WANANCHI WA NAMANDITI NA RUHUWIKO WAPATA TUMAINI JIPYA LA HUDUMA SAFI YA MAJI |Shamteeblog.

Mhandisi Jafari Kinjalambaya kutoka Ofisi ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA)Mkoani Ruvuma akizungumzia kuhusu mradi unaosubiriwa kutekelezwa wa Namanditi na Ruhuwiko Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma kutoka katika Mfuko wa Wizara ya mipango na fedha.

***

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma

Wananchi wa Namanditi, iliyopo katika Kata ya Ruhuwiko, Manispaa ya Songea, wamekosa huduma ya maji safi kwa muda mrefu hali inayowalazimu kutumia maji ya visima visivyo salama kiafya. 

Wakizungumza kwa masikitiko, wananchi hao wamesema kuwa licha ya ahadi na malengo ya serikali ya kuhakikisha mwanamke hatembei na ndoo kichwani, wao bado hawajawahi kupata huduma ya maji safi kwenye maeneo yao, huku wakitegemea visima ambavyo mara nyingine vina uchafu na kuuzwa kwa maji  gharama kubwa.

Eliza Edward, mkazi wa Namanditi, ameelezea kuwa wanalazimika kununua ndoo ya maji kwa Shilingi 1,000, hali inayowaweka katika mazingira magumu ya maisha. 

Aidha, amedai kuwa baadhi ya maeneo wanayochotea maji si rafiki kiafya kwani kuna ushahidi kuwa watu hutumia maeneo hayo kwa kujisaidia, jambo linalohatarisha afya za wakazi. 

Ametoa wito kwa serikali kuharakisha jitihada za kupeleka huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Namanditi.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Maji kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea Mjini(SOUWASA), Japhary Yahaya Kinjalambaya, amethibitisha uwepo wa changamoto hiyo na kueleza kuwa tayari kuna mpango maalum wa kutoa huduma ya maji kwa Kata ya Ruhuwiko, ikiwa ni pamoja na Namanditi. 

Hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa ukisubiri kibali kutoka Wizara ya Mipango na Fedha ili fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya TIB zitolewe.

Amefafanua kuwa tayari mkopo wa Shilingi Bilioni 1.361 umeidhinishwa kutoka TIB kwa ajili ya mradi huo, kwa riba nafuu ya asilimia 6. 

Fedha hizo zitakapopatikana, hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na ununuzi wa mabomba, uchimbaji wa mitaro, na ulazaji wa mabomba kuanzia eneo la Ruhuwiko C hadi Ruhuwiko Voda, kabla ya kufika Namanditi. 

Changamoto kubwa iliyoibuliwa ni uwezo mdogo wa mabomba ya sasa, ambapo bomba la sasa la nchi 4 haliwezi kukidhi mahitaji ya Namanditi, na linahitajika bomba la nchi 6.

Mhandisi Kinjalambaya ameongeza kuwa michoro ya mradi huo tayari ipo, tathmini imefanyika, na maafisa wa Benki ya TIB wameshatoa idhini baada ya ukaguzi. 

Kinachosubiriwa kwa sasa ni kibali kutoka kwa kamati ya utekelezaji ya wizara husika, ambayo hukutana mara nne kwa mwaka. 

Ameeleza kuwa kucheleweshwa kwa kibali hicho kimesababisha wananchi waendelee kuteseka. 

Mradi huo unafadhiliwa na Mfuko wa Maji unaopata fedha kupitia tozo ya Shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta inayouzwa nchini.


By Mpekuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post