Maswali tete watuhumiwa kujinyonga mahabusu |Shamteeblog.




Dar es Salaam. Wakati vituo vya Polisi vikiaminiwa kuwa sehemu salama, matukio ya watuhumiwa kujinyonga wakiwa mahabusu ya vituo hivyo yameibua maswali ya usalama huo.

Tukio la hivi karibuni la aliyekuwa fundi ujenzi, Gaston Moshi kudaiwa kujinyonga akiwa mahabusu ya kituo cha Polisi cha Bonanza jijini Dodoma, limeibua hisia tofauti miongoni mwa wananchi, huku ndugu zake wakidai kuwa aliteswa kabla hajafa.

Tukio lingine ni la Januari 22 mwaka huu, ambapo ofisa wa Polisi, Grayson Mahembe alidaiwa kujinyonga kwa tambala la deki akiwa mahabusu ya Kituo cha Polisi mkoani Mtwara.

Tukio hilo lilifuatia kuuawa kwa mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamisi aliyeshikiliwa na Polisi mkoani humo, ambapo maofisa saba wa Polisi wameshitakiwa kwa kuhusika na kifo chake.


Tukio kama hilo limetokea Septemba 13, mwaka huu, ambapo Nicholaus Mushi (27) alijinyonga kwa tambala la deki akiwa katika mahabusu ya kituo kikuu cha polisi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Desemba 2020 lilitokea lingine lililomuhusisha Stella Moses (30) aliyejinyonga katika mahabusu ya kituo cha polisi Mburahati.

Victoria Wenga (51) alikatisha uhai wake akiwa mahabusu jijini Arusha mwaka 2016, baada ya kujinyonga kwa kutumia shuka lake la kujifunika.


Kadhalika, Februari 15, 2014 iliripotiwa kuwa Vumi Elias (30) alijinyonga na kupoteza maisha akiwa mahabusu ya kituo cha polisi cha wilayani Momba, tukio ambalo lilithibitishwa na aliyekuwa Kaimu Kamanada wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Robert Mayala.

Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai jana kwa simu, alisema matukio hayo si kigezo cha kuondoa usalama wa mahabusu.

“Mahabusu ni sehemu salama ukitaka kuthibitisha hilo, kibaka awe anafukuzwa na wananchi anakimbilia kituo cha Polisi na kuomba awekwe mahabusu,” alisema.

Aghalabu, matukio hayo ya kujinyonga alisema hutokea chooni mahali ambapo mtuhumiwa anaruhusiwa kuingia peke yake na si kwenye vyumba vya mahabusu.


Katika maelezo yake hayo, alitolea mfano tukio la Mburahati kwamba aliyejinyonga alitumia mavazi yake, ambayo kimsingi ni vigumu kumzuia kuingia nayo.

Kwa mujibu wa Kingai, si furaha ya jeshi hilo kuweka watu mahabusu, hivyo ni vema wazingatie sheria ili kujiepusha na makosa yatakayowaweka hatiani.

Kuhusu taratibu za mtuhumiwa hadi kuwekwa mahabusu, alisema kwa kosa la kwanza anawekwa chini ya ulinzi mkali wakati shauri lake likiendelea, uamuzi wa kuwekwa mahabusu utatokana na aina ya kesi yake kama inadhaminika ama laa.

“Ni utaratibu wa kisheria mtu kuwekwa mahabusu pale anapotuhumiwa ila si lazima kukaa kama kuna mtu anafahamika au polisi wanajua alipo na wanajua uhakika wa kupatikana kwake.


“Ni rahisi anaweza kudhaminiwa tu ilimradi atawajibika hadi shauri lake litakapopelekwa mahakamani afahamishwe na apatikane kiurahisi,” alisema.

Inawezekanaje?

Mwanaharakati wa haki za binadamu, Tito Magoti aliyewahi kukaa mahabusu, alishuku kutokea kwa matukio hayo, akisema hakuna mazingira yanayomwezesha mtu kujinyonga.

Badala yake alisema ni kutokana na uzembe wa walinzi wa siku husika au nia ovu ya polisi.

“Kwa sababu mara nyingi mnakuwa zaidi ya mmoja, watu wanapotoka mahabusu zinafungwa hata ukibaki huruhusiwi kuwa peke yako lazima kutakuwa na watu wengine,” alisema.

Alibainisha kabla ya mtuhumiwa kuingia mahabusu, anaamriwa kuvua mkanda, viatu, kuacha fedha na vitu vingine vyote vinavyomwezesha kujidhuru.


Kuhusu matambala ya deki kutumika, alisema kwa uzoefu wake hakuwahi kuliona mahabusu, badala yake usafi hufanywa kwa kutumia vifaa vingine yakiwemo mafagio.

Hata hivyo, alisisitiza mahabusu hakuna tambala la deki lenye uimara utakaomfanya mtu alifunge na kujinyonga.

Kulingana na Magoti ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu, uchunguzi maalumu ni muhimu ufanyike ili kubaini undani wa matukio hayo.

Haya yanajiri kipindi ambacho Rais Samia Suluhu Hassan ameunda kamati ya watu 12 na sekretarieti ya watu watano itakayoongozwa na Jaji mstaafu Othman Chande na Balozi Ombeni Sefue kwa ajili ya kumshauri juu ya utendaji wa vyombo vya haki jinai.

“Nimeunda kamati ya watu 12 na sekretarieti ya watu watano ambayo itaongozwa na Mwenyekiti Jaji Mohamed Chande Othmani, mwenyekiti na makamu mwenyekiti atakuwa katibu mkuu mstaafu Balozi Ombeni Sefue,” alisema Rais Samia alipowaapisha viongozi wateule Julai 20, mwaka huu.

Kasoro katika haki jinai

Mkurugenzi Msaidizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe alisema mazingira ya mahabusu na changamoto katika mfumo wa haki jinai ni sababu za kutokea kwa matukio hayo.

Massawe alifafanua kuwa mfumo wa haki jinai unapaswa kuzifanya mahabusu na magereza kama vituo vya kurekebisha tabia za wahalifu na sio kuwaadhibu.

“Iwapo mtu ametenda kosa kimsingi atajilaumu, akikutana na adhabu anaendelea kujilaumu, mwisho wa siku anatafuta namna ya kujipumzisha dhidi ya lawama binafsi, hapo ndipo anajiuwa,” alisema.

Lakini, alisema hayo yasingewezekana iwapo mahabusu zingeziba mianya ya mtu kujidhuru, hivyo ipo shida hata katika maeneo hayo ya kuhifadhia watuhumiwa wa uhalifu.

Mtazamo wa kisheria

Mtaalamu wa masuala ya sheria, Dk Onesmo Kyauke alisema mtu kujinyonga mahabusu si suala la kisheria lakini litakuwa hivyo iwapo utabainika uzembe.

“Mtu akitaka kujidhuru hata ufanyeje atajidhuru tu, kwa hiyo ni vigumu kuliingiza kisheria, isipokuwa litakuwa suala la kisheria iwapo itabainika kuna uzembe upande wa mahabusu au magereza, uliosababisha tukio hilo,” alisema.

Alifafanua kuwa kukiwa na mashaka, daktari atatakiwa kuthibitisha sababu ya kifo na kama kuna sintofahamu ndipo uchunguzi wa polisi utahitajika ili kubaini tukio limetokeaje.

Hata hivyo, alisema ikibainika kuwa tukio limesababishwa na mmoja wa maofisa wa mahabusu, litabaki kuwa kosa la mauaji kama mengine na mtuhumiwa atahukumiwa kwa hilo.

Maelezo ya Polisi

Katika ufafanuzi wake, Msemaji wa jeshi hilo, David Misime alisema jeshi hilo linaendelea kuboresha mifumo ya kusimamia watuhumiwa wanapokuwa mahabusu, ikiwemo kujenga vituo vipya na vya kisasa vitakavyoimarisha usalama zaidi.

“Jeshi la Polisi linaendelea kuboresha mifumo ya kusimamia watuhumiwa wawapo katika mahabusu za polisi ikiwepo kujenga vituo vipya na vya kisasa ambavyo vitawezesha mahabusu kuwa salama zaidi ya ilivyo sasa,” alisema.

Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa changamoto chache katika baadhi ya mahabusu, ingawa alisema ni salama.

Iwapo mtu atadhamiria kujidhuru, alisema anaweza kufanya hivyo hata kwa kugonga kichwa ukutani na si kujinyonga pekee, lakini yote hayo hutokana na kukata tamaa.

“Mahabusu hizi zimehifadhi maelfu ya watuhumiwa na wanatoka salama ingawa kuna matukio hayo machache na kwa kipindi kirefu na hata ukilinganisha takwimu za wanaojinyonga wakiwa nje ya mahabusu ni wengi zaidi,” alisema.

Alisema lengo la jeshi hilo ni kushirikiana na jamii kuhakikisha hakuna Mtanzania anayepoteza maisha kwa kujinyonga au kunywa sumu akiwa popote.

Mwananchi




from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post