RC MACHA AWASISITIZA WANAWAKE KUJITOKEZA KUSHIRIKI FURSA ZA KIUCHUMI. |Shamteeblog.



Na. Paul Kasembo, MSALALA DC

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewasihi wanawake na wasichana mkoani Shinyanga kujitokeza kwa wingi kushiriki katika fursa mbalimbali za kiuchumi na ujasiriamali zinazojitokeza ili kujiimarisha kiuchumi.


RC Macha ameyasema haya Machi 6, 2025 kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kimkoa yamefanyika Kata ya Bugarama, Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na kuhudhuriwa na Viongozi wa Taasisi za Serikali na Binafsi,Watumishi pamoja na wanachi, maadhimisho yenye Kaulimbiu “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji”.


“NIchukue fursa hii kuwahimiza wanawake na wasichana wote kujitokeza kushiriki katika fursa mbalimbali za kiuchumi na ujasiriamali zinazojitokeza ili kujiimarisha kiuchumi”, amesema RC Macha.


Aidha RC Macha ameongeza kwa kuwasihi wananawake kutumia nishati safi ya gesi na umeme ili kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuifanya Tanzania iwe na matumizi ya nishati safi na utunzaji wa mazingira.


Akiwasilisha taarifa fupi ya shughuli zilizofanyika kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake kwa siku 3, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga Bi. Rehema Edson amesema kuwa wamefanikiwa kushirikiana na wajasiriamali 15, Taasisi takribani 9 zimeshiriki maonesho na kutoa huduma, zoezi la ugawaji miti ili kutunza mazingira pamoja na kongamano kubwa la wanawake ambapo wanawake takribani 466 walihudhuria na kupata elimu ya masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi mkoani Shinyanga Dkt. Regina Malima ameshauri kuanzishwa kwa sera na mikakati ya kuwakwamua wanawake na wasichana kiuchumi sambamba na utoaji elimu endelevu ili wafahamu fursa zilizopo za kuwawezesha kiuchumi.


Maadhimisho ya Siku ya Wanawake mkoani Shinyanga yamehitimishwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Anamringi Macha ambaye ndiye mgeni rasmi ambapo yaliambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo maandamano, kutembelea mabanda ya maonesho pamoja na utoaji hundi za mikopo ya Serikali ya asilimia 10 kwa vikundi kwenye Halmashauri.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post