Na Shamimu Nyaki
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango ameziagiza Taasisi na Mashirika ya Umma pamoja na Makampuni Binafsi kuhakikisha Bajeti iliyotengwa kwa ajili ya shughuli za Michezo haibadilishwi Matumizi.
Mhe. Mpango ametoa agizo hilo Novemba 20, 2022 jijini Tanga wakati akifungua Mashindano ya Michezo kwa Mashirika ya Umma, Taasisi za Serikali na Makampuni Binafsi (SHIMMUTA) mwaka 2022.
Mhe. Mpango amesema Waajiri wahakikishe Watumishi wao wanashiriki michezo hiyo kila mwaka kwakua inajenga undugu, upendo kubadilisha uzoefu mahala pa kazi pamoja na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
"Kabla ya Kalenda ya Michezo hii, lazima kuwe na mabonanza mbalimbali ili Wanamichezo wajiandae vyema, nawasihi pia kuendelea kuzingatia Sheria Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma wakati wote wa mashindano" amesema Mhe. Mpango.
Amesisitiza Viongozi wa Shirikisho hilo kuhamasisha wanamichezo wengi zaidi kushiriki michezo hiyo, huku akiwaasa waamuzi watakaochezesha michezo hiyo kufuata Sheria na kutenda haki katika michezo hiyo.
Aidha, amewagiza Wakuu wa Taasisi kuhakikisha watumishi wao wanakua na vifaa vyote vinavyohitajika wakati wa mashindano, pamoja na kuhakikisha timu zinajiandaa vyema kabla ya michezo
Awali Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba amesema Mkoa huo umeweka mazingira vyema ikiwemo ulinzi na usalama siku zote za Mashindano.
Amewaasa Wanamichezo hao kutembelea vivutio vya Utalii vyilivyopo Tanga ikiwemo mapango ya Amboni, Hifadhi za Taifa za Mkomazi na Saadani ili kuwa mabalozi wa Utalii na kufurahia Mkoa huo.
Michezo hiyo itadumu mpaka Novemba 29 mwaka huu na itahusisha timu 52 zitazoshiriki michezo takriban 12 na inaongozwa na Kauli Mbiu "Michezo ni Fursa tuitumie vyema kuimarisha Afya za Wafanyakazi kwa Uchumi imara wa Taifa".
By Mpekuzi
Post a Comment