TAKUKURU RUVUMA YATEKELEZA HATUA MADHUBUTI KUPAMBANA NA RUSHWA, YATOA WITO KWA UCHAGUZI WA HAKI 2025 |Shamteeblog.

Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Ruvuma bi. Janeth Haule akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 30 Mei 2025

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ruvuma imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa kupitia uchambuzi wa mifumo, utekelezaji wa programu za kijamii, uelimishaji wa wananchi, na uchunguzi wa mashtaka ya rushwa. 

Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Ruvuma bi. Janeth Haule amesema jumla ya chambuzi tatu zimefanyika sambamba na warsha tatu zilizoandaliwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali, ambazo zilifanikisha maazimio 16 ya kuziba mianya ya rushwa katika maeneo mbalimbali ya utawala na utoaji huduma.

Katika juhudi za kuwahusisha wananchi moja kwa moja, Takukuru imetekeleza programu katika kata 12 ambapo jumla ya kero 118 ziliibuliwa, kati ya hizo kero 89 zilitatuliwa huku 29 zikiendelea kufanyiwa kazi. 

Aidha, semina 24 zimeendeshwa kwa ajili ya uelimishaji, pamoja na kuimarisha klabu 53 za wapinga rushwa. Pia, mikutano ya hadhara 26, maonesho 6, makala 2 na vipindi vya redio 3 vimefanyika kwa lengo la kufikisha elimu ya kupinga rushwa kwa wananchi kwa njia mbalimbali.

Kwa upande wa uchunguzi wa malalamiko ya rushwa, Takukuru Ruvuma imepokea malalamiko 100 ambapo 80 kati yake yanahusiana moja kwa moja na rushwa na 20 hayakuhusu rushwa. 

Kutokana na uchunguzi huo, kesi nne zimefunguliwa mahakamani, tatu kati ya hizo tayari zimetolewa hukumu na Jamhuri imeshinda zote, jambo linaloashiria ufanisi na umakini katika kushughulikia masuala ya rushwa mkoani humo.

Akizungumza katika hitimisho la taarifa hiyo, Janeth Haule ametoa wito kwa wananchi kujiandaa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa kuepuka kushiriki vitendo vya rushwa. 

Amewataka wananchi kuchagua viongozi waadilifu wasiopatikana kwa njia ya rushwa, ili kuimarisha maendeleo ya taifa na kulinda imani ya wananchi kwa serikali na taasisi zake.



By Mpekuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post