Utawala wa Rais wa Kenya William Ruto unachunguza vitendo vya ukwepaji kodi uliofanywa na makampuni pamoja na familia kubwa za kitajiri nchini humo.
Kwa mujibu wa gazeti la Sunday Nation, Katibu Mkuu wa Hazina (Profesa Ngujuna Ndung’u ( pichani) pamoja na Mwenyekiti wa mamlaka ya kodi nchini humo ( KRA) Anthony Ng’ang’a Mwaura wamethibitisha kufanyika kwa zoezi hilo.
Wawili hao wamesema kuwa wanachunguza makampuni ambayo aidha yalipewa msamaha wa kutolipa kodi au yalikwepa kulipa kodi kwa makusudi.
” Kuna sheria ya msamaha wa kodi tutaifuatilia kwa umakini zaidi kujua,” amesema Ndung’u.
Sunday Nation limesema kuwa taarifa za ndani zinasema makampuni yatakayoathirika zaidi na zoezi hilo ni yale yanayomilikiwa na vigogo waliokuwa na nguvu wakati wa utawala uliopita wa Rais Uhuru Kenyatta.
Familia hizo zinadaiwa kuwa na nguvu sana kiasi kwamba zilikuwa ni ngumu kuzigusa licha ya uwepo wa sheria.
Amesema makampuni mengi yanayochunguzwa yalikwepa kulipa kodi kwa sababu viongozi wake walikuwa karibu sana na watendaji wakubwa serikali, hivyo waliihujumu KRA kimapato.
Na kwa mujibu wa Mwaura, baadhi ya makampuni hayo hajawahi kulipa kodi toka Kenya ilipopata Uhuru.
Ametolea mfano wa kampuni ya kutengeneza Wine na Spirit inayomilikiwa na kigogo wa serikali iliyopita kuwa inadaiwa kodi kiasi cha bilioni 7.6 na KRA.
” Linapokuja suala la kulipa kodi, kila mtu anatakiwa alipe kodi,”
” Hata Rais mwenyewe analipa kodi zinazomhusu,”
” Hata mimi mwenyewe nalipa kodi,” amesema.
” Katika utawala wa Kenya Kwanza, kila mtu atalipa kodi , hata vigogo na makampuni ambayo yalikuwa hayaguswi sasa yatalipa kodi,” amesema.
Zoezi hilo linakuja wakati ambapo utawala wa Kenya Kwanza ukiwa katika presha ya kukusanya mapato kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Makusanyo yanatakiwa kufikia trilioni 3, huku kukiwa na madeni katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Na katika kupigilia msumari jambo hilo, Makamu wa Rais ( DP) Rigathi Gagachua amesema hivi karibuni kuwa kila mtu anatakiwa alipe kodi nchini humo.
Wachambuzi wanasema kwa mantiki hiyo, zoezi hilo haliwalengi waliokwepa kodi katika utawala uliopita tu, lakini pia linawahusu wanaokwepa kodi katika utawala wa sasa wa Rais Ruto.
Hivi karibuni, maseneta wa Kenya Kwanza walitoa wito wa kuchunguzwa kwa familia ya Rais wa zamani Uhuru Kenyatta kwa misamaha ya kutolipa kodi iliyoipata wakati wa utawala wa Kenyatta.
The post Matajiri, makampuni kutikiswa kwa ukwepaji kodi appeared first on KITENGE BLOG.
By Author
Post a Comment