Na Sumai Salum -Kishapu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Josephat Limbe, amefanya ziara ya kikazi Februari 19, 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa lengo la kukagua utoaji wa huduma na kuzungumza na watumishi wa afya.
Katika ziara hiyo, Mhe. Limbe amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya afya kupitia maboresho ya miundombinu na upatikanaji wa vifaa tiba, hali inayowezesha wananchi kupata huduma bora karibu na maeneo yao.
Aidha, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Emmanuel Johnson, kwa usimamizi madhubuti wa fedha za Serikali uliowezesha utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo na kuinua kiwango cha huduma hospitalini hapo.
Akizungumza na watumishi wa hospitali, Mhe. Limbe amewahimiza kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya taaluma zao, kutoa huduma kwa wakati, kushirikisha jamii kwa kuwapa elimu ya afya na kulinda heshima ya taaluma zao.
“Nimeridhishwa na jinsi mnavyotoa huduma kwa wateja wenu licha ya kuwa jukumu la kuponya mlilonalo ni gumu na zito. Ninawapongeza sana,” amesema Mhe. Limbe.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Mohamed Ally Mkumbwa, ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya utoaji wa huduma za afya na kuomba kuendelea kuboreshwa kwa mazingira ya kazi kwa watumishi wa afya.
Dkt. Mkumbwa amesema hospitali hiyo kwa sasa ina wodi tano za kulaza wagonjwa ambazo ni wodi ya wanawake, wanaume, watoto, wazazi pamoja na wodi ya watoto wachanga mahututi (NCU), ikiwa na jumla ya vitanda 156.
Ameeleza kuwa huduma zinazotolewa ni pamoja na huduma za meno, macho, dharura, upasuaji, maabara, kuhifadhi maiti, kulaza wagonjwa, mazoezi ya viungo, huduma za baba, mama na mtoto (RCH), ustawi wa jamii, kliniki ya CTC, huduma za mawimbi ya sauti (Ultrasound), huduma za mionzi (X-Ray) pamoja na huduma za dawa.
Kwa mujibu wa Dkt. Mkumbwa, maboresho hayo yamechangia kupunguza vifo vya wajawazito kutoka vifo sita mwaka 2021 hadi kifo kimoja mwaka 2025, huku vifo vya watoto chini ya miaka mitano vikishuka kutoka 24 mwaka 2021 hadi sita mwaka 2025.
Ameongeza kuwa kwa juhudi za Serikali na wadau mbalimbali, hospitali imefanikiwa kuongeza majengo hadi kufikia 20, hatua inayoimarisha zaidi utoaji wa huduma.
Akizungumza katika kikao hicho, kwa niaba ya Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu. Gabriel K. Pastory ambaye ni Afisa tawala Ofisi ya Mkurugenzi, amewasisitiza watumishi kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia miongozo, kanuni, sheria na taratibu za utumishi wa umma. Amesema kuwa nidhamu na ufuataji wa taratibu ni msingi wa utoaji wa huduma bora na endelevu kwa wananchi.
Gabriel ameongeza kuwa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji itaendelea kuwa karibu na watumishi hao, kuwapa ushirikiano unaohitajika na kuhakikisha wanapata mazingira wezeshi ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Naye Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Pius Mwandu, amesema kutokana na utendaji mzuri wa watumishi wa hospitali hiyo, Mbunge wa Jimbo hilo, Lucy Mayenga, atafanya jambo maalum la kuwapongeza na kuwatia moyo ili waendelee kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Pius Mwandu, akizungumza kwenye ziara ya kikazi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Josephat Limbe Februari 19, 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa lengo la kukagua utoaji wa huduma na kuzungumza na watumishi wa afya
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Dkt. Mohamed Ally Mkumbwa, akizungumza kwenye ziara ya kikazi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Josephat Limbe Februari 19, 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa lengo la kukagua utoaji wa huduma na kuzungumza na watumishi wa afya
Gabriel K. Pastory Afisa tawala Ofisi ya Mkurugenzi, akizungumza kwenye ziara ya kikazi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Josephat Limbe Februari 19, 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa lengo la kukagua utoaji wa huduma na kuzungumza na watumishi wa afya
Mteknolojia wa mionzi Hospital ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Wilaynai Kishapu mkoani Shinyanga Efraim M. Isaya
Mteknolojia wa maabara Hospital ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Wilaynai Kishapu mkoani Shinyanga Salum Idd Mwinyibweni




By Mpekuzi
Post a Comment