MAPINDUZI YA KOROSHO TUNDURU-MAAFISA UGANI 50 WAPATIWA PIKIPIKI KUINUA KILIMO |Shamteeblog.

Pikipiki 50 zilizotolewa kwa maafisa ugani katika harakati za kuinua uchumi Wilayani Tunduru kutoka kwa BBT Korosho 

Na Regina Ndumbaro-Tunduru

Katika kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa na tija kwa wakulima, Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma imepokea jumla ya pikipiki 50 zilizotolewa kwa maafisa ugani wa BBT Korosho. 

Mkuu wa Wilaya hiyo, Denis Masanja, ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya awamu ya sita wa kuimarisha huduma za ugani, kuongeza uzalishaji na ubora wa zao la korosho kuanzia msimu wa 2025/2026. 

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vyombo hivyo vya usafiri, Masanja ameeleza kuwa uwezeshaji huo utasaidia maafisa kuwafikia wakulima kwa urahisi zaidi ili kuwapa elimu na ushauri wa kitaalamu.

Masanja amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa katika kuinua kilimo, akisema kuwa hatua hiyo ni uthibitisho wa namna anavyowajali watendaji na wakulima wa nchi hii. 

Amesisitiza kuwa pikipiki hizo hazipaswi kutumika kinyume na malengo yaliyokusudiwa, bali zitumike kuongeza tija katika uzalishaji wa korosho – zao ambalo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tunduru.

 Aidha, ametoa wito kwa maafisa ugani kuzitumia pikipiki kwa weledi, uwajibikaji na bidii ili kuleta mageuzi chanya katika sekta hiyo

Kwa upande wake, Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania – Tawi la Tunduru, Shauri Makiwa, amesema program ya BBT Korosho inalenga kuwawezesha vijana waliobobea katika kilimo kushughulikia changamoto za uzalishaji wa korosho. 

Amebainisha kuwa tayari maafisa 50 wamepangiwa kazi katika kata zote za Wilaya ya Tunduru na kuwa uwepo wao umesaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto kama matumizi sahihi ya viuatilifu.

 Makiwa amesisitiza kuwa pikipiki hizo ni sehemu ya ahadi ya kuwapatia vitendea kazi ikiwemo vishikwambi ili kuimarisha utendaji kazi wa maafisa hao.

Pascal Kaguo, mmoja wa maafisa ugani waliopokea pikipiki, ameeleza kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria na imetatua kilio cha muda mrefu cha maafisa ugani waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya usafiri. 

Amesema kuwa sasa watakuwa na uwezo mkubwa wa kuwahudumia wakulima kwa karibu zaidi na kuboresha uzalishaji wa zao la korosho.

 Serikali imedhamiria kufanikisha lengo la kuzalisha tani 700,000 za korosho kwa mwaka, kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Denis Masanja akiwa amepanda  moja ya pikipiki zilizotolewa kwa maafisa ugani Wilayani Tunduru 



By Mpekuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post