Mbunge wa Jimbo la Madaba Mhe. Joseph Kizito Mhagama akizungumza na wananchi katika eneo la stendi inayotarajiwa kuanza ujenzi wake wiki ijayo
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba Abdul Manga akizungumza na wananchi kuhusu mradi huo wa ujenzi wa stendi Lituta kitongoji cha Kifaguro Madaba
Mhandisi Jeremiah Chambai akionesha Mchoro wa ramani ya stendi itakayojengwa Lituta Madaba
Wananchi na Wanachama waliojitokeza kumpokea Mbunge Joseph Kizito Mhagama Katika kata ya Lituta kitongoji cha kifaguro Madaba Mkoani Ruvuma
Mbunge wa Madaba Joseph Kizito Mhagama alipowasili katika eneo la kitongoji cha kifaguro ambapo mradi wa ujenzi wa stendi hiyo unaotarajiwa kufanyika
Na Regina Ndumbaro-Madaba.
Ujenzi wa stendi ya mabasi katika Halmashauri ya Madaba, mkoani Ruvuma, unatarajiwa kuanza rasmi mwezi Aprili 2025.
Stendi hiyo itakayojengwa katika kitongoji cha Kifaguro kata ya Lituta, ina gharimu kiasi cha shilingi bilioni 5.
Mbunge wa Madaba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joseph Kizito Mhagama, amethibitisha taarifa hiyo katika kikao cha utekelezaji wa miradi mbalimbali katika jimbo lake.
Amesema kuwa mradi huu ni moja ya hatua kubwa za maendeleo zinazotekelezwa kwa manufaa ya wananchi wa Madaba.
Mhagama amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kipaumbele kikubwa alichotoa kwa wananchi wa Madaba kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ameeleza kuwa, pamoja na mradi wa ujenzi wa stendi, mradi mwingine mkubwa unaoendelea ni wa maji katika Kata ya Mtyangimbole, wenye thamani ya shilingi bilioni 5.500.
Ameongeza kuwa miradi hii inaashiria uwekezaji mkubwa wa serikali katika kuimarisha huduma za kijamii kwa wananchi wa Madaba.
Aidha, Mhagama amewashukuru viongozi wa Halmashauri ya Madaba na wananchi wa Kata ya Lituta kwa kushirikiana kikamilifu katika kuhakikisha mradi huu unafanikiwa.
Amesisitiza kuwa, wakazi wa maeneo jirani kama Mahanje, Matetereka, na Wino pia watanufaika na mradi huu.
Pia ameipongeza kamati ya mradi iliyoundwa kutoka vijiji hivyo kwa mshikamano wao katika kuhakikisha utekelezaji wa ujenzi wa stendi unafanikiwa.
Kwa upande wake, Mhandisi Jeremiah Chambai, ambaye amepewa jukumu la kusimamia mradi huo, amethibitisha kuwa stendi hiyo itajengwa katika eneo lenye ukubwa wa takriban hekari tatu.
Ameeleza kuwa mchoro wa ramani ya stendi hiyo tayari umeandaliwa na wananchi wameonyeshwa jinsi itakavyokuwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba, Abdul Manga, amesema kuwa ujenzi wa stendi hii utafanyika kwa viwango vya juu, ikiendana na hadhi ya stendi kubwa za miji mingine kama Njombe na Tanga na Iringa.
Manga ameongeza kuwa stendi hii italeta manufaa makubwa kwa wakazi wa Madaba, ikiwemo kuboresha biashara na kuondoa kero za usafiri kwa abiria.
Amesema kuwa ujenzi utaanza na awamu ya kwanza kwa gharama ya shilingi milioni 205.
Pia amewataka wafanyabiashara waliopo katika maeneo ya stendi kushiriki katika majadiliano kuhusu mpangilio wa majengo mapya ili kuhakikisha hakuna anayepata hasara na mji wa Madaba unakuwa na taswira inayolingana na hadhi mpya ya stendi hiyo.
viongozi wa Madaba wameeleza matumaini yao kuwa mradi huu utachochea maendeleo makubwa katika eneo hilo.
Wananchi wa Kata ya Kifaguro wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza kilio chao na kuwapatia fedha za mradi huu.
Pia wamempongeza Mbunge wao Joseph Kizito Mhagama kwa kazi kubwa anayoifanya.
Ujenzi wa stendi hii unatarajiwa kubadilisha mazingira ya usafiri na biashara, huku ukiimarisha uchumi wa Madaba na maeneo jirani.
By Mpekuzi
Post a Comment