MCHEZO wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Namungo FC umemalizika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa wenyeji kupata ushindi wa bao 1-0.
Bao la Simba limewekwa kimiani na Moses Phiri dakika ya 32 na kuifanya kufikisha pointi 24 ikiwa nafasi ya pili nyuma ya vinara Azam FC wenye 26 huku Namungo ikisalia ya saba na pointi 15.
ZIFUATAZO NI DONDOO MUHIMU ZA MCHEZO HUO
Bao la Moses Phiri linamfanya nyota huyo kufikisha mabao sita katika Ligi Kuu Bara hadi sasa akizidiwa bao moja tu na mshambuliaji kinara wa Mbeya City, Sixtus Sabilo ambaye ana saba.
Tangu Namungo imepanda rasmi Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/20 huu ni mchezo wake wa saba kukutana na Simba ambapo imefungwa mara tano na kutoka sare miwili bila ya ushindi wowote.
Katika michezo hiyo Namungo FC imefunga mabao matano tu katika kipindi hicho chote huku wao wakiruhusu nyavu zao kutikiswa na Simba mara 14.
Kabla ya mchezo huu mara ya mwisho kwa timu hizi kukutana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ilishinda pia bao 1-0, Novemba 3, mwaka jana lililofungwa na mshambuliaji wake wa zamani, Meddie Kagere anayeichezea Singida Big Stars.
Kipigo kikali ilichokipata Namungo dhidi ya Simba kilikuwa cha mabao 4-0, Julai 18, 2021, kwa mabao ya Meddie Kagere, John Bocco na Chris Mugalu aliyefunga mawili.
Kipigo hiki kwa Namungo FC ni cha nne hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara katika michezo 11 iliyocheza ambapo kati ya hiyo imeshinda minne na kutoka sare mitatu.
from Author
Post a Comment