
Na Woinde Shizza ,moshi
Diwani wa kata ya Boma Mbuzi Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Juma Rahibu, amewajia juu baadhi ya Watanzania wanaomkashifu na kumtukana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akisema ni ishara ya kuporomoka kwa maadili katika jamii na kudhalilisha heshima ya taifa.
Akizungumza kwa hisia kali katika sherehe za uzinduzi wa kikundi cha mtetezi wa mama , Rahibu alisema ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya watu wakitumia majukwaa ya mitandao ya kijamii na mikusanyiko ya watu kumvunjia heshima kiongozi mkuu wa nchi ambaye, kwa mujibu wake, amekuwa akitekeleza majukumu yake kwa bidii na mafanikio makubwa.
“Huu si ustaarabu Rais Samia anajitahidi kutuletea maendeleo kama barabara, afya, elimu halafu mtu anajitokeza tu na kuanza kumtukana? Tunataka vyombo vya dola viwajibike,” alisema Rahibu.
Diwani huyo alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuenzi maadili ya taifa, hasa heshima kwa viongozi walioko madarakani, huku akionya kuwa uhuru wa kutoa maoni haupaswi kuwa kisingizio cha matusi, kashfa na propaganda zisizojengwa kwenye hoja za msingi.
Katika hatua nyingine, Rahibu alielekeza lawama kwa baadhi ya raia kutoka mataifa jirani ya Kenya na Uganda kwa kile alichokieleza kuwa ni tabia ya kudhalilisha na kumsema vibaya Rais Samia kwenye mitandao ya kijamii.
“Sasa imefika hatua hata baadhi ya Wakenya na Waganda wanathubutu kumtukana Rais wetu? Hii ni dharau ya hali ya juu ,Tanzania si uwanja wa mazoezi wa siasa za kejeli,” alisema kwa msisitizo.
Alisema Tanzania imekuwa nchi ya mfano wa heshima na ustaarabu kwa viongozi wa mataifa jirani, hivyo si haki kuona baadhi ya watu kutoka nje ya nchi wakitumia vibaya uhuru wa mitandao kwa maneno ya matusi dhidi ya kiongozi wa Tanzania.
“Tunawaheshimu viongozi wao, hatujawahi kusikia Watanzania wakimtukana Rais wa Kenya au wa Uganda ,Na wao wajifunze kutufanyia heshima hiyo hiyo,” aliongeza.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wakazi wa Moshi wameonyesha kuguswa na kauli hiyo, wakisema kuwa ni kweli kuwa maadili yanaporomoka na watu kutumia mitandao ya kijamii vibaya.
Esther Kilave, mkazi wa Pasua, alisema:
“Mitandao inatumika kama sehemu ya matusi sasa huu si utamaduni wetu ,Rais Samia anastahili kuheshimiwa kwa kazi anayoifanya.”
John Mlay, fundi umeme mjini Moshi, alisema:
“Tunaona mabadiliko mengi nchini Watu wanapaswa kutoa hoja za maana, si kejeli na matusi na niseme Wanapotukana Rais, wanatudhalilisha sisi sote. Acheni siasa za matusi.”
Rais Samia ameendelea kupokea pongezi kutoka kwa wananchi wa makundi mbalimbali nchini, kufuatia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na msimamo wake wa kudumisha amani, umoja wa kitaifa na usawa wa kijinsia.
By Mpekuzi
Post a Comment