Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Makete
NAIBUWaziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha huduma za mawasiliano nchini kwa kuwekeza katika miundombinu itakayosaidia katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.
Akizungumza juzi (Novemba 26, 2022) wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua miundombinu mbalimbali ya watoa huduma za mawasiliano katika Wilaya ya Makete mkoani Njombe, Naibu Waziri huyo amesema kuwa Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuboresha sekta ya mawasiliano nchini ambapo ametolea mfano uwekezaji unaofanywa katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
“Awali bajeti ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa ilikuwa shilingi bilioni nane kwa mwaka, lakini Mhe. Rais Samia ametenga shilingi bilioni 230 kwa ajili ya ujenzi wa huu, Mkongo huu wa Taifa wa Mawasilino utakuwa na faida mbalimbali ikiwemo kusaidia minara ifanyekazi pamoja na kupunguza gharama za huduma mawasiliano nchini”. Amesisitiza Mhe. Naibu Waziri Kundo.
Akifafanua zaidi kuhusu jitihada za Serikali kwa kushirikiana na Wizara za kuboresha huduma za mawasiliano anasema “Oktoba 2021 tumetangaza zabuni za ujenzi wa minara 763 nchi nzima. Aidha, miradi 168 imeshatekelezwa na miradi 188 inaendelea kutekelezwa”.
Kuhusu uwekezaji huo wa miundombinu unaofanywa nchi nzima, Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Juma Sweda ameishukuru Serikali kwa jitihada zake za kuboresha huduma za mawasiliano katika wilaya yake huku akiwasisitiza wananchi kutumia huduma hizo kwa lengo kuinua uchumi wao.
“Tunashuhudia fursa hii muhimu ya ujenzi wa mnara wa mawasiliano hapa Makete ambayo itasaidia kuboresha mawasiliano ya simu lakini pia ni ulinzi”. Amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
By Mpekuzi
Post a Comment