
Mbunge wa Jimbo la Madaba Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama akiwapungia mkono wananchi wa kijiji cha Lituta Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma

Mbunge wa Jimbo la Madaba Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama akicheza ngoma wakati wa mapokezi yake kijiji cha Lituta Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma
Wananchi wa kijiji cha Lituta Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma wakimshangilia Mbunge wa Jimbo hilo Dkt Joseph Kizito Mhagama
Na Regina Ndumbaro-Madaba.
Katika mkutano wa wananchi na wanachama wa Kijiji cha Lituta, Halmashauri ya Madaba, Mbunge wa Jimbo hilo, Dkt. Joseph Kizito Mhagama, ameishukuru jamii kwa mapokezi mazuri na uungwaji mkono wanaompa katika safari yake ya uongozi.
Wananchi wa Lituta walichanga fedha kwa ajili ya kumuwezesha kuchukua tena fomu ya ubunge kwa uchaguzi wa mwaka huu, jambo ambalo Mhagama amelipokea kwa furaha na shukrani.
Amewaahidi wananchi hao kuwa ataendelea kuwatumikia kwa bidii na kuhakikisha maendeleo yanaimarika katika maeneo yote ya jimbo hilo.
Katika hotuba yake, Mhagama ameeleza kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye thamani ya shilingi bilioni 7.69 katika sekta tofauti kijiji cha Lituta.
Katika sekta ya afya, amesema kuwa hospitali ya wilaya imekamilika, ikiwa na vifaa vyote muhimu kwa utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, ameeleza kuwa maendeleo katika sekta za barabara, elimu, umeme na maji yamefanyika kwa kiwango kikubwa, na kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika miradi hiyo ili kuimarisha maisha ya wakazi wa Madaba.
Pamoja na mafanikio hayo, Mhagama ameonesha masikitiko yake kuhusu vitendo vya wizi vilivyofanywa na baadhi ya watu walioiba vifaa vya Hospitali ya Halmashauri ya Madaba.
Amesema kuwa wahusika wamebainika, majina yao yamehifadhiwa, na hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi yao.
Amehakikisha kuwa hospitali hiyo inaendelea kutoa huduma bila shida, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana katika kulinda miundombinu ya umma ili kuendeleza maendeleo yaliyopatikana.
Katika sekta ya miundombinu, Mhagama ameeleza kuwa ujenzi wa barabara na madaraja unaendelea, huku zaidi ya shilingi bilioni 1.5 zikiwa zimetumika katika mradi huo.
Amesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha barabara zote za lami zinajengwa ndani ya Halmashauri ya Madaba, ikiwa ni pamoja na barabara ya Kifaguro.
Vilevile, amesema mradi wa maji utaimarishwa zaidi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji safi na salama.
Mhagama amewataka wananchi wa Lituta na Madaba kwa ujumla kuwa na mshikamano na kutoacha mtu yeyote kuvuruga maendeleo yao kwa maslahi binafsi.
Amesema kuwa maendeleo yaliyopatikana ni matokeo ya juhudi za pamoja, na akawataka wananchi kutokubali maneno ya upotoshaji dhidi ya viongozi wanaowahudumia.
Amewasihi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao kwa kuchagua viongozi wanaoleta maendeleo kwa Madaba.
By Mpekuzi
Post a Comment