MITENDEWAWA YABAHATIKA KUPATA MRADI MKUBWA WA UMEME |Shamteeblog.

Kaimu Afisa Habari wa Huduma kwa Wateja TANESCO Ruvuma Emma Ulendo akizungumza na wananchi wa Mitendewawa
 
Afisa Habari na Uhusiano Tanesco Mkoani Ruvuma Allan Njiro akizungumzia namna ya kulinda miundombinu ya umeme katika kijiji cha Mitendewawa

Wananchi waliojitokeza kupata elimu ya jinsi ya kupata fomu ya maombi ya kupata umeme Mitendewawa



Na Regina Ndumbaro - Ruvuma

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma limeendelea na ziara yake ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza miundombinu ya umeme. 

Ziara hiyo imefanyika katika kijiji cha Mitendewawa, kata ya Mshangano, ambako wananchi walipata fursa ya kufahamu hatua mbalimbali za kuhakikisha wanapata na kutumia umeme kwa usahihi.

Afisa Habari na Uhusiano wa TANESCO mkoani Ruvuma, Allan Njiro, amesema kuwa mradi mkubwa wa umeme umefanikiwa kutekelezwa katika kijiji cha Mitendewawa.

 Hata hivyo, mradi huo ulipitia changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vifaa maalum, hali iliyopelekea ucheleweshaji wa kukamilika kwa wakati uliotarajiwa. 

Pamoja na hayo, amewashukuru wananchi wa Mitendewawa kwa kuwa wavumilivu wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Njiro ameongeza kuwa katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya umeme, kijiji cha Mitendewawa kimebahatika kufungiwa transfoma mbili kwa ajili ya matumizi ya wananchi. 

Ameeleza kuwa kwa wale ambao bado hawajapata huduma ya umeme, mpango wa kuendelea na mradi mwingine upo na unatarajiwa kutekelezwa ifikapo mwezi Julai.

Aidha, amewakumbusha wananchi kuwa ni jukumu lao kuhakikisha miundombinu ya umeme inatunzwa vizuri ili kuepusha hasara kubwa inayoweza kutokea. 

Amewataka kuepuka ukataji miti kiholela karibu na nyaya za umeme na kuwa makini na matapeli wanaoweza kuwalaghai katika upatikanaji wa huduma hiyo. 

Pia, ameonya kuwa uharibifu wa miundombinu ya umeme husababisha hasara kubwa kwa serikali na kuwanyima wananchi huduma ya umeme.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Habari wa Huduma kwa Wateja TANESCO Ruvuma, Emma Ulendo, amewashauri wananchi kuhakikisha wanafanya wiring kwa kutumia vifaa bora. 

Ameeleza kuwa maombi ya kuunganishiwa umeme yanaweza kufanywa kupitia ofisi za TANESCO Ruvuma au kwa njia ya mtandao kwa kutumia mfumo wa "NIKONEKTI" unaorahisisha ujazaji wa fomu. Pia, amesisitiza umuhimu wa kulipa ada za umeme kupitia benki au simu ili kuepuka udanganyifu.

Ulendo ameongeza kuwa wale ambao bado hawajafanya wiring wanapaswa kutuma maombi haraka ili waweze kufanikisha upatikanaji wa huduma hiyo. 

Ameeleza kuwa umeme una faida nyingi, ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani ya ardhi na kurahisisha shughuli za biashara na maendeleo mengine ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mshangano, Samweli Mbano, ameishukuru TANESCO mkoani Ruvuma kwa jitihada zao za kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya umeme. 

Ameeleza kuwa elimu hiyo itawasaidia wananchi kuutumia umeme kwa usalama na kuhakikisha miundombinu inatunzwa ipasavyo.

Mbano pia ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhakikisha wananchi wa maeneo ya vijijini wanapata huduma ya umeme. 

Ameeleza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi na uchumi wa taifa kwa ujumla.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post