WANAWAKE WASISITIZWA KUGOMBEA NA KULETA ULINGANIFU KATIKA NGAZI MBALIMBALI ZA UONGOZI |Shamteeblog.

 



NA NEEMA NKUMBI- MSALALA

Wanawake wanatakiwa kuhudhuria na mabinti zao katika makongamano ya wanawake ili kujifunza na kuwajengea uwezo katika maisha.


Hayo yamesemwa Machi 5, 2025, na Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Mkoa wa Shinyanga, Regina Malima, katika kongamano la Wanawake lililofanyika Bugarama, Halmashauri ya Msalala, Mkoani Shinyanga.


"Tunakubali kuwa wanaume ni kichwa cha familia na pia wana mamlaka, lakini kuwa na uchumi mzuri hakukufanyi kuacha majukumu yako kama mwanamke," amesema Malima.


Mbunge wa Viti Maalumu, Santiel Kirumba, amesema kuwa kila mwanamke ana uwezo wa kuwa kiongozi, na kwamba wanawake wanapaswa kujitokeza kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.


"Mwanamke ana uwezo wa kuongoza familia, hivyo anatakiwa pia kuwa na nafasi katika uongozi wa taifa," amesema Kilumba.


Mwezeshaji wa afya ya akili ameeleza kwamba katika jamii tunayoishi, kuna matarajio yanayoleta athari kubwa kwa wanawake, ikiwa ni pamoja na watoto kulazimishwa kuolewa, vipigo, na maneno yasiyostahili, Hali hii inaathiri sana afya ya akili ya wanawake, na inasababisha msongo wa mawazo.


Mwezeshaji huyo amebainisha njia za kuondokana na changamoto za akili, ikiwa ni pamoja na kupata muda wa kulala, kufanya mazoezi mara kwa mara yanayoendana na afya zao, kuwa na mahusiano chanya, na kuchangamana na watu wanaofaa katika maisha yao.


Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga, Lydia Kwesigabo, amesisitiza kuwa wazazi wanatakiwa kuhakikisha ulinzi na usalama wa watoto, kuimarisha mahusiano mazuri kati ya wazazi, na kutoa adhabu sahihi kwa watoto.

"Ukali wa kupitiliza husababisha watoto kuwa waongo," alisema Kwesigabo.


Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Rehema Edson, ameonyesha takwimu za ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, akisema kuwa katika ngazi ya uongozi kuanzia Mkuu wa Mkoa, Makatibu Tawala, Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Idara, Watendaji wa Kata na Watendaji wa Kijiji, wanaume ni 1497 sawa na asilimia 86%, huku wanawake wakiwa ni 243 tu, sawa na asilimia 14%.


Rehema amesisitiza umuhimu wa wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kuweka ulinganifu na usawa katika suala la uongozi.


Kongamano hili la wanawake limebeba kauli mbiu inayosema, "WANAWAKE NA WASICHANA 2025; TUIMARISHE HAKI, USAWA NA UWEZESHAJI," ikiwasisitiza wanawake na wasichana kuongeza juhudi katika kukuza haki, usawa, na uwezo wao katika jamii.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post