MAOFISA WA MAHAKAMA WASHAURIWA KUTUMIA MWONGOZO WA KUKABILIANA NA UKATILI WA KIJINSIA |Shamteeblog.




Balozi wa Sweden nchini Mhe.Anders Sjoberg(katikati) akitoa jana jijini Dar es salaam salamu za kuwaaga wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), viongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na masuala wanawake (UN Women ) mara baada ya kumaliza muda wake kufanya kazi ya Ubalozi hapa nchini .
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake nchini(TAWJA) Mhe. Joaquine De-Mello(kulia) akitoa salamu jana Jijini Dar es salaam wakati wakimuaga Balozi wa Sweden nchini Mhe.Anders Sjoberg(katikati) mara baada ya kumaliza muda wake kufanya kazi ya Ubalozi hapa nchini .
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na masuala wanawake (UN Women) Hodan Addou(kushoto) akitoa salamu jana Jijini Dar es salaam wakati wakimuaga Balozi wa Sweden nchini Mhe.Anders Sjoberg(katikati) mara baada ya kumaliza muda wake kufanya kazi ya Ubalozi hapa nchini .


Balozi wa Sweden nchini Mhe.Anders Sjoberg(katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama mara baada ya kutoa salamu zake jana Jijini Dar es salaam za kuwaaga wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), viongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na masuala wanawake (UN Women ) mara baada ya kumaliza muda wake kufanya kazi ya Ubalozi hapa nchini .

Picha na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania

*************
Na Tiganya Vincent-Mahakama


Balozi wa Sweden nchini Mhe. Anders Sjoberg ametoa wito kwa maafisa wa Mahakama nchini kutumia kitabu cha Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu kinachohusu ukatili wa kijinsia ili kuwawezesha wanawake na wasichana kupata haki zao .

Mhe. Sjoberg ametoa kauli jana tarehe 3 Agisti, 2022 jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa salamu za kuwaaga wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na viongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na masuala wanawake (UN Women ) mara baada ya kumaliza muda wake kufanya kazi ya Ubalozi hapa nchini wakati wa kikao cha siku moja cha wadau hao.

Amesema Kitabu hicho kinatoa fursa na mbinu bora za kushughulikia masuala yanasababisha ukosefu wa haki na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na wasichana nchini Tanzania.

Aidha, Mhe. Sjoberg ameongeza kuwa nchi ya Sweden itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wengine katika kusaidia mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na kutetea usawa wa kijinsia.

“Upatikanaji wa haki ni haki ya msingi ya binadamu na kwa pamoja, tunaweza kuhakikisha upatikanaji haki sawa kwa wote bila kumuacha mtu nyuma,” amesisitiza.

Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake nchini(TAWJA) Mhe. Joaquine De-Mello amesema Kitabu hicho kinatoa mwanga juu ya ukubwa na tatizo la ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na uhusiano wa mfumo dume unavyochangia tatizo hilo.

Amesema Kitabu kitawasaidia maofisa wa Mahakama kufanya rejea thabiti wakati wa matumizi ya sheria na kuwaongoza katika masuala ya kiutendaji wa kukabiliana na dhana potofu zinazokwamisha upatikanaji kwa wanawake Mahakamani.

Mhe. De-Mello ameishukuru Sweden kwa kuendelea kusaidia katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na maeneo mengine hapa nchini.

“Kwa kheri mpendwa wetu Anders Sjoberg Balozi wa Sweden nchini Tanzania unayemaliza muda wako!”amesema.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na masuala wanawake (UN Women) Hodan Addou amesema Serikali kwa kushirikiana na Mahakama na wadau wengine wanaweza kuhakikisha vikwazo vinavyowakabili wanawake na wasichana katika kupata haki vinaondolewa.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post