WANANCHI NA WAKULIMA HALMASHAURI YA DODOMA WASHAURIWA KUTEMBELEA MAONESHO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI NANE-NANE |Shamteeblog.


Na. Josephina Kayugwa, DODOMA

WANANCHI na wakulima wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa kutembelea maonesho ya wakulima na wafugaji-Nanenane ili kuweza kujifunza na kupata elimu kuhusu kilimo cha mbogamboga na faida zake.

Ushauri huo ulitolewa na mwakilishi wa Kikundi cha Wanawake wanaojishughulisha na Kilimo (BIBEO Farm) Agness Billah wakati akitoa elimu juu ya umuhimu wa kilimo cha mbogamboga na faida zake.

“Wananchi watembelee maonesho ya Nanenane, kuna vitu vingi vyakujifunza ikiwemo kilimo cha mbogamboga. Kilimo hiki kina faida nyingi, hakitumii gharama kubwa. Mtu anaweza kulima hata akiwa nyumbani kwake, pia bidhaa zikishalimwa kuna wengine wanaweza kuchukua na kutengeneza vitu vingine kupitia mazao ambayo yameshalimwa na wakulima. Hivyo, nawashauri wakulima na wananchi waendelee kuja katika maonesho kujifunza mengi zaidi” alisema Billah.

Sambamba na hilo Billah aliishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwapa fursa zaidi wakulima katika maonesho kuonesha kile ambacho wanakifanya na kukipata kupitia kilimo.

“Tumepewa fursa na serikali kwa kupata mikopo mbalimbali kwaajili ya kuendeleza kilimo na kuleta maendeleo katika Taifa. Tunaishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutupa nafasi yakuonesha kile tunachokifanya. Kupitia maonesho ya Nanenane bidhaa zetu ambazo zimetokana na kilimo zitatambulika pia wakulima na wananchi watajifunza zaidi kuhusu kilimo” alisema Billah.

Maonesho ya Nanenane mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu inayosema “Wekeza katika Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa maendeleo ya Viwanda”.




By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post