RC MACHA AWATAKA WANAWAKE KUWA WALEZI BORA NA KUPINGA UKATILI NA UBAGUZI DHIDI YA WATOTO |Shamteeblog.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha akizungumza na wanawake waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya siku ya wanawake Mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika Machi 6, 2025, Bugarama Halmshauri ya Msalala

NA NEEMA NKUMBI -MSALALA


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amewataka wanawake kuwa walezi bora kwa kuwapa watoto wao elimu itakayowasaidia kuwa viongozi wazuri.


Hayo yamesemwa Machi 6, 2025, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake kwa Mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika katika Kata ya Bugarama, Halmashauri ya Msalala, RC Macha amesema kuwa elimu inawasaidia wanawake wengi kuwa viongozi wazuri.


"Tusimame pamoja kupinga ukatili wa kijinsia na kuendelea kuwa walezi bora bila ubaguzi. Watoto wote ni sawa, tuwalee katika msingi bora pia mjitokeze katika fursa za kiuchumi," amesema RC Macha.


Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Rehema Edson, amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Mkoa wa Shinyanga umepanga kutoa zaidi ya shilingi bilioni 5, na hadi kufikia Februari 2025, zimetolewa zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa vikundi 119 vya wanawake, 110 vya vijana, na vikundi 10 vya watu wenye ulemavu.


Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Mkoa wa Shinyanga, Regina Malima, amesema katika risala yake kuwa bado wanapambana kuhakikisha wanawake wanashika nafasi mbalimbali za uongozi.


Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Nikolaus, amesema kuwa serikali inawajali wanawake, ndiyo maana imetoa mikopo ya asilimia kumi ili kuwainua wanawake.

Pia amesisitiza kuwa wanawake waende wakazalishe, wafanye tathmini, na warudishe mikopo hiyo ili na wengine waweze kunufaika nayo.

Siku ya wanawake duniani inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 8 mwezi wa tatu, Mwaka huu imebeba kauli mbiu inayosema, "WANAWAKE NA WASICHANA 2025; TUIMARISHE HAKI, USAWA NA UWEZESHAJI," ikiwasisitiza wanawake na wasichana kuongeza juhudi katika kukuza haki, usawa, na uwezo wao katika jamii.




By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post