Na Veronica Mwafisi - Dodoma
Mameneja na Wataalam wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma Barani Afrika wanatarajia kukutana jijini Arusha nchini Tanzania kujadili mikakatika mbalimbali itatakayosaidia kujenga rasilimaliwatu yenye tija katika Bara la Afrika.
Hayo yamesemwa Oktoba 25, 2024 na Rais wa Mtandao wa Mameneja wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMNet) ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Bw. Daudi amesema katika mkutano huo wajumbe watapata fursa ya kubadilishana uzoefu na utaalam kwa lengo la kuwezesha nchi za Bara la Afrika kupiga hatua za kimaendeleo kwa kutumia mbinu za kisasa.
“Mtandao huu umeanzishwa kwa lengo la kutafsiri mikakati ya maendeleo ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kujenga uwezo wa rasilimaliwatu yenye matokeo chanya katika kuhudumia wananchi wetu Barani Afrika. Bw. Daudi amesema.
Amesema mtandao huo unaundwa na wanachama kutoka Bara lote la Afrika ambao wamegawanyika katika Kanda tano ikiwemo Afrika Magharibi yenye Nchi 17, Afrika Mashariki Nchi 10, Afrika ya Kati Nchi 8, Afrika Kaskazini Nchi 6 na Nchi za Kusini mwa Afrika 13.
Bw. Daudi amesema Tanzania ni nchi mwanachama wa APS-HRMNet hivyo imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa 9 wa mwaka utakaowakutanisha Mawaziri wenye dhamana ya Utumishi wa Umma, Makatibu Wakuu, Wanataaluma na Wataalam mbalimbali kutoka Barani Afrika.
Mkutano wa Mtandao wa Mameneja wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMNet) unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 4 hadi 7 Novemba, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa jijini Arusha.
Kaulimbiu ya Mkutano huo ni Uhimilivu wa Utawala na Ubunifu Kukuza Sekta ya Umma yenye Uelekeo wa Baadae Kupitia Uongozi wa Rasilimaliwatu’.
By Mpekuzi
Post a Comment