Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
Golikipa wa Kimataifa wa Mali, Djigui Diarra ameongeza mkataba wa miaka miwili na Young Africans SC ambapo atasalia Klabuni hapo hadi msimu wa 2024-2025 ikiwa ni mara ya kwanza tangu asajiliwe msimu wa 2021-2022.
Diarra aliibuka kuwa Golikipa bora wa Lig Kuu Soka Tanzania Bara msimu wa 2021-2022 wakati Yanga SC wakitwaa mataji yote matatu ya Ligi Kuu, Ngao ya Jamii na Michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) na kuisaidia timu hiyo ya Wananchi kufuzu makundi ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC).
Yanga SC wamethibitisha kuongeza mkataba wa Nyanda huyo waliyemsajili katika Kikosi cha Stade Malien ya Mali, kupitia Rais wa Klabu, Mhandisi Hersi Said amesema: “Tunaendelea kufanyia kazi ripoti ya Benchi la Ufunndi, kwa sasa hatujengi timu, hiyo hatua tulishaivuka misimu kadhaa nyuma. Sasa hivi tunaendelea na mazungumzo na Wachezaji wetu Nyota kuhakikisha wanabaki na kuendelea kuwapa furaha mashabiki wetu.”
“Diarra ni mmoja wa Wachezaji muhimu kwenye Kikosi chetu, kama Uongozi tuna furaha amekubali kubaki kuendelea kuvaa Jezi ya Yanga,” amesema Mhandisi Hersi.
Kwa upande wake, Nyanda Diarra amesema: “Ni siku ya furaha sana kwangu, nashukuru kwa Uongozi wa Yanga kwa kuniongeza mkataba. Yanga ni klabu kubwa Afrika na bila shaka ni ndoto ya wachezaji wengi kucheza hapa.
“Niwaahidi Mashabiki wa Yanga SC kuwa nitaendelea kujituma na kuhakikisha timu yetu inafanya vyema kwenye Michuano ya ndani na Kimataifa,” amesema Diarra.
By Mpekuzi
Post a Comment