
Na Lydia Lugakila - Bukoba.
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera umetahadharishwa juu ya matumizi mabaya ya Mitandao ya kijamii huku chama hicho kikisema hakitahusika kwa namna yoyote ile pale kijana atakayekiuka sheria za mtandao hata kama atakuwa ni kiongozi wa chama hicho.
Tahadhari hiyo imetolewa na viongozi mbali mbali wa chama cha Mapinduzi CCM ngazi ya Mkoa na Wilaya wakati wakizungumza na vijana wapatao 285 kutoka kata 29 za Wilaya ya Bukoba katika mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo Wenyeviti, Makatibu wa umoja huo yaliyofanyika katika ukumbi wa Bukoba Resort uliopo kata Kemondo Wilayani humo.
Akizungumza katika mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Sima amesema kuwa Vijana hao wana dhamana kubwa katika Nchi hii ambapo Chama na Serikali vinawategemea hivyo wanatakiwa kusimamia nafasi zao kwa kufuata kanuni sheria na taratibu za chama ikiwa ni pamoja na kujihadhari na tabia mbaya zinazoweza kuhatarisha amani hasa matumizi mabaya ya mitandao.
DC Sima amesema kuwa kuna baadhi ya Vijana wanatumia vibaya simu zao badala ya kuzitumia kwenye mawasiliano na kujitafutia fursa za kiuchumi wanazitumia kutoa lugha chafu kwa viongozi wao waliopo madarakani.
"Uwe kiongozi wa Chama uwe wa Jumuiya uwe wa Wilaya uwe wa Mkoa uwe wa Taifa kukaa unaandika maneno ya kubeza na kutukana viongozi hiyo haikubaliki",amesema Dc Sima.
Ameongeza kuwa viongozi waliopo madarakani wanatakiwa kuheshimiwa hivyo wao kama viongozi watashughulika na vijana wenye tabia za kutumia vibaya mitandao.
Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Vijana hao kutambua kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia kwani kuna miradi mingi imeletwa katika Wilaya hiyo hivyo zawadi kubwa kwa Rais huyo ni kumpa ridhaa ya kuongoza miaka mingine mitano .
Katibu Mwenezi CCM Mkoa wa Kagera Hamimu Mahmoud amesema kuwa Vijana hao ni tegemeo la Chama hivyo wanatakiwa kutovuruga amani na utulivu uliopo kupitia mitandao au majukwaa mbali mbali
"Hatutakuwa na namna ya kumsaidia kijana yeyote atakayeenda kinyume hata kama atakuwa kiongozi wa chama kwani sheria ni msumeno jiadhari na matumizi mabaya ya mtandao", amesema Hamimu.
Ameongeza kuwa sheria za Mtandao hazitamtambua kada wa chama wala nani hivyo watumie mitandao hiyo kujinufaisha, kueleza mazuri yaliyofanywa viongozi wao, na kuwa nidhamu ndiyo itakayowavusha na kufikia malengo yao.

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika mafunzo hayo Mbunge wa Bukoba vijijini Dkt. Jasson Rweikiza amewataka vijana kuwa mstari wa mbele kukisemea Chama,kuwasemea mazuri viongozi ikiwa ni pamoja na kuisoma ilani na katiba ya Chama cha Mapinduzi ili waelewa malengo ya chama hicho pamoja na kanuni ya UVCCM ili wazifahamu na ikitokea wamekutana na watu wanaobeza chama wawajibu kwa hoja.
"Mwaka huu ni wa uchaguzi lazima vijana mjitambue kukisemea chama ili kisonge mbele pia mtambue mazuri yaliyofanywa na Rais Samia hasa katika Wilaya yetu kwani tumejionea miradi mikubwa ikiwemo ya maji, umeme, Barabara, Hospitali, kujengwa kwa vituo vya afya, Madaraja makubwa" amesema Dkt. Rweikiza.
Mbunge huyo ameongeza kuwa Vijana hao pia wanatakiwa kuendelea kutunza amani na utulivu kwani Nchi nyingi bado zinataabika na migogoro inayosababisha machafuko.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania Wilaya ya Bukoba Joyce Namatovu alisema Vijana wengi wanatumia mitandao vibaya kutokana na ukosefu wa elimu hivyo watumie mafunzo hayo kujitambua wenyewe pamoja kutumia mitandao kujiletea fursa mbali mbali kuliko kutumia katika mambo yasiyofaa.
Naye Katibu wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Kagera Christina Hussein amewaomba Vijana kuzingatia maadili ya chama na kujiepushe na vurugu zinazohatarisha amani.
"Msitumie mitandao kama majukwaa ya kukikosesha heshima na thamani chama chetu inauma nasema tutawafuatilia" amesema katibu huyo.
Hata hivyo Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukoba Andrew Byera amesema Vijana ni nguzo imara ya chama hivyo wahakikishe wanalinda na kuendeleza misingi ya chama hicho ikiwa ni pamoja na kuonesha nidhamu kwa viongozi wao.
By Mpekuzi
Post a Comment