SERIKALI YAANZISHA OPERESHENI KABAMBE KUONDOA WAFUGAJI WALIOINGIA MAENEO YA KILIMO TUNDURU |Shamteeblog.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Denis Masanja akizungumza na wananchi wa kijiji cha Cheleweni kata ya Sisi kwa Sisi kuhusu operesheni kabambe ya kuwaondoa wafugaji wote waliovamia maeneo ya wakulima wilayani Tunduru 

Na Regina Ndumbaro- Tunduru

Serikali wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma, imetangaza kuanza rasmi operesheni kabambe ya kuwaondoa wafugaji wote waliovamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo na uhifadhi. 

Hatua hii inalenga kudhibiti migogoro ya mara kwa mara kati ya wafugaji na wakulima ambayo imekuwa ikisababisha usumbufu kwa wananchi.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Cheleweni, kata ya Sisi kwa Sisi, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Denis Masanja, amesema kuwa operesheni hiyo itaanza rasmi Julai 21, na inalenga kuhakikisha kuwa wafugaji wote wanafuata sheria kwa kufanya shughuli zao kwenye maeneo rasmi ya ufugaji. 

Amesisitiza kuwa baada ya operesheni hiyo, wafugaji watatakiwa kuripoti katika ofisi za serikali za vijiji husika ili kuelekezwa maeneo wanayopaswa kwenda.

Katika hatua ya kudumu ya kutatua migogoro hiyo, Masanja ameeleza kuwa serikali itaunda kamati ya pamoja itakayojumuisha wafugaji, wakulima na baadhi ya wananchi waliopendekezwa na vijiji. 

Kamati hiyo itakuwa na jukumu la kutafuta suluhisho la kudumu la kuzuia muingiliano wa makundi hayo mawili, ambao mara nyingi huibua migogoro mikubwa.

Mkuu huyo wa wilaya ametaja kuwa chanzo kikuu cha migogoro hiyo ni baadhi ya viongozi wa vijiji na wananchi wanaopokea fedha kutoka kwa wafugaji kwa maslahi binafsi na kuwakaribisha kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kwa shughuli za ufugaji. 

Amewaonya kuwa tabia hiyo inachochea migogoro na kuwataka wananchi kuacha kuwapokea watu wasiofahamika kiholela bila kufuata taratibu za kisheria.

Kuhusu changamoto ya miundombinu, Masanja ameahidi kuwa serikali itashughulikia tatizo la barabara inayounganisha kijiji cha Cheleweni na makao makuu ya kata ya Sisi kwa Sisi, ambayo imeharibiwa vibaya na mvua za masika. 

Amesema ukarabati huo utafanyika haraka ili kurudisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa eneo hilo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Chiza Marando, ameeleza kuwa jumla ya vitalu 221 tayari vimetengwa kwa ajili ya wafugaji, hivyo amewataka wafugaji waondoke katika maeneo ya wakulima na kuelekea kwenye vitalu hivyo vilivyopangwa rasmi.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Cheleweni, Mustafa Ponera, amefafanua kuwa kutokana na ubovu wa barabara, wananchi hulazimika kutembea kwa miguu zaidi ya kilometa 7 hadi kijiji cha Sisi kwa Sisi kufuata magari ya usafiri kwenda Tunduru mjini. 

Amesema wamiliki wa magari wameacha kabisa kupeleka magari yao kijijini hapo kwa kuhofia kuharibika kutokana na hali mbaya ya barabara hiyo.

Katika kutatua tatizo hilo, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Tunduru, Silvanus Ngonyani, amebainisha kuwa serikali imetenga kiasi cha Shilingi milioni 155 kwa ajili ya ukarabati wa barabara hiyo. 

Ameahidi kuwa kabla ya mwezi Agosti, barabara zote zenye changamoto zitafanyiwa matengenezo, huku akiwaomba wananchi kuwa wavumilivu.

Mkuu wa Wilaya Masanja amewasihi wananchi kushirikiana na serikali katika ujenzi na utunzaji wa miradi ya maendeleo kama vile vyumba vya madarasa, badala ya kuiachia serikali pekee jukumu hilo, kwani maendeleo ni jukumu la kila mmoja.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post