KUELEKEA UTEKELEZAJI WA MRADI WA KUBORESHA MIFUMO YA CHAKULA NCHINI, MWENDAMTITU MBARALI KUIMARISHA ULINZI NA KUKOMESHA MIFUGO KWENYE SKIMU |Shamteeblog.

 
Mwenyekiti wa skimu ya umwagiliaji Mwendamtitu iliyopo Mbarali mkoani Mbeya Evaristo Mgiya

Na Christina Cosmas, Morogoro

WAKULIMA wa mpunga kwenye skimu ya Mwendamtitu iliyopo Wilayani Mbarali mkoani Mbeya wamejipanga kuimarisha ulinzi na kuhakikisha mifugo haiingii mashambani na kuharibu utaratibu wa mradi wa kuboresha mifumo ya chakula na kuleta tija ya kilimo unaotarajiwa kuanza mwakani hapa nchini.

Mwenyekiti wa skimu ya umwagiliaji ya Mwendamtitu iliyopo Wilayani Mbarali Evaristo Mgiye alisema hayo kwenye Kongamano la wadau wa Wizara ya kilimo na FAO wakijadili mbinu za kuanza kutekeleza mradi huo mara baada ya mwaka mmoja kuanzia sasa ambao utatekelezwa kwenye nchi 35 duniani ikiwemo Tanzania unaofadhiliwa na mfuko wa mazingira (GEF).

Mgiye alisema watahakikisha watakaoingiza mifugo na kuharibu miundombinu ikiwemo barabara wanachukulia hatua kali za kisheria ili kuiweka skimu kwenye mazingira bora na kuleta tija ya mradi huo.

Aidha aliiomba Serikali kuwaongezea nguvu ya kuboresha miundombinu kwenye skimu hiyo ambayo ina uwezo wa kuiingizia Halmashauri pato la shilingi Bilioni 1.5 kwa mwaka itakayotokana na kila gunia la mpunga kukatwa kwa shilingi 1,000 na kuwezesha suala la chakula nchini.

 “serikali itujengee miundombinu kwa maana mifereji ina changamoto kubwa ya kujaa mchanga, pamoja na kujenga, suala la mchanga linapaswa kuchukuliwa hatua kwa utaalamu kwa kuangaliwa zaidi sababu maji yakipita kipindi cha mvua mchanga unaletwa mwingi, ambao unafanya maji yanasambaa na kupotea sababu ya kupoteza mwelekeo na ujenzi huo utasaidia kuondoa upotevu wa maji pia” alisema Mgiye.

Mgiye alisema kwa kila hekari huzalisha gunia 30-35 kwa sasa ambapo wakulima bado wanakosa mazao baada ya mifereji kujaa mchanga na ikiwa changamoto hiyo itatatuliwa wataweza kuzalisha gunia 35-40 kutokana na eneo lenye ukubwa wa hekta 15,000 walilopo.

Alisema wameshatumia zaidi ya shilingi Milioni 100 katika kufanya tathmini ya uharibifu na kupata ramani halisi ya eneo kwenye skimu hiyo kama walivyoelekezwa ambapo wanaiomba Serikali kuona namna ya kurejea kuwasaidia ili kukamilisha ujenzi kwenye eneo hilo.

Naye Afisa Umwagiliaji kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wilayani Mbarali mkoani Mbeya Titus Osano alisema Tume imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa wakulima na kuhakikisha miundombinu na mazingira yanayowazunguka yanakuwa katika hali ya usawa kulingana na matakwa ya mradi huo.

Alisema uharibifu wa mazingira unachangiwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo kama vile wa bonde la Usangu ambapo wao wanatoa elimu itakayowahakikishia kupata uzalishaji mkubwa kwenye mazao wanayolima huku wakitunza mazingira.

Osano alisema kwa kutumia katiba na sheria zilizopo kwenye kila skimu watahakikisha miti inazidi kupandwa kuzunguka vyanzo vya maji na kuhakikisha makopo ya viuatilifu yanachomwa au yanatunzwa kwenye mazingira mazuri zaidi ili kuepusha athari zozote za kijamii na mimea.

Akizungumzia bonde la Usangu alisema zipo zaidi ya skimu 70 katika bonde hilo huku kukiwa na vyama vya wakulima vingine vilivyopata kibali kuendeleza kilimo katika maeneo hayo ambazo zinapaswa kufuata kanuni bora za kilimo huku zikizingatia utunzaji wa mazingira.

Hivyo Osano aliwashauri wakulima kuhakikisha wanafuata miongozo ya skimu za umwagiliaji zilizopo chini ya serikali na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kutunza miundombinu ambayo ni mifereji na vyanzo vya maji na kufuata taratibu zilizopangwa katika kuhakikisha skimu hizo zinaratibiwa vizuri kwa kufuata miongozo iliyopo.

Mradi wa kuboresha mifumo ya chakula (food systems integrated program) unatarajia kutekelezwa baada yam waka mmoja kuanzia sasa katika maeneo ya Usangu jijini Mbeya na Zanzibar kwa kutumia zaidi ya Dola za kimarekani Milioni 9 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 20 za kitanzania.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post