TAKUKURU YAREJESHA MILIONI 137.8 BAADA YA KUBAINI RUSHWA YA VIWANJA KAHAMA |Shamteeblog.

Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy,  akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo, Februari 4, 2025 kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha robo ya pili kuanzia Oktoba hadi Disemba 2024/2025. Picha na Marco Maduhu

Na Mwandishi wetu - Shinyanga

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imeokoa jumla ya shilingi milioni 137.8 kutokana na fedha za mauzo ya viwanja katika Manispaa ya Kahama. Hii ni baada ya kubaini kwamba baadhi ya watu waliomilikishwa viwanja walikwepa kulipa gharama halisi za mauzo hayo.

Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, amebainisha hayo leo, Februari 4, 2025, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha robo ya pili kuanzia Oktoba hadi Disemba 2024/2025.

Amesema katika kipindi hicho, TAKUKURU imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi milioni 137.8, ikiwa ni sehemu ya malipo ya viwanja 29 vilivyopimwa na Manispaa ya Kahama mwaka 2019. Kati ya viwanja hivyo, ni vitatu pekee ambavyo vililipwa kwa gharama halisi, huku viwanja 26 vikilipwa chini ya kiwango kilichowekwa na Manispaa.

“Manispaa ya Kahama ilikuwa na ardhi katika eneo la Phantom, ambalo lilipimwa na kuuzwa kwa wananchi mwaka 2019. Viwanja hivyo vilipaswa kumilikishwa kwa bei ya shilingi 15,000 kwa mita moja ya mraba, na viwanja vya biashara vikiuzwa kwa shilingi 20,000 kwa mita moja ya mraba,” amesema Kessy.

Ameongeza kuwa, mwaka 2024, TAKUKURU ilipokea taarifa kupitia vyanzo vyake vya siri zikielezea kuwa baadhi ya wananchi walimilikishwa viwanja hivyo bila ya kulipa gharama halisi. Baada ya uchunguzi, walibaini kuwa kati ya viwanja 29, vitatu pekee ndivyo vilivyolipwa kwa gharama halali, wakati viwanja 26 vililipa kiasi kidogo kilichokuwa kinyume na bei halisi, ambacho kilikuwa na thamani ya jumla ya shilingi milioni 800.

“Kutokana na uchunguzi wetu, tulifanikiwa kuwafikia wamiliki wa viwanja 26, na kuwataka walipie kiasi kilichobaki cha fedha kulingana na gharama halali. Hadi sasa, shilingi milioni 137.8 zimekusanywa, na tunafanya juhudi kuhakikisha kwamba fedha zilizobaki, takriban shilingi milioni 662.2, zitapatikana na kuingizwa serikalini,” amefafanua.

Kwa upande mwingine, Kamanda Kessy amesema kuwa TAKUKURU imepokea malalamiko 38 kuhusu rushwa katika kipindi hicho, ambapo 20 ni ya rushwa na 18 ni ya masuala yasiyo husu rushwa. Uchunguzi wa malalamiko haya unaendelea. 

Aidha, Kessy ameongeza kuwa TAKUKURU imejipanga kuzuia vitendo vya rushwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu, 2025.

Kamanda Kessy amewataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa taarifa pindi wanapoona vitendo vya rushwa, ikiwa ni pamoja na kwenye miradi ya maendeleo, ili hatua za haraka zichukuliwe.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post