DC KILAKALA ASISITIZA MIRADI KUKAMILIKA KWA WAKATI ILI WANANCHI WAPATE HUDUMA |Shamteeblog.


Na Hadija Bagasha Tanga

Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mussa Kilakala amewataka wasimamizi wa miradi yote ya maendeleo kwenye eneo lake kuhakikisha miradi hiyo inasimamiwa kwa viwango vinavyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi. 

Kilakala amesema miradi hiyo inapaswa kusimamiwa vizuri ili kuhakikisha inakamilika na kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi 
ili iendane na mpango wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuleta fedha kwenye Wilaya hiyo kwajili ya maendeleo ya wananchi. 

Kilakala ametoa maelekezo hayo wakati alipofanya ziara katika Kata ya Masaika Wilayani Pangani yenye lengo la kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali sambamba na kufanya mkutano wa hadhara kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi. 

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ametembelea na kukagua ujenzi wa miundombinu ya usafi chini ya program ya uendelevu wa usambazaji wa maji na usafi wa mazingira vijijini (SRWSSP) katika zahanati ya Masaika ambao umepokea kiasi cha shilingi 49,000,000.00.

 Miradi iliyokaguliwa ikiwa katika hatua za utekelezaji inahusisha ujenzi wa choo cha mashimo 03 kwa ajili ya wagonjwa, ukarabati wa choo cha mashimo 02 kwa ajili ya watumishi, ujenzi wa kichomea taka, shimo la kutupia kondo la nyuma, shimo la kutupia majivu, ujenzi wa kinawia mikono, ujenzi wa mnara wa tanki la maji na uingizaji wa maji katika jengo la zahanati. 

Aidha Kilakala amepongeza maendeleo ya kazi ya ujenzi na kusisitiza mradi huo kusimamiwa vizuri ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kutoa huduma kwa wananchi.

Sambamba na mradi huo katika zahanati ya Masaika Mkuu wa Wilaya alifika katika Kijiji cha Kigurusimba na kukagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Masaika ambayo ilipatiwa fedha za ujenzi kiasi cha shilingi 584,280,028.28 kupitia mradi wa kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP).

 Miundombinu iliyojengwa katika shule hii ilihusisha; ujenzi wa nyumba 08 vyumba vya madarasa, jengo la Utawala, vyumba 03 vya maabara za sayansi, jengo la maktaba, jengo la TEHAMA na vyoo matundi 11 (wavulana matundu 05 na wasichana matundu 06) kwa ajili ya wanafunzi.

 "Pamoja na fedha hizo shule hii pia imepokea fedha kiasi cha shilingi 98,000,000.00 kupitia mradi huo wa kuboresha elimu ya sekondari kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya walimu mbili kwa moja ikiwa na vyumba 03 kila moja ambapo taratibu kumpata fundi zinakamilishwa, "amesisitiza DC Kilakala.  

Hata hivyo Kilakala amewapongeza wananchi kwa kushiriki katika ujenzi wa shule hiyo ikiwa ni ishara ya kuunga mkono dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha elimu katika Wilaya ya Pangani.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post