Na Dotto Kwilasa, KILIMANJARO
Wizara ya Katiba na Sheria imeanzisha kambi mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kutoa mafunzo ya uraia na utawala bora, huku ikielekeza juhudi zake katika kutoa elimu ya masuala ya sheria kwa wananchi.
Mafunzo haya ni sehemu ya mpango wa Wizara wa kufikisha huduma za kisheria kwa wananchi ili kukuza utawala bora na haki za binadamu katika jamii.
Hatua hii ya kuendesha mafunzo mkoani Kilimanjaro inafuatia mara baada ya mafunzo ya yaliyotolewa mkoani Mtwara kwa viongozi wa ngazi mbalimbali, kuanzia mkoa, wilaya, kata, hadi vijiji.
Pia, mkoa wa Mtwara ulikuwa na kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, ambapo wananchi walipatiwa huduma za kisheria bure katika halmashauri zote tisa za mkoa huo.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji wa Haki, Jane Lyimo, ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yanawaleta pamoja viongozi na wadau wa haki kwa ajili ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya kiutendaji.
Amesisitiza kuwa mpango huu utaziba ombwe lililopo kwenye jamii kwa kuwaachia wananchi wa chini nafasi ya kujua na kuelewa haki zao, hivyo kuwapa fursa ya kufaidika na huduma za kisheria.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa mafunzo haya yatasaidia katika kuboresha utawala bora na kupunguza matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu, na kwamba baada ya mkoa wa Kilimanjaro kupokea mafunzo haya, watendaji na viongozi wataweza kuboresha huduma kwa wananchi na kuhakikisha sheria zinafuatwa ipasavyo.
"Tupo hapa kusikiliza kero za wananchi na kuenenda kwa misingi ya haki na maendeleo kwa nchi yetu," amesema Jane Lyimo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Yusuf, alieleza kuwa mafunzo haya ni ya muhimu sana kwa viongozi na watendaji wa mkoa, kwani yatawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa haki na kuleta manufaa kwa jamii.
Amesema kuwa viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wana jukumu la kutumia mafunzo hayo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa misingi ya utawala bora.
"Ni matumaini yetu sisi kama viongozi wa Mkoa mtayafanyia kazi mafunzo haya katika kufanikisha na kuleta tija kwenye majukumu yenu," amesema Kiseo Yusuf.
Mratibu wa Mafunzo hayo, Prosper Kisinini, amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuboresha huduma kwa wananchi na kuwaongoza watendaji kutoa huduma bila ubaguzi, kwa kuhakikisha kuwa sheria na haki zinatimizwa kwa usawa na ufanisi.
Amesema mafunzo haya ni hatua muhimu katika kuboresha usimamizi wa haki za binadamu na kuhimiza utawala bora katika mikoa mbalimbali, na hivyo kutengeneza mazingira bora ya kisheria kwa wananchi wa Tanzania.
By Mpekuzi
Post a Comment