
Na Deogratius Koyanga, Hanang’ DC
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, Bi. Teresia Irafay, amesema kuwa Halmashauri yake imejipanga kuhakikisha mchakato wa maandalizi ya mipango na bajeti unazingatia usawa wa kijinsia ili kuboresha huduma za afya, maji na usafi wa mazingira katika jamii.
Akizungumza wakati wa kufunga warsha ya siku mbili ya kuwawezesha wanawake viongozi wa vijijini kuhusu masuala ya afya, maji na usafi wa mazingira (WASH), iliyoandaliwa na shirika la WaterAid Tanzania katika mradi wa Afya ya Mwanamke sasa, Bi. Irafay alisema kuwa Halmashauri itaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika kupanga na kufuatilia utekelezaji wa huduma hizi muhimu.
Warsha hiyo iliyofanyika Hanang’ na kushirikisha jumla ya washiriki 47, ililenga kuwajengea uwezo wanawake viongozi kutoka serikali za vijiji katika kuelewa kwa kina dhana ya huduma bora za afya, maji na usafi wa mazingira, kutambua changamoto zilizopo na namna ya kuziorodhesha kwenye mipango ya maendeleo kupitia mchakato wa O&OD (Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo), pamoja na kujiamini kufuatilia utekelezaji wake kupitia mikutano ya kijiji na kata.
Bi. Irafay alieleza kuwa tayari amemwagiza Afisa Mipango wa Halmashauri kuhakikisha mahitaji ya jamii yanayoibuliwa kupitia O&OD, hasa yale yanayowahusu wanawake, wazee, watoto na watu wenye ulemavu, yanapewa uzito unaostahili.
Alisisitiza kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/27, Halmashauri itahakikisha maeneo ya maji na usafi wa mazingira yanawekwa kwenye vipaumbele, sambamba na kutenga bajeti kwa ajili ya kutoa elimu ya kijinsia kwa jamii ili kuondoa vikwazo vya kihistoria vinavyowazuia wanawake kunufaika kikamilifu na huduma hizi.
Katika warsha hiyo, wanawake walijifunza mbinu shirikishi za kupanga maendeleo ya jamii, namna ya kutumia nafasi zao kushawishi maamuzi ya maendeleo kwenye mikutano rasmi, na mikakati ya pamoja ya kuhamasisha jamii kushiriki katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya WASH kwenye vituo vya afya, shule na maeneo ya makazi.
Bi. Irafay alibainisha kuwa dhamira ya Halmashauri ni kuhakikisha kuwa mtoto wa kike wa Hanang’ anapata elimu katika mazingira salama, yenye miundombinu rafiki, hasa wakati wa hedhi.
Aliongeza kuwa katika mwaka ujao wa fedha, Halmashauri itaweka bajeti ya kuboresha vyoo shuleni, kuweka maji ya uhakika, na kutoa elimu ya afya ya uzazi na hedhi salama kwa wanafunzi wa kike ili waweze kusoma bila vikwazo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sera, Ushawishi na Utetezi, kutoka shirika la WaterAid Tanzania, Bi. Christina Muhando, alisema kuwa taasisi yao itaendelea kushirikiana na serikali katika kujenga uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa huduma jumuishi za WASH.
Alisema kuwa WaterAid kwa kushirikiana na wadau kama TGNP imekuwa ikitekeleza miradi ya kuongeza uelewa wa kijinsia katika WASH kwa kuhakikisha kwamba wanawake, wazee, watoto na watu wenye ulemavu wanapewa nafasi sawa ya kushiriki na kunufaika.
Bi. Muhando alieleza kuwa elimu inayotolewa kupitia programu za WaterAid imeanza kuleta mabadiliko chanya ya kijamii ambapo wananchi wengi sasa wamehamasika kujitokeza kuboresha miundombinu ya maji, vyoo na huduma za afya katika maeneo ya wazi na kwenye makazi yao.
Kwa mujibu wa ripoti ya WaterAid ya mwaka 2023, takriban asilimia 40 ya vituo vya afya nchini Tanzania havina huduma ya maji ya uhakika, hali inayoweka maisha ya wanawake wajawazito na watoto wachanga katika hatari kubwa.
Hali hiyo inaenda kinyume na malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 6) yanayolenga kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na usafi kwa wote ifikapo mwaka 2030. Vilevile, Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002, Sera ya Afya ya mwaka 2007, na miongozo ya TAMISEMI kuhusu ushirikishwaji wa jamii katika upangaji wa maendeleo, zinatoa mwongozo wa wazi kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya kijinsia katika upangaji wa huduma za jamii hususan sekta ya WASH.
Warsha hiyo ilizaa maazimio ya vitendo ya kuunda mitandao ya wanawake viongozi kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji, afya na usafi wa mazingira, pamoja na kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu wajibu wao katika kuhakikisha huduma bora zinapatikana.
Wanawake walisisitiza kuwa watatumia nafasi zao katika Kamati za Maendeleo ya Vijiji (VDCs) na mikutano ya kijiji kuhoji uwajibikaji na kushawishi upangaji wa bajeti jumuishi zinazojibu mahitaji ya makundi yote katika jamii.
Kwa kuzingatia vipaumbele vya taifa na mikataba ya kimataifa, kama vile Mkataba wa CEDAW na Azimio la Beijing, warsha hii inadhihirisha kuwa uwekezaji katika uongozi wa wanawake vijijini ni nguzo muhimu ya kufanikisha huduma jumuishi na endelevu za afya, maji na usafi wa mazingira.
Kama alivyosema Bi. Irafay, “Tunahitaji kuona mtoto wa kike wa Hanang’ akisoma vizuri shuleni, apate mahitaji muhimu ili atulie darasani. Tutaendelea kuboresha mazingira ya kutolea elimu na huduma za afya kupitia miundombinu rafiki ya WASH katika jamii yetu.”
Kupitia ushirikiano kati ya serikali na mashirika ya kiraia, kama WaterAid na TGNP, mafanikio haya ni dalili kuwa mabadiliko yanawezekana, endapo wanawake watawezeshwa na kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa maendeleo.
By Mpekuzi
Post a Comment