TANZANIA NYUMBA YETU: VIJANA WAASWA KUTUMIA MAZUNGUMZO KUJENGA, SI KUCHOMA NCHI |Shamteeblog.

Wakati juhudi za baadhi ya watu wachache zikielekezwa katika kuhamasisha vurugu na maandamano yasiyo na kibali, viongozi wa kisiasa na jumuiya za vijana wameungana kuwasisitiza Watanzania, hususan vijana, kwamba wajibu wao mkuu ni kuifanya Tanzania kuwa mahali bora pa kuishi kupitia njia za busara, umoja na mazungumzo, na si kwa kuichoma nchi.

Mwanasiasa Peter Daffi alisisitiza kuwa Serikali haiwezi kuruhusu maandamano yasiyo na kibali, akionya kuwa hatua hiyo inaweza kuifanya dunia kushangaa kwa nini Watanzania wanashindwa kukaa, kuzungumza na kukubaliana kama taifa.

"Mnataka turuhusu tena hali ya kushangaza duniani kwamba tumeshindwa kukaa na kuzungumza na kukubaliana?" alihoji Daffi, akisisitiza kwamba juhudi za kuhamasisha vurugu hazikubaliki kwani zinahatarisha usalama wa watu na mali.

Daffi aliwaelekeza wananchi kutumia njia sahihi zilizowekwa na Serikali ili kufikia maridhiano. Alisema waliotaka kutoa maoni yao tayari wametengewa nafasi kupitia Tume iliyoanzishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Rais ameunda tume. Ile tume sasa tuiisikilize ili itekeleze yale tunayodhania na tunayotamani yafanyike," alisema Daffi. Alisisitiza kuwa Tume hiyo ndiyo njia sahihi ya kusikiliza maoni ya wananchi, na kwamba wananchi wanapaswa kutoa maoni yao wanapofika kwenye maeneo mbalimbali ili Serikali iweze kutekeleza wanayoyahitaji.

Vijana Kujenga, Sio Kubomoa

Kauli za wanasiasa ziliungwa mkono na ujumbe mzito kutoka kwa jumuiya ya vijana, wakisisitiza kwamba nguvu za vijana ni za kujenga, si kubomoa. Ujumbe huo uliwakumbusha vijana kuwa Tanzania ni urithi pekee wa thamani unaohitaji kulindwa.

"Tuchague busara, umoja na ustaarabu tunapotafuta 'HAKI' si hasira, wala kutumia vurugu," ulisema ujumbe huo.

Wito huu unaakisi kuongezeka kwa ushiriki wa vijana katika Bunge na katika nafasi za uongozi. Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha, Cecilia Paresso (CCM), ambaye pia ni kijana, alisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii ili kumsaidia Rais Samia kufikia azma yake ya kuacha tabasamu kwa Watanzania ifikapo 2030, akisimamia misingi ya kazi na utu.

Vijana walisisitizwa kutokuwa chombo cha kuchochewa, kupandikizwa chuki na kufuata mkumbo. Badala yake, wanapaswa kuwa walinzi wa utulivu na mshikamano. Tanzania ni nyumba yetu sote; hatuna nyingine.

Wito kwa Taasisi za Dini

Kama nguzo muhimu, taasisi za dini nazo ziliaswa kuendelea kuwa daraja la upatanisho na si ukuta unaowatenganisha raia na viongozi wao. Waliombwa kutumia maneno yao kuleta matumaini na kurejesha mioyo iliyokata tamaa.

Kwa ujumla, ujumbe mkuu kwa taifa ni kwamba ulinzi wa amani na juhudi za kujenga nchi bora zinapaswa kupitia mazungumzo na taasisi rasmi, huku kila hatua ikielekezwa katika kuijenga Tanzania tunayotaka kuiona kesho.




By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post