amelitumikia taifa letu kwa utumishi uliotukuka na ameshika nafasi mbalimbali ndani ya Chama na serikali.
Kabla ya kumwelezea zaidi Kinana, naomba msomaji wa makala haya umfahamu japo kwa ufupi. Kinana alizaliwa mwaka 1951 mkoani Arusha, Kaskazni mwa nchi yetu nzuri ya Tanzania.
Alihitimu shahada yake katika Chuo Kikuu cha Havard cha Marekani akibobea katika masuala ya mikakati. Havard ni moja ya vyuo vikuu vyenye heshima kubwa duniani.
Unaweza kujiuliza tu wanasiasa wangapi wa Tanzania na Afrika Mashariki waliosoma kwenye chuo hicho? Utakapotaja orodha ya waliopitia hapo utakutana na jina la Kinana.
Katika utumishi kama ambavyo nimetangulia kueleza Kinana ni mmoja wa wanasiasa wachache ambao wamebahatika kushika nafasi nyeti katika serikali kwa awamu tofauti.
Kabla sijataja maeneo ambayo ameyatumikia nikukumbushe mapema, Kinana ndiye Spika wa kwanza wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) nafasi aliyoishikilia kuanzia mwaka 2001 hadi 2006.
Amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha nafasi ambayo aliitendea haki, wananchi walimpenda naye akawapenda.
Kinana ambaye ni gwiji la siasa, mwenye uwezo wa kupanga mikakati, amewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimatafa, kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taita.
Pamoja na kuwa kwenye nafasi hizo, Kinana aliwahi kufanya kazi na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa miaka 20 kabla ya kustaafu mwaka 1972 akiwa na cheo cha Kanali.
Kila ambako Kinana amepita ameacha alama ambayo itachukua miaka mingi kufutika, hiyo inatokana na hekima, busara na maarifa ambayo Mungu amemjaalia, ni kiongozi mahiri, kiongozi mfano wa kuigwa.
Amejeaaliwa kila kitu, lakini siku zote amebaki kuwa Kinana yule yule ambaye anafikika na kila mtu. Hana makuu mzee wa watu na siku zote anaamini katika ushirikiano wenye hoja na sio vioja.
Binafsi nashukuru Mungu angalau mara chache nimekuwa naye kwa karibu. Ninaposema mara chache unielewe yaani mara chache haswaa, ananitambua kwa jina na kwangu hiyo inanitosha sana. Acha nivimbe, acha niringe kwani kuna ubaya gani.
Kwa hiyo ninaposema Kinana ni nguli wa siasa nadhani umeelewa japo kidogo na nafahamu wapo ambao wanamfahamu zaidi, lakini kwenye kumfahamu huko na hiki ninachoeleza kitakuwa miongoni mwao.
Ni huyu huyu Kinana kwa nyakati tofauti amekuwa Kampeni Meneja wa wagombea urais wa CCM, amewahi kuwa Kampeni Meneja wa Mgombea urais wa Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne. Akiwa katika nafasi hiyo Kinana ametimiza wajibu wake kwa mafanikio makubwa. Ni mtalaamu wa kupanga mipango na ikafanikiwa.
Mbali na kuwa Kampeni Meneja, Kinana kutokana na uwezo wake mkubwa kisiasa, amekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kwa miaka 30 kabla ya kung’atuka baada ya utumishi wake uliotukuka wa muda mrefu.
Hata hivyo, CCM baada ya kutafakari kwa kina ikaona haitakuwa vema kumwacha Kinana akapumzike ingali Chama kilikuwa kinamhitaji, ndipo aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa wakati huo na Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete kuamua kumteua kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho.
Ngoja nieleze kitu kidogo kwenye mchakato wake wa kuwa Katibu Mkuu nami nakumbuka niliufatilia kwa karibu.Zipo sababu zilizonifanya nifuatilie, hakika alistahili kushika nafasi hiyo ya Ukatibu Mkuu
Hapo kwenye Ukatibu Mkuu wa CCM nami ndipo sasa naweza kuanza kumweleza kwa kujiamini, tena kwa kujiamini haswaa. Unajua kwa nini? Nimebahatika kuwa naye kwa karibu. Kila alipokwenda nami nilikuwepo.
Tunakumbuka wakati Kinana anakuwa Katibu Mkuu wa CCM alikikuta Chama hicho kikiwa katika hali ngumu, hakikuwa na mvuto, kilipoteza mwelekeo. Hakikuwa kikizungumzwa vizuri na mamilioni ya wananchi. Kuvaa sare za CCM ilikuwa inahitaji moyo wa Simba, ilihitaji ujasiri wa Chui.Nakumbuka ambavyo wana CCM walichaniwa sare zao na kuzomewa hadharani, CCM ilikuwa kwenye wakati mgumu.
Baada ya Kinana kuona hali hiyo alikaa chini na kusuka mipango, aliweka mikakati, akaweka ramani yake. Hapo akaja na mbinu kadhaa na moja ya mbinu hizo akatangaza kufanya ziara ya kukihuisha Chama. Akazunguka kwenye majimbo yote ya uchaguzi, akazunguka wilaya zote, mikoa yote.
Alizunguka katika Kata,Vitongoji na Vijiji mbalimbali. Kwa kifupi Kinana alifika kila mahali na huenda akawa Katibu mkuu pekee wa Chama hicho kwa sasa aliyeweka historia ya kuzunguka kila mahali kwa ajili ya Chama chake. Ziara zake zikairejeshea uhai CCM, Chama kikapendwa, kikabalika.Alitumia zaidi ya miaka miwili kuzunguka nchi.
Akiwa kwenye ziara zake Kinana alifanya mambo makubwa, alikagua miradi ya maendeleo na ili kufika huko alitumia kila aina ya usafiri, kila alikoona ni muhimu kufika alikwenda.Hakuogopa mvua, hakuogopa jua, hakuogopa mwanga wala hakugopa giza.Mzee wa watu aliamua kujitoa kwa ajili ya Chama chake.
Watanzania wanayo kukumbuku nzuri ya ziara za Kinana akiwa Katibu Mkuu wa CCM. Alitatua changamoto za wananchi, hata waliokuwa na shida binafsi alizibeba na kuzitatua kwa niaba ya Chama chake.
Kinana alikutana na makundi ya watu mbalimbali, hakujali dini, rangi wala kabila wote kwake aliaamini ni wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akakutana nao , akazungumza nao, akashikana nao mikono , akala nao na kubwa zaidi alicheka nao, pale kwenye huzuni alihuzunika nao.
Wakati Nape Nnauye akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi kwa ushirikiano wa karibu na Kinana walitengeneza muunganiko mzuri wa kukitumikia Chama. Walipitia raha na karaha na leo CCM iko salama.Kuwabeza kwa kazi yao ni kuwakoesea heshima.
Hata hivyo Kinana baada ya kuondoka katika nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM alikwenda kupumzika. Akawa kimya na bahati mbaya akapita kwenye misukosuko kidogo, lakini tunafahamu jiwe la baharini huwa halitikiswi na mawimbi.
Ni Kinana ambaye aliamua kujitokeza hadharani kuomba radhi kwa kiongozi wake.Alionesha uungwana wa hali ya juu, alionesha namna anavyoweza kujishusha bila kujali wengine watamuonaje.Hakutaka kuangalia amekosea au hajakosea, aliamini kwenye kutafuta suluhu, leo amebaki na heshima yake.
Kwangu amebakia kuwa shujaa atakayedumu kwenye akili zangu kwa miaka mingi ijayo.Ni ngumu kumyumbisha na sifa ya mwanajeshi mwenye cheo kama alichokuwa nacho yeye huwa hayumbi.Hajawahi kuyumba.
Basi bwana baada ya kuwa nje ya siasa kwa muda, Kinana amerejea tena kukitumikia Chama Cha Mapinduzi na sasa ndiye Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Tanzania Bara. Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameona Kinana ni mtu sahihi kumsaidia kazi za Chama.Nafasi hiyo iliachwa wazi baada ya Mzee Philip Mangulla kuomba kung'atuka, barua yake ilijieleza vizuri.
Hivyo jina la Kinana lilifikishwa kwa wana CCM waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Chama na baada ya Rais Samia kulitaja mbele ya wajumbe ukumbi mzima uliripuka kwa shangwe. Kinana anakubalika kwa wana CCM na hilo linatokana na kutambua uwezo na utendaji wake.Kinana anakubalika kwa Watanzania.
Na sasa Kinana kama kawaida yake ameamua kufanya tena ziara ya kupita kwenye mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kukutana na wana CCM pamoja na wananchi. Kwa muda mfupi ziara zake zake zimekuwa na msaada mkubwa, anatatua changamoto nyingi ambazo zinawakabili wananchi.
Tangu amekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM tayari ameshakwenda kwenye mikoa zaidi ya 10 na kote huko amefanya kazi kubwa ya kukijenga Chama chake, kusikiliza kero za wananchi na wakati huo huo akikagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.Kuna changamoto ambazo zimedumu kwa muda mrefu lakini kupitia ziara zake zimepata ufumbuzi.Anapoona changamoto ni kubwa kuliko nafasi yake anazipeleka kwenye Mamlaka za juu zaidi.
Anapokuwa kwenye mikutano ya ndani ya CCM Kinana anafanya kazi kubwa sana ya kuweka mambo sawa, amekuwa na uwezo mkubwa wa kujibu maswali ya wananchi, hata pale ambapo swali linakuwa gumu kwake anatoa majibu yanayotoa matumaini kwa kila aliyepo ukumbini.Kuna maeneo anakwenda anakuta Wana CCM wenyewe kwa wenyewe Wana migongano, anawasikiliza anapokuja kufanya majumuisho watu wanacheka,mambo yanakwenda.Hadi raha yaani.
Kinana Mungu amempa karama ya pekee, anashughulikia mambo kwa utulivu kabisa. Nikiri tunao wana siasa wengi katika nchi hii, lakini kuwa na mwanasiasa wa aina ya Kinana ni wachache sana, binafsi naona hakuna anayeweza kufanana naye ingawa wapo wanaoweza kufuata nyayo zake kama wako tayari kujifunza.
Nakumbuka Kinana akiwa katika ziara zake za kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Katavi,Rukwa, Songwe na Mbeya , Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho, Shaka Hamdu Shaka aliamua kutoa ya moyoni kuhusu Kinana.
Shaka anamuona Kinana kama Chuo Kikuu cha Siasa kinachotembea na akaomba wanasiasa wengine hususan vijana kujifunza kutoka kwa Kinana.Na bahati nzuri Shaka amekuwa Mwanafunzi wa Kinana anayejifunza kwa Kasi, hakika CCM inatengeneza hazina nyingine kupitia Kinana .Hongera Shaka kwa kazi kubwa na nzuri unayofanya, fuata nyayo ndugu yangu.
Mimi sio mwana siasa, lakini kupitia Kinana nimejifunza mambo mengi sana, amenifundisha jinsi gani kiongozi wa umma anavyopaswa kuwa. Hakika nimejifunza na nitaendelea kujifunza kutoka kwa Mzee Kinana. Bahati niliyonayo tangu amekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM nimepata nafasi ya kuzunguka naye kwenye mikoa aliyokwenda.Nilijifunza kwa Kinana akiwa Katibu Mkuu na sasa najifunza tena Kinana akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM.
Nitoe rai kwa kila Mtanzania kwa nafasi yake kujitazama na kisha kuangalia anaweza kujifunza kitu gani kupitia Kinana.Wanaotaka kujifunza kuhusu siasa hapo ndio mahala pake, wanaotoka kujifunza kuhusu utumishi wa umma Kinana aliifanya kazi hiyo kwa uaminifu na uzalendo mkubwa.
Lakini hata wale wanaotaka kujifunza kuhusu namna ya kufanikiwa kimaisha bado wanaweza kujifunza kwa Kinana.Mzee Kinana amefanikiwa katika kila eneo.Kuna wakati nilikuwa najaribu kufuatilia aina ya marafiki zake, hakika utagundua ana marafiki ambao wengi wao wamesheheni maarifa na waliofanikiwa.
Moja ya marafiki zake ni Dk.Jakaya Kikwete ambaye ni Rais wetu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Huyo ndio Kinana na hapo sijamtaja mzee Yusufu Makamba(Baba Januari) na wengine kibao lakini angalia tu aina ya marafiki niliokutajia utagundua Kinana ni wa aina gani.
Lakini nikukumbushe Kinana ni miongoni mwa vijana wa enzi hizo ambao waliaminiwa kwa kiwango kikubwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Kwanza Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Kinana aliamianiwa sana na Mwalimu Nyerere na hata chanzo chake cha kutoka jeshini na kuingia kwenye siasa ni baada ya Mwalimu Nyerere kumtaka aingie kwenye Chama kuongeza nguvu.
Baada ya Kinana kupelekwa kwenye Chama naye akaamua kuwachukua Kikwete, Mosses Nnauye(Baba yake na Nape).Mzee Nnauye alishatangulia mbele ya haki, tumuombee kwa Allah amuepushe na adhabu za kaburini.Mwingine aliyechukuliwa na Kinana alikuwa Kapteni John Komba (Marehemu) pamoja na Yusufu Makamba na kuwa nao kwenye Chama.Kila mmoja akawa na majukumu yake.Leo wazee hao kila mmoja ameacha alama kwenye nafasi yake ndani ya siasa za Tanzania.
Nihitimishe kwa kueleza hivi; tunamuomba Mwenyezi Mungu azidi kumpa afya njema na maisha marefu mzee Kinana. Mchango wako katika nchi hii bado unahitajika sana. Tunahitaji kuendelea kupata ushauri wake, kupata maelekezo yake, kupata maoni yake na kubwa zaidi tunahitaji kuona akiwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kupiga hatua.
Kinana anafanya kazi nzuri ya kumsaidia Rais Samia kwa upande wa Chama chao(CCM).Kabla ya kumaliza naomba nieleze hivi ipo siku Mzee Kinana nitakualika kwenye chakula cha mchana huku uswahili kwetu, nikishindwa basi mimi nitajialika mwenyewe nyumbani kwake, najua utanikubalia hivyo kikubwa tuombe uzima.
Ka-simu kangu
0713-833822
JUNI 11,2015 : Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman na msafara wake ukielekea kukagua mradi wa maji uliopo katika kata ya Bundaza,wilayani Missenyi mkoani Kagera.Ndugu Kinana na ujumbe wake wapo katika ziara za kujenga na kuimarisha chama, kukagua,kuhimiza na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM.
MEI 29,2014; Msafara wa Katibu Mkuu wa CCM,Ndugu Kinana ukivuka katika mto Magara mapema leo asubuhi kuelekea wilayani Babati mkoani Manyara. Kinana ameambatana na Katibu wa NEC Itikadi,na Uenezi Nape Nnauye,wakiwa kwenye ziara ya siku saba ya kukagua kuhimiza na kusukuma miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kufuata Ilani ya Chama,kukagua maandalizi ya uchaguzi ya serikali za mitaa,kusikiliza kero za wananchi na kuzitafututia ufumbuzi.
NOVEMBA 23,2013. Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, asubuhi hii amemaliza ziara yake katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na kuanza safari ya kwenda Kyela ambako ataanza ziara katika mkoa wa Mbeya. Pichani Kinana na wajumbe wa sekretarieti ya CCM, Nape Nnauye (Itikadi na Uenezi) na Dk. Asha-Rose Migiro (Siasa na Uhusiano wa Kimataifa), wakiwapungia mikono wananchi wa Nyasa, baada ya kupanda Mv Songea katika bandari ndogo ya Mbamba Bay, kuanza safari ya kwenda Kyela ambayo ilichukua zaidi ya saa 18. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Nyasa, Ernest Kahindi.
APRILI 9,201 : Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Kinana akihutubia umati wa Wananchi katika kijiji cha Kutugongo, wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
NOVEMBA 22,2013 : Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akitumia mtumbwi kwenda na kurudi katika Kijiji cha Lupingu, mkoani Njombe, alipokwenda kusikiliza kero za wakazi wa maeneo hayo mawili ambao hutumia Mv Ruhuhu kuvuka mto Ruhuhu, leo Nov 22, 2013. Kero kubwa ya kivuko hicho ni kutofanya kazi kufuatia kina cha maji ya mto huo kinapopungua hivyo kulazimika kutumia mitumbwi. Kulia ni Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro.
MACHI 14, 2015 : Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akishiriki palizi na baadhi ya wakulima kwenye shamba la mpunga Mto wa Mbu,Monduli mkoani Arusha.
NKASI April 02, 2014 : Wanahabari waliokuwa kwenye msafara wa Katibu Mkuu wa CCM,Ndugu Kinana wakiwa hoi kabisa,wakisubiri kudra za Mwenyezi Mungu,msafara wa magari yao yanasuliwe na kuendelea na safari.Picha hii imepigwa na Katibu Mkuu,Ndugu Kinana.
NKASI April 02, 2014 ; Katibu Mkuu wa CCM,Ndugu Abdulrahman Kinana akimueleza jambo Mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini,Mh.Ali Mohammed Kessy,walipokuwa wakitembea kwa miguu kufuatia msafara huo kukumbana na changamoto ya barabara mapema jana jioni katikati ya Msitu wa hifadhi ya wilaya ya Nkasi.Ndugu Kinana na Msafara wake ulikuwa umetoka kijiji cha Namanyere kuelekea kijiji cha Mwampemba kusikiliza matatizo ya Wananchi na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 100,lakini iliwachukua zaidi ya saa 12 kwenda na kurudi kutokana na ubovu wa barabara.Ndugu Kinana yuko Mkoani Rukwa,Katavi na Kigoma kwa ziara ya siku 21 ya kuimarisha Chama cha CCM,kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kiwemo na kuzisikiliza kero mbalimbali za wananchi
MACHI 23,2015 : Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akikatisha kwenye migomba alipokuwa akikagua mifereji ya inayotiririsha maji kuelekea kwenye mashamba ya ndizi akiongozana na Mh. Agrey Mwanri.
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana amewasili katika jimbo la Siha, katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua kuhimiza na kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo katika jimbo la Siha imetekelezwa kwa asilimia kubwa ikisimamiwa na Mbunge wa jimbo hilo na Naibu Waziri wa TAMISEMI Mh. Agrey Mwanri.
By Mpekuzi
Post a Comment