SERIKALI YAIMARISHA HUDUMA NA MAZINGIRA MAKAZI YA WAZEE |Shamteeblog.



Na Jackline Minja, WMJJWM Dar Es Salaam

Serikali imeendelea kuimarisha huduma na mazingira katika Makazi ya Wazee na Wasiojiweza kwa lengo la kuhakikisha wazee wanaishi kwa heshima, usalama na kupata huduma stahiki za kijamii na afya.

Hayo yamesema na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi tarehe 20, Februari 2026 wakati alipotembelea Makazi ya wazee Nunge yaliyopo Kigamboni, mkoani Dar Es Salaam kwa lengo la kujionea hali ya utoaji wa huduma na kusikiliza changamoto zinazowakabili wazee wanaoishi katika kituo hicho.

Mhandisi Mahundi amesema Serikali inawatambua Wazee kama tunu, hazina ya hekima na msingi wa maadili ya Taifa hivyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya kuishi kwa Wazee, hususan wale walio katika mazingira hatarishi na wasiokuwa na msaada wa familia.

“Ndugu zangu nipende kusema Serikali inawatambua Wazee kama tunu, hazina ya hekima na msingi wa maadili ya Taifa letu, Tunathamini mchango wenu mkubwa walioutoa katika ujenzi wa familia, jamii na Taifa na tutaendelea kuhakikisha wanaishi kwa heshima, usalama na utu wanaostahili ni ukweli usiopingika kuwa kuzeeka ni hatua ya maisha ambayo kila mmoja wetu anaelekea kuifikia na kufikia uzee ni neema kubwa ya Mwenyezi Mungu,” amesema Mhandisi Mahundi.

Kwa upande wake, Mfawidhi wa Makazi ya Wazee Nunge, Jacklina Kanyamwenge, amesema kituo hicho kinaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wazee ikiwemo malazi, lishe na huduma za afya kwa lengo la kuhakikisha ustawi wao unaimarika.

“Tunawahudumia wazee hawa kwa kuwapatia mahitaji yao muhimu ya kila siku na tunaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuboresha zaidi huduma na mazingira ya makazi haya ili yaendane na mahitaji yao,” amesema Jacklina.

Nao Baadhi ya wazee wanaoishi katika makazi hayo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapatia matunzo na huduma muhimu, wakisema hatua hiyo imewapa faraja na kuwafanya waishi kwa matumaini na amani.




By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post