TUMBAKU NA UFUTA VYA PAMBA MOTO RUVUMA, MINADA KUANZA RASMI NAMTUMBO |Shamteeblog.


Katibu Tawala Mkoa Marry Makondo akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas leo katika Ukumbi wa Chandamali Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Ushirika wa Mazao Namtumbo Songea
Baadhi ya wakulima waliojitokeza katika Mkutano wa 22 wa mazao Songea Namtumbo Mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro Songea – Ruvuma

Uzalishaji wa mazao ya biashara mkoani Ruvuma umeendelea kushamiri, ambapo zao la tumbaku limeongezeka kutoka tani 1,664 mwaka 2023/2024 hadi kufikia tani 2,053 kwa msimu wa 2024/2025. 

Kwa upande wa ufuta, uzalishaji umefikia tani 5,538 huku matarajio yakiwa ni kuvuna hadi tani 10,000 msimu wa 2025/2026. 

Mafanikio haya yanatokana na mfumo wa stakabadhi gharani unaoendelea kuimarika na kupanda kwa bei ya mazao ya kibiashara kama ufuta, mbaazi na soya.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 22 wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Mazao Songea Namtumbo (SONAMCU) uliofanyika Mei 28, 2025 mjini Songea, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Mary Makondo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, ameeleza kuwa mkoa unajivunia mchango wa SONAMCU katika kukuza uchumi wa wakulima na mkoa kwa ujumla. 

Ameeleza kuwa chama hicho kimekuwa chachu ya maendeleo kupitia usimamizi wa masoko na uzalishaji wa mazao ya biashara.

Katika hatua nyingine, Makondo ametangaza kuwa msimu mpya wa minada ya ufuta utaanza rasmi kesho, Mei 29, 2025, katika Wilaya ya Namtumbo. 

Amewahimiza wakulima kushiriki kikamilifu ili kupata bei nzuri kupitia mfumo rasmi wa masoko, ambao una lengo la kuwanufaisha wakulima na kukuza kipato chao.

Kwa upande wake, Meneja wa SONAMCU, Juma Mwanga, amesema chama hicho kimejikita katika kuratibu na kusimamia masoko ya mazao ya biashara kupitia mfumo wa stakabadhi gharani. 

Amebainisha kuwa elimu inayotolewa kwa wakulima kuhusu kilimo bora imechangia kuongezeka kwa uzalishaji na mapato kwa wakulima wengi wanaotegemea kilimo kama njia ya maisha.

Mdau wa SONAMCU kutoka Namtumbo, Eleterius Cosmas Mbawala, ameeleza kuwa hali ya kilimo ni nzuri kwa sasa na wakulima wamepata mafanikio makubwa. 

Amesifu mchango wa vyama vya msingi katika kutoa msaada wa pembejeo na ushauri. 

Mbawala pia ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwalipa wakulima kwa kutumia shilingi badala ya dola, akieleza kuwa wengi hawana uelewa wa thamani ya dola, hali inayowapa changamoto katika kufanya maamuzi ya kibiashara.



By Mpekuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post