WAKULIMA WILAYA YA MAGU WAPATA MAFUNZO YA KILIMO CHA PAMBA CHENYE TIJA KUPITIA MRADI WA BEYOND COTTON |Shamteeblog.

Mkulima wa Kijiji cha Chandulu Wilaya ya Magu mkoani Mwanza akijifunza kupanda mbegu za pamba kwa kutumia teknolojia rahisi inayotumia muda mfupi baada ya kupata mafunzo kupitia mradi wa ‘Beyond Cotton, unaotekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI), Bodi ya Pamba (TCB) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP)
Mafunzo ya upandaji mbegu kwa kumia teknolojia rahisi yakiendelea.
Mafunzo ya uunganishaji wa mashine ya kufanyia palizi ya pamba yakifanyika.
Mafunzo ya ujenzi wa matenki kwa kutumia teknolojia rahisi yakitolewa kwa mafundi wa kijiji hicho.
Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa TARI, Profesa Joseph Ndunguru akizungumzia mafunzo hayo.

Wanawake wa Kijiji cha Chandulu wakiwa kwenye mafunzo ya lishe.
Mtaalamu wa masuala ya Lishe akitoa mafunzo.
Mkazi wa Kijiji cha Chandulu, Modesta Ngando akiandika aina ya vyakula wakati wa mafunzo hayo.
Mafunzo ya kuweka mbegu kwenye mashine rahisi ya kupandia mbegu za pamba yakifanyika.


Washiriki wa mafunzo hayo wa Kijiji cha Chandulu wakiwa katika picha ya pamoja na wataalam kutoka katika mashirika hayo.


Na Dotto Mwaibale, Mwanza

WAKULIMA wa Kijiji cha Chandulu kilichopo Wilaya ya Magu mkoani Mwanza wameanza kupata mafunzo ya kuzalisha na kuongeza tija kwenye mnyororo wa thamani wa zao la pamba na mazao mengine ya chakula lishe.

Mafunzo hayo yanatolewa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI), Bodi ya Pamba (TCB) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) baada kutiliana saini mkataba wa mashirikiano ya kiutendaji (MoU) katika eneo la mradi wa kuzalisha na kuongeza tija kwenye mnyororo wa thamani wa mazao hayo.

Mradi huo wa mwaka mmoja unaojulikana kama ’‘Beyond Cotton, unafadhiliwa na Serikali ya Brazil kwa gharama ya Dola za kimarekani 629,000, na kutekelezwa na taasisi hizo, ambao umeanza kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo wa zao la pamba takribani 9,000 kutoka wilaya za Magu, Kwimba na Misungwi.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyoanza wiki iliyopita Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa TARI, Profesa Joseph Ndunguru alisema wakulima wameanza kupata mafunzo ya teknolojia mbalimbali ya kilimo cha pamba chenye tija chini ya mradi wa ‘Beyond Cotton.

Alisema mafunzo yanayotolewa ni ya teknolojia rahisi ambazo zinahitajika kwenye kilimo cha pamba kama vile mashine rahisi za bei nafuu za kupandia zao hilo ambazo zilikuwa zimeletwa katika mafunzo ili wakulima hao wadogo waweze kujifunza namna ya kuzitumia.

Alitaja mashine nyingine iliyoletwa katika mafunzo hayo kuwa ni mashine ya palizi na vifaa vya kupimia hali ya hewa ambavyo vinamsaidia mkulima kujua akipata mvua kiasi gani anaweza kwenda kuanza kupanda mazao yake.

"Teknolojia zingine zilizofundishwa ni lishe kwani katika mradi huu wa ‘Beyond Cotton' unaangalia pia uboreshaji wa lishe ambapo kilimo hicho kitakachofanyika zaidi katika mashule ambacho kitakuwa ni cha maharagwe lishe, viazi lishe na mbogamboga." alisema Ndunguru.

Aliongeza kuwa ili kufanikisha kilimo hicho yatajengwa matenki ya teknolojia rahisi kwa ajili ya kuvuna maji ambayo yatatumika kumwagilia mazao hayo pamoja na matumizi mengine.

Alisema mashamba hayo yatakayokuwepo katika shule hizo yatatumika kama mashamba darasa ambapo wakulima kutoka maeneo mengine watafika kujifunza pamoja na teknolojia ya utengenezaji wa matenki hayo.

Aidha Ndunguru alisema mafunzo hayo yanaendelea hadi kwenye usindikaji na uchakataji wa mabaki ya pamba na kutengeneza bidhaa ambazo zitaongeza thamani ya zao hilo.

Awali akizungumza hivi karibuni wakati wa kusaini mkataba huo, Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Geofrey Mkamilo alipongeza serikali ya Brazili na Tanzania kupitia Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono na mtazamo chanya katika kuhakikisha zao la pamba na mazao mengine ya chakula yanaendelezwa na kuongezewa tija kwa manufaa ya wakulima wake na ukuaji wa uchumi.

Mkamilo alisema kwa namna serikali zote mbili zilivyojipanga, chini ya utekelezaji wa wadau mbalimbali, watahakikisha matokeo ya utekelezaji wa mradi huo yanakwenda kuleta ustawi na ongezeko la ubora na uzalishaji kwenye zao la pamba na kilimo mseto.

Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson, alisema ndani ya mfumo wa Ushirikiano wa Kusini-Kusini, Mradi wa ‘Beyond Cotton’ unalenga zaidi kubadilishana maarifa kati ya Tanzania na Brazili katika mustakabali chanya unaolenga kuongeza tija katika kilimo cha pamba na mazao mengine ya chakula, pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani, ikiwemo kuwaunganisha wakulima na masoko ya ndani na nje.

“Naishukuru Serikali ya Brazil kupitia Shirika la Ushirikiano la Brazili, kwa kufadhili mpango huu, na kwa kuwachukulia wakulima wadogo wa Tanzania kama wadau watarajiwa katika sekta ya pamba. Pia ningependa kushukuru Chuo Kikuu cha Shirikisho cha Campina Grande na Taasisi ya Pamba ya Brazili kwa kusaidia mradi huu" alisema.

Mwakilishi wa TCB, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi wa bodi hiyo, James Shimbe, alisema ustawi, tija na ongezeko chanya la uzalishaji wa zao la pamba nchini linategemea zaidi utafiti. Hivyo katika kutekeleza azma ya mradi huo TCB, TARI na WFP wamejipanga kuhakikisha wanashirikiana kwa karibu na halmashauri zote zitakazofikiwa ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI-Ukiruguru mkoani hapa, ambaye pia ni mratibu wa zao la Pamba nchini, Dkt. Paul Saidia, aliainisha baadhi ya mambo yatakayotazamwa zaidi katika utafiti kulingana na mkataba huo kuwa ni pamoja na kuongeza thamani kwa kuwa na mbegu bora za pamba, kuongeza usalama wa chakula na namna ya kupambana na magugu.

“Na tunatarajia wakulima takribani 9,000 wa pamba watakaofikiwa wataelimishwa juu ya kilimo cha maharagwe lishe, viazi lishe na mbogamboga.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Mathias Masalu akizungumza kwa niaba ya wakulima aliyashukuru mashirika hayo kwa kuwapelekea mafunzo hayo ambayo yatawaletea tija katika kilimo hicho na akatumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali watu wa chini kwa kuwapekekea mpango huo ambao unakwenda kuwakomboa kiuchumi.

Mkazi wa Kijiji hicho Modesta Ngando alisema mafunzo ya lishe waliopatiwa na Mtaalamu Profesa Vannote kutoka Chuo Kikuu cha Shirikisho cha Campina Grande cha nchini Brazili yamewanufaisha kwani walikuwa hawajui kuwa wakila wali na maharagwe na kunywa majiwa wakati huo huo wanaharibu kabisa mlo huo ambapo walielezwa kuwa wanapokula chakula hicho wasinywe maziwa hadi baada ya masaa manne au zaidi


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post