Mwanza wavuka lengo la kitaifa la utoaji chanjo ya UVIKO-19 |Shamteeblog.

Mkoa wa Mwanza umevuka lengo la kitaifa la utoaji chanjo kamili ya UVIKO-19 kwa wananchi ambalo ni asilimia 70 ifikapo mwezi Disemba mwaka 2022.

Mganga Mkuu Mkoa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachunzibwa amesema hadi kufikia Oktoba 17, 2022 wananchi milioni 1.6 kati ya milioni 1.8 kwa mjibu wa Sensa ya mwaka 2012 wamepata chanjo kamili ya UVIKO-19 ikiwa ni sawa na asilimia 87 juu ya lengo la kitaifa.

Dkt. Rutachunzibwa aliyasema hayo Oktoba 18, 2022 wakati akifungua kikao cha tathimini ya chanjo ya UVIKO-19 na Uhuru wa Kupata Taarifa kilichoratibiwa na Chama cha Wanahabari Mkoa Mwanza (MPC) kwa ufadhili wa Shirika la Internews kupitia mradi wa Boresha Habari.

Alisema wakati zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO-19 linaanza nchini Agosti 03, 2021 kulikuwa na upotoshaji uliosababisha changamoto kwa wananchi kuwa tayari kupokea chanjo lakini waandishi wa habari walisaidia kuelimisha jamii.

Pia Dkt. Rutachunzibwa aliwaomba Waandishi wa Habari kuendelea kuhamasisha wananchi kuwa na desturi ya kupima afya hususani magonja yasiyoambukiza kama walivyosaidia kufanikisha utoaji wa chanjo ya UVIKO-19.

Aliwahimiza kushiriki katika maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza itakayoanza kitaifa katika uwanja wa Furahisha kuanzia Novemba 05-12, 2022 ambapo watapata huduma mbalimbali ikiwemo vipimo vya magonjwa hayo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Mkoa Mwanza (MPC), Edwin Soko aliwakumbusha wanahabari kuendelea kuelimisha wananchi kuwa tayari kupata chanjo mbalimbali ikiwemo UVIKO-19 hatua itakayowaweka salama huku wakihakikisha wanaondoa ombwe la habari zisizo sahihi kwa wananchi hususani kuhusu chanjo ya UVIKO-19.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mganga Mkuu Mkoa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachunzibwa akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwenyekiti wa MPC, Edwin Soko akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwanahabari Tonny Alphonce akichangia mada kwenye kikao hicho.
Picha ya pamoja


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post