Kanisa la Nabii Suguye lafungwa, ulinzi mkali |Shamteeblog.



Huduma za kiroho katika Kanisa la The Word of Reconciliation Ministries (WRM) la Kivule- Matembele ya pili, jijini Dar es Salaam zimesitishwa huku ulinzi wa Jeshi la Polisi ukiimarishwa ili kuzuia huduma yoyote isifanyike.



Dar es Salaam. Huduma za kiroho katika Kanisa la The Word of Reconciliation Ministries (WRM) la Kivule- Matembele ya pili, jijini Dar es Salaam zimesitishwa huku ulinzi wa Jeshi la Polisi ukiimarishwa ili kuzuia huduma yoyote isifanyike.

Huduma ya kanisa hilo lililo chini ya Nabii Nicolaus Suguye imezuiliwa kwa zaidi ya wiki mbili zilizopita, huku waumini zaidi ya 4,000 wakidai kupewa maelekezo ya kutakiwa kutafuta maeneo mengine ya kuabudu.

Vyanzo vinaeleza kanisa hilo lilikuwa ni miongoni mwa taasisi ambazo hazijapata usajili rasmi, isipokuwa barua ya usajili wa awali inayoruhusu kufanya huduma sehemu moja bila kualika wageni kutoka nje, kufungua matawi na kufanya makongamano huku Serikali ikifanya uchunguzi wa mwenendo wake.

ALSO READ
Ochuka arejeshwa Kenya, anyongwa-10
Kimataifa 16 hours ago
Kijiji ambacho ni marufuku kunywa pombe
Kitaifa 16 hours ago
“Baada ya uchunguzi wa mamlaka za usajili imeonekana huduma ya WRM imepungukiwa sifa za kupata usajili kamili, hivyo ikapewa notice ya kuzuiwa kuendelea na shughuli, ikisajiliwa ataruhusiwa kuendelea na shughuli za kutoa huduma ya neno la Mungu,” kilieleza chanzo.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema kwa sasa anayelalamikia si yeye (Suguye) kwani yeye anajua kanisa halina usajili na anajua kwa nini amefungiwa.

Muliro alisema wao ni wasimamizi wa sheria na wanapaswa kuzilinda, “na kama (kufungiwa) ingekuwa ni kinyume cha sheria au taratibu unafikiri wenye kanisa wangekaa kimya? Kuna vitu haviko sawa kuhusiana na taasisi hiyo ya dini na lazima vitimie.”

Gazeti hili tangu juzi na jana liliwatafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na naibu wake, Jumanne Sagini ambao taasisi za dini ziko chini ya wizara yao, lakini hawakupokea simu na wakati mwingine zilizimwa.

Msemaji wa wizara hiyo, Christina Mwangosi alipokea simu mara moja na alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo aliomba apigiwe baadaye.

Hata hivyo, alipotafutwa baadaye hakupokea tena na mwandishi alipofika ofisi za msajili wa taasisi hizo jijini Dar es Salaam alikutana na maofisa waliomwambia hawawezi kulizungumzia suala hilo isipokuwa msemaji.

Suguye, anayetambuliwa na waumini wake kama nabii, alianza kutoa huduma za kiroho mwaka 1998 kabla ya kuanzisha kanisa hilo mwaka 2007.

Kanisa hilo limefungwa ikiwa ni mwaka mmoja baada ya wizara hiyo chini ya ofisi ya Msajili wa Jumuiya, Emmanuel Kihampa kutangaza mabadiliko ya hadhi ya vyeti vya usajili wa taasisi za kidini na jumuiya mbalimbali za kijamii inayoelekeza kuhuisha vyeti vya usajili kila baada ya miaka mitano.

Pia limefungiwa ikiwa ni miezi minne baada ya Nabii Suguye kuibua mjadala ufunuo wa kucha na nywele, akidai Mungu wake kuagiza waumini kutoa kucha za kidole cha mwisho cha kushoto (mguu na mkono) na nywele za utosini na paji la uso kisha kufunga kwenye kitambaa cheupe ili awaponye.



Hali ilivyo kanisani

Jana, gazeti hili lilifika katika kanisa hilo eneo la Kivule- Matembele ya pili, saa 8 mchana na kukuta limezungushiwa utepe wa njano.

Mwandishi alipojaribu kuingia alizuiliwa na walinzi walioeleza hakuna anayeruhusiwa kuingia eneo hilo, licha ya kushawishi kwa utambulisho wa kitaaluma bila mafanikio.

Mwandishi: Bwana Yesu asifiwe wapendwa, kwa nini pamefungwa kuingia kanisani?

Mlinzi: Amina mtumishi. Huduma zimesitishwa na hakuna anayeruhusiwa kuingia hapa. Ni maelekezo tuliyopewa.

Mwandishi: Poleni sana kwa changamoto, Mungu atawavusha. Naomba kuongea na Nabii, mimi ni mwandishi wa habari natokea gazeti la Mwananchi.

Mlinzi: Hapana huyo unayemuhitaji hayupo, ukihitaji maelezo unaweza kuwafuata, maelekezo tuliyopewa ni kuzuia mtu yeyote bila kujali ni nani. Huduma zimesimama zaidi ya wiki mbili zilizopita.

Suguye hakupatikana kwa njia ya simu, lakini mkewe alipokea na hakutaka kutoa ushirikiano wowote licha ya kuuliza utambulisho wa aliyepiga simu kisha kukata simu.

Mwandishi: Mama, bwana Yesu asifiwe

Mama Mchungaji: Amina, naongea na nani?

Mwandishi: Unaongea na mwandishi wa gazeti la Mwananchi, poleni kwa changamoto ya kufungiwa huduma. (Hakujibu kisha kukata simu ghafla).

Hili ni kanisa la pili kufungiwa na Serikali baada ya kusitisha shughuli zote za ibada katika Kanisa la ‘Mfalme Zumaridi’ chini ya Diana Bundala, eneo la Iseni, jijini Mwanza kabla ya kufunguliwa kesi ya kuendesha ibada kinyume cha sheria ya usajili wa vyama na jumuiya za kijamii sura 337.



Ujumbe mtandao wa kijamii

Suguye alipotafutwa kwa njia ya simu hakupokea wala kujibu ujumbe, lakini baada ya kufungiwa huduma Desemba 13, mwaka huu katika ukurasa wake wa Facebook aliweka ujumbe unaosomeka; “1Petro 1:7” Ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.”

Pia siku tano zilizopita akaweka ujumbe wa salamu za kurejea kutoka ziara yake katika majimbo manne nchini Marekani alikoalikwa, huku akiwashirikisha Watanzania kuomba katika kufunga mwaka na kuombea Taifa, ili kupata mvua, baraka na mafanikio kupitia maombi yao.



Kuhusu usajili

Kisheria ili kusajili taasisi hizo za kidini, mwombaji anatakiwa kuwa na nakala za katiba, kujaza fomu mbili yenye wasifu wa viongozi, muhtasari wa vikao, kulipia ada ya maombi ya usajili, ada ya usajili, ada na tozo ya kila mwaka baada ya kusajiliwa na kuwasilisha ripoti ya utendaji na fedha ya kila mwaka.

Mwananchi


from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post