
Dar-es-Salaam
Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini, Bi. Stella Tullo amesisitiza umuhimu wa mashauri kumalizika kwa wakati na kwa Haki ili kuhakikisha wananchi wanapata haki za
umiliki wa ardhi zao kwa haraka kwani ardhi ni rasilimali muhimu ya kuwawezesha kuendesha
shughulli za kujipatia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Bi. Tullo ameyasema hayo Februari 12, 2025, alipokutana na mawakili wa kujitegemea katika
kikao kazi kilichofanyika kwenye ofisi za ndogo za Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, Bi.Tullo amewataka mawakili na wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi jijini Dar es Salaam kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na kuzingatia muda wa mashauri ili kuharakisha uamuzi wa kesi.
Ameeleza kuwa lengo ni kuhakikisha mashauri yote yanamalizika ndani ya muda mfupi, huku akisisitiza kuwa mashauri yaliyodumu Barazani zaidi ya miaka miwili yanapaswa kupewa kipaumbele zaidi yamalizike kwa haki na kwa haraka ili kupunguza msongamano wa kesi.
Aidha, Bi.Tullo amewapongeza wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi jijini Dar es Salaam kwa ushirikiano wao mzuri na wadau wa utoaji haki.
Msajili ameridhishwa na juhudi zao za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu za mashauri ya ardhi, pamoja na ushiriki wao wa dhati katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini.
"Tumeona maendeleo chanya kutokana na ushirikiano wenu na mihimili mingine ya utoaji haki. Ni muhimu tuendelee kushirikiana ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati," alisema Bi. Tullo.
Kwa upande wake Wakili Geofrey akizungumza kwa niaba ya mawakili wa kujitegemea, amemshukuru Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba kwa kuitisha kikao hicho na kusema wamepa fursa ya kujadili changamoto na kupata suluhisho la pamoja kwa
ajili ya kuboresha utendaji kazi.
"Tunamshukuru Bi.Tullo kwa kutupa nafasi ya kushiriki kwenye kikao hiki muhimu.Tumepata
fursa ya kujadili masuala muhimu ambayo yameimarisha mahusiano yetu na kutukumbusha
wajibu wetu wa kuhakikisha mashauri yote yanamalizika kwa wakati," alisema Wakili Geofrey.
Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini yamekuwa na jukumu muhimu katika kuhakikisha
migogoro ya ardhi inatatuliwa kwa wakati na kwa haki. Hatua hii ya Msajili wa Mabaraza ya
Ardhi inatarajiwa kuongeza ufanisi na kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi nchini kote.

By Mpekuzi
Post a Comment